Sakata la mama aliyejifungua mapacha na kufa katika Zahanati ya COH ya Ukonga Mazizini, jijini Dar es Salaam, limezidi kuchukua sura mpya baada ya Baraza la Wauguzi na Wakunga nchini (TNMC), kubaini siri nzito kwa muuguzi wa zahanati hiyo anatumia vyeti visivyokuwa vyake.
Msajili wa Baraza hilo, Gustav Moyo, alisema uchunguzi wa kashfa hiyo umebaini kuwa muuguzi huyo, Selustina Kondamwali, anatumia vyeti visivyokuwa vyake, kinyume cha sheria.
Alisema uchunguzi huo umebaini kuwa mmiliki halali wa vyeti hivyo, ni mtumishi katika Hospitali ya St. Francis, iliyoko Wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro.
“Uchunguzi wetu wa awali, tulibaini kuwa hakuwa muuguzi halali. Kwani alikuwa akitumia vyeti vya mtu mwingine, ambaye tumemsajili Wilaya ya Kilombero. Na hata ukiangalia katika hili faili letu, sisi ndio tunamtambua na sio huyo muuguzi wa Ukonga,” alisema Moyo.
Alisema walijaribu kumtafuta Kondamwali, lakini hawakuweza kumpata kutokana na kwamba, tangu zahanati hiyo ilivyofungwa, walitawanyika na kwa hiyo, wakaamua kutoa taarifa katika kituo cha polisi ili washirikiane kumkamata.
Awali, serikali iliunda tume ambayo ilipendekeza kwamba, Dk. Abby Ndimbe, Dk. Kuzungu James na Dk. Ibiya wapelekwe mara moja mbele ya Baraza la Madaktari Tanganyika kujibu tuhuma na ikiwezekana wafutiwe usajili na wasimamishwe kutoa huduma kama madaktari.
Pia, ilipendekeza Kondamwali afikishwe kwenye Baraza la Wauguzi na Wakunga mara moja na ikiwezekana asimamishwe kutoa huduma kama muuguzi au mkunga na afutiwe usajili.
Tukio hilo lilitokea Februari 7, mwaka huu, katika eneo hilo, baada ya mama huyo, Sabela Mganga (31), kujifungua mapacha wawili katika zahanati hiyo na kuzuiliwa kwenda katika Hospitali ya Amana kutokana na kwamba, hakuwa amemaliza deni analodaiwa.
Baada ya kujifungua kwenye zahanati hiyo, Daktari aliyekuwa zamu, Dk. Babu Machondela, alishauri mzazi huyo ahamishiwe Hospitali ya Amana kwa ajili ya kuongezewa damu, lakini wauguzi hawakutekeleza kwa madai kuwa mgonjwa hajamaliza deni lake.
Licha ya ushauri huo wa daktari, wauguzi waliendelea kumshikilia wakidai kuwa hawezi kuondoka hadi atakapolipa deni la Sh. 125,800 anazodaiwa na zahanati hiyo kwa huduma ya kujifungua, baada ya kuwa amelipa Sh. 30,000.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment