ANGALIA LIVE NEWS

Friday, April 22, 2011

Majambazi yamuua kwa risasi mfanyabiashara wa madini

Kundi la watu wanaosadikiwa kuwa majambazi wakiwa na silaha za moto, wamemuua mfanyabiashara wa madini ya dhahabu, Mwita Shibota (28), mkazi wa kijiji cha Nyangoto wilayani humu.
Majambazi hayo yalimvamia mfanyabiashara huyo usiku wa kuamkia Aprili 19, mwaka huu akiwa amelala nyumbani kwake baada ya kuvunja mlango wa nyumba yake kwa kutumia jiwe maarufu kama `fatuma'.
Baada ya kuingia ndani ya nyumba yake, walimpiga risasi begani na kufa papo hapo kisha wakapora dhahabu ambayo thamani yake haifahamika na kutoweka nayo.

Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya, Costantine Massawe, alisema baada ya majambazi hayo kuua na kupora dhahabu hiyo, yalikutana na mkulima wa kijijini Nyangoto, Ramadhan Chacha (25), na kumjeruhi kwa kumkata mapanga mguuni.
Majeruhi huyo kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya Mkoa ya Musoma akiendelea na matibabu.
Majeruhi mwingine aliyejeruhiwa na majambazi hayo wakati wakitoka katika tukioni Joseph Nyanda (25) aliyekutana nao wakati akienda nyumbani kwake karibu na mto Tigite ambapo walimsimamisha na kumpiga risasi kifuani.
Nyanda amelazwa katika Hospital ya Wilaya Tarime ingawa na hali yake si nzuri kwa mujibu wa Kamanda Massawe.
Kamanda Massawe ametoa rai kwa wakazi wa wilaya za Tarime na Rorya kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ama kwa viongozi wa serikali waliopo vijijini wanapowahisi watu wabaya.
CHANZO: NIPASHE

No comments: