.jpg)
Hatma ya Diwani wa Kata ya Mgama, Denis Lupala, aliyegoma kushiriki utambulisho wa viongozi wa ngazi ya wilaya na mkoa wa Iringa, mbele ya Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania bara, John Chiligati, akidai kuwa hamuelewi na hautambui ujio wake kwenye kata hiyo, sasa itajulikana kabla ya Pasaka.
Tukio hilo lilitokea juzi saa 7:10 mchana katika kata hiyo muda mfupi baada ya viongozi hao kutoka katika Chuo cha Makada wa CCM-Ihemi ambako Nape Nnauye, Katibu wa Itikati na Uenezi wa chama hicho taifa alipokabidhiwa ujenzi na usimamizi wa chuo hicho.
Diwani Lupala aliukataa utambulisho huo akidai kuwa amedhalilishwa na kudharauliwa, kwa kuwa hakupewa taarifa za ugeni huo na kwamba hata hivyo yeye hamtambui Chiligati wala haelewi ujio wake katika kata yake na kwamba anauona ni batili.
Katibu wa CCM Wilaya ya Iringa Vijijini, Mohamed Dhikiri, aliithibitishia NIPASHE kuwa tayari ameshawasiliana na wajumbe wa Sekretarieti ya chama hicho na wanatarajia kukutana kabla ya Pasaka kujadili hali iliyojitokeza katika ziara hiyo ya viongozi wapya wa kitaifa.
Chiligati na Nape walikuwa mkoani Iringa kwa ziara ya siku mbili kujitambulisha kwa wanachama wa CCM kufuatia Sekretarieti ya chama hicho kuundwa upya baada ya kuvunjwa ili kukamilisha falsafa ya Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete ya kujivua gamba.
Katika ziara hiyo ambayo siku ya pili ilitawaliwa na vibweka ikiwamo viongozi hao kudondoka chini baada ya jukwaa walilokuwa wamekaa kuanguka; Diwani Lupala, pia aliusimamisha tena msafara wa Chiligati na kumweleza bila kificho kwamba yeye ni kiongozi wa wananchi lakini anashangaa ni kwa nini hakupewa nafasi ya kuwasilisha kero zao.
Akifafanua kuhusu madai hayo, Katibu wa CCM wa Wilaya hiyo alisema si kweli kwamba Lupala hakushirikishwa katika maandalizi ya ujio wa viongozi hao, kwa kuwa alitaarifiwa na juzi asubuhi aliitwa lakini hakufika na akaonekana saa 5:00 asubuhi bila ya kuwa na taarifa yoyote.
"Sasa hivi tunaandaa kikao cha Sekretarieti pamoja na vikao vingine vya chama, tutamjadili na tutawatangazia maamuzi ya vikao yaliyofikiwa, ule haukuwa mkutano wa kueleza kero za wananchi ila viongozi wetu walipita kujitambulisha…kwa maana hiyo yapo mambo mengi tutakayoyajadili lakini mojawapo ni la utovu wa nidhamu,” alisema Dhikiri.
Hata hivyo, jukwaa hilo linalodaiwa kujengwa chini ya kiwango na muda mfupi baadaye kumomonyoka sehemu ya chini na kuanguka linadaiwa lilijengwa kwa gharama ya Sh. 500,000
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment