Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kilitangaza zawadi ya gari ndogo aina ya Toyota lenye thamani ya Sh Milioni 13 kwa mshindi wa tuzo ya ‘Mwanamichezo Bora wa Tanzania 2010’ itakayotolewa Mei 6 jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto, alisema kuwa hafla ya kukabidhi tuzo hiyo iliyodhaminiwa na Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), itafanyika kwenye ukumbi wa hoteli ya Movenpic jijini Dar es Salaam, ambao nao ni miongoni mwa wadhamini wenza.
Alisema kuwa mbali na tuzo ya gari kwa mwanamichezo bora wa mwaka, washindi mmoja mmoja wa vipengele zaidi ya 15 watapata zawadi ya Sh. Milioni Moja kila mmoja.
“Kama tulivyosema, tuzo zetu mwaka huu zina mabadiliko makubwa na tunawashukuru wadhamini kwa kutusaidia kuboresha tuzo hizi,” alisema Pinto.
Mbali na zawadi hizo, hoteli ya Movenpic imetoa zawadi ya kulala siku moja katika chumba cha hadhi ya juu hotelini kwao kwa mwanamichezo bora wa mwaka.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa SBL, Teddy Mapunda alisema kuwa kampuni yake imeamua kuboresha zawadi za washindi ikiwa ni njia mojawapo ya kuthamini michezo nchini. Kampuni hiyo imetoa Sh. Milioni 80 kwa ajili ya kudhamini tuzo za mwaka huu.
Wanamichezo 12 waliowahi kushinda tuzo ya mwanamichezo bora wa mwezi katika kipindi cha mwaka 2010/2011, watapigiwa kura kumpata mshindi wa tuzo ya mwaka.
Tuzo za TASWA za wanamichezo bora wa mwaka kuanzia mwaka 2006 zilishatwaliwa na Samson Ramadhan, Martin Sulle (2007), Mary Naali (2008) na mwanariadha Mwanaid Hassan aliyeibuka kidedea mwaka 2009 na kutwaa zawadi ya juu zaidi tangu tuzo hizo zianzishwe ya Sh 700,000.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment