ANGALIA LIVE NEWS

Friday, April 22, 2011

Ufisadi: CCM Dar yamvaa mbunge

 Wamlima barua
  Ni baada ya kuishushia tuhuma nzito
Mbunge wa Kinondoni, Iddi Azzan
Ule moto wa kuwababua mafisadi uliokolezwa Dodoma katika vikao vya Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi na hatimaye kubarikiwa na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho, sasa umelipuka mkoani Dar es Salaam kwa staili ya aina yake.
Mlipuko wa Dar es Salaam ulichochewa na Mbunge wa Kinondoni, Iddi Azzan, kwa kuitaka Halmashauri ya CCM mkoani humo ijivue gamba kama ambavyo Sektretarieti na Kamati Kuu za CCM zilivyofanya kwa kujiuzulu, sasa umeelekezwa kwake baada ya kupewa barua kutakiwa kujieleza juu ya tuhuma hizo.

Taarifa ambazo NIPASHE imezipata na kuthibitishwa na Azzan mwenyewe, barua hiyo inadawa kuwa ni mkakati wa kumkata makali mbunge huyo ambaye ameapa kuanika ufisadi wa uongozi wa CCM mkoa kama hautaitisha kikao kujadili madudu hayo.
Habari ambazo NIPASHE imezipata zinaeleza kuwa Azzan alipewa barua hiyo juzi ambayo iliandikwa na Katibu wa chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam, Kilumbe Ng’enda.
Hata hivyo, Azzan hakutaka kueleza yaliyomo kwenye barua hiyo kwa madai kuwa ni siri, ingawa taarifa zaidi zinasema kwamba ameitwa kujieleza kufuatia tuhuma alizozitoa dhidi ya Sekretarieti ya mkoa huo.
Jumatatu wiki hii, Azzan alisema Halmashauri ya CCM Mkoa wa Dar es Salaam imechafuka kwa ufisadi.
Kutokana na hali hiyo, Azzan aliipa siku 10 kuitisha kikao kwa ajili ya kujadili tathmini ya mwenendo mzima wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 31, mwaka jana vinginevyo atawalipua kwa kuanika madudu yanayofanywa watendaji wake.
Kadhalika, Azzan alidai kutishiwa maisha na watu wasiofahamika baada ya kuitaka sekretarieti ya mkoa huo ijivue gamba.
Mbunge huyo aliitaka sekretarieti ya mkoa kujivua gamba mjini Dodoma baada ya kumalizika kwa vikao vya CCM vya Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na kuamua kujivua gamba ili kukirejesha chama katika misingi yake ya awali.
Azzan alisema kuwa mpaka sasa Halmashauri ya mkoa haijafanya kikao chochote na hakuna matarajio ya kuitisha kikao licha ya katiba kuwataka kufanya hivyo.
Alikwenda mbali zaidi kwa kuitaka sekretarieti hiyo ijiuzulu vinginevyo aliahidi kuanika uozo unaofanywa na wajumbe hao baada ya siku 10.
Alisema viongozi wa mkoa wamekuwa na utendaji mbovu hali ambayo ilisababisha kuwepo makundi ndani ya CCM tangu mwaka 2007 ulipofanyika uchaguzi wa ndani wa chama.
“Kuna makundi mawili yamegawanyika ndani ya chama hali ambayo ilisababisha kuchukuliwa kwa majimbo yetu kwani walikuwa wanafanya ufisadi mkubwa wa kuwaweka watu wao wagombee wakati hawakuwa chaguo la wananchi,” alisema.
Alisema kitendo hicho cha kujichagulia watu wao kimesababisha kwa asilimia kubwa kura nyingi kwenda upinzani kutokana na wanachama wa CCM kuwapigia kura wagombea wa upinzani baada ya kuwekewa wagombea ambao hawakubaliki.
“Kwa upande wangu walinifanyia uchakachuaji, lakini walishindwa tena sekretarieti ya Mkoa wa Dar es Salaam ilitaka nianguke katika Uchaguzi Mkuu ila nashukuru wananchi waliniokoa kwa kunipitisha kwa asilimia kubwa,” alisema.
Azzan alisema alinyimwa hata vifaa vya uchaguzi katika jimbo lake hali ambayo ilimsikitisha na kwamba hata alipojaribu kuulizia suala hilo alikuwa akipatiwa taarifa za vitisho.
“Majimbo ya wenzangu kama la Kawe, Ubungo na mengineyo walipatiwa fulana 5,000 pamoja na kofia, lakini mimi hawakunipatia. Nikasikia kuwa zimepelekwa katika Jimbo la Kilwa wakati mgombea wa huko alishapatiwa...yapo mambo mengi na nitayaanika wasipofanya kikao hicho,” alisema.
Alisema sekretarieti ya mkoa inatakiwa kujivua gamba kwani wajumbe wake wamekuwa wakifanya ufisadi mkubwa wa kukiangamiza chama kutokana na kujali maslahi yao binafsi.
Alisema amelazimika kusisitiza msimamo wake kwa kuwa amekuwa akipigiwa simu za vitisho pamoja na ujumbe mfupi (SMS) kutoka kwa watu asiowajua baada ya kauli yake ya hivi karibuni aliyoitoa mjini Dodoma na kuitaka CCM Mkoa wa Dar es Salaam nayo ijivue gamba.
“Mimi siogopi vitisho wanaogopa kuitisha hicho kikao kutokana na kwamba wanayajua waliyoyafanya katika Uchaguzi Mkuu, lakini wasipoitisha kikao mwezi ujao nitaanika hadharani mambo yote waliyoyafanya,” alisema.
Ng'enda alipoulizwa kuhusu tuhuma zilizotolewa na Azzan dhidi ya chama hicho mkoa na hatua ya kumwandikia barua, alikataa kutoa ufafanuzi.
Ng’enda alisema kuwa hawezi kuzungumza jambo lolote kutokana kuwa tayari habari hizo zimeshaandikwa.
“Mimi siwezi kusema chochote kuhusiana na suala hilo kwani nyie mmeshaandika taarifa hiyo mngetakiwa mnitafute kabla ya kuandika habari hizo mlizopatiwa,” alisema Ng'enda.
CHANZO: NIPASHE

No comments: