ANGALIA LIVE NEWS

Monday, April 25, 2011

‘Ndiyo’ ya Pinda Ilivyotunisha misuli Upinzani bungeni

Image
MAKOFI mazito mezani, ndicho pekee kilikuwa kiashiria na namna wabunge wa Kambi ya Upinzani bungeni, walivyofarijika, kwa jibu la Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alipomuunga mkono Mbunge wa Singida Mashariki, wakili machachari, Tundu Lissu (Chadema) hivi karibuni. 

Kauli ya Pinda aliyoirudia mara tatu, iliwaacha midomo wazi baadhi ya Wabunge wa chama tawala – Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku wengine wakijilazimisha kuamini kuwa jibu hilo alilitoa kuwatia moyo wapinzani. 

Pinda aliunga mkono marekebisho ya kuingiza mapendekezo ya Lissu, kutaka wakuu wa mikoa na wilaya wasiwepo katika Kamati za Maadili za Wilaya za Mahakama, kwa kile alichosimamia kuwa wanateuliwa na Rais ambaye ni Mwenyekiti wa CCM, hivyo wakuu hao ni makada wa chama hicho.
 

Kamati hizo ni zile zinazosimamia maadili ya mahakimu, kama inavyopendekezwa katika kifungu cha 50 cha Muswada wa Sheria ya Utawala wa Mahakama wa mwaka 2011, uliowasilishwa bungeni na Serikali na kupitishwa katika Mkutano wa Tatu wa Bunge mjini Dodoma hivi karibuni. 

Lissu alitaka kifungu hicho, kirekebishwe kwa kuwaondoa wakuu hao ; na badala yake awepo mwakilishi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS). 

Baada ya Spika, Anne Makinda, kuuliza wanaoafiki marekebisho ya Lissu, waseme ‘Ndiyo’ na wasioafiki waseme ‘hapana’, sauti zilisikika kuwiana. Ndipo Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema), alipoomba mwongozo wa Spika na kutaka kura za kuulizwa mbunge mmoja mmoja zipigwe. 

Spika aliridhia pendekezo la Zitto ; na kura zilianza kupigwa, kwa kuanza kumuuliza Waziri Mkuu, ambaye ni Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni. Pinda alipoulizwa, alisema ‘ndiyo’, akionesha kuwa anakubaliana na mapendekezo ya Lissu, kuingizwa katika muswada huo. 

Wabunge wa upande wa Upinzani, walishangilia kiasi cha kusababisha Spika, arudie swali kwa Pinda mara tatu, ambapo mara ya tatu Waziri Mkuu, huku akiwa amesimama alisema; “Nimesema Ndiyo” . Jibu hilo liliwaacha mawaziri na wabunge wa CCM, wakishangaa, kutokana na ukweli kwamba walitegemea jibu la ‘siyo’. 

Kura hizo za ‘ndiyo’ au ‘hapana’, zilipigwa wakati Bunge lilipokaa kama Kamati, kupitia kifungu kimoja baada ya kingine cha muswada huo wa sheria ya uendeshaji wa Mahakama wa mwaka 2011, unaosubiri sasa rais ausaini, ili uwe Sheria. 

Pinda aliposema ‘ndiyo’, Zitto alisimama na kumpongeza. Lakini, ghalfa alisimama Spika Makinda ; na kueleza kuwa hakusikia jibu la Pinda, hivyo alimuuliza tena. Waziri Mkuu alirudia kusema ‘ndiyo’. Jibu hilo liliamsha hisia kwa wabunge wa upinzani, ambao hukaa upande wa kushoto kwa Spika. 

Hali hiyo ilisababisha upande wa kulia waliko wabunge wa CCM, ambao ni wengi zaidi, kuduwaa kwa dakika chache. 

Nje ya Bunge, Zitto ambaye ni Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alisema jibu la Waziri Mkuu, linadhihirisha kuwa mapendekezo ya Upinzani, yanakubalika na yana msingi, lakini kutokana na uchache wao, yanakosa nguvu ya kusababisha yapite. 

Baada ya ‘ndiyo’ ya Pinda, baadhi ya wabunge wa CCM, walisema ‘ndiyo’ lakini walipoulizwa mara ya pili, walisema ‘siyo’, akiwemo Mbunge wa Viti Maalumu, Angelah Kairuki, anayewakilisha kundi la Wafanyakazi. 

Hata hivyo, pamoja na nia njema ya Waziri Mkuu kumuunga mkono Lissu, matokeo ya kura yaliwagaragaza wapinzani, ambapo Spika alipotangaza, alisema waliosema ‘ndiyo’ wakiwa upande wa Lissu akiwemo Pinda ni 69 ;na siyo ni 152, hivyo ushindi kupatikana kwa waliosema ‘siyo’. 

Hata hivyo, kura hizo za mmoja mmoja kuulizwa, zilipigwa na wabunge 122 pekee, kati ya wabunge 350 waliopaswa kuwepo bungeni. Spika alionesha kukerwa na idadi ya wabunge 128, kutokuwepo bungeni wakati huo.


CHANZO:MAJIRA 

No comments: