ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 14, 2011

U23 uso kwa uso na Nigeria

Timu ya taifa ya soka ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 23 imepangwa kucheza na Nigeria kwenye hatua ya pili ya kusaka tiketi ya kushiriki michezo ya mwakani ya Olimpiki itakayofanyika jijini London nchini Uingereza.
Ratiba ya hatua ya pili ya mashindano hayo ilipangwa jana katika Makao Makuu ya Shirikisho la soka barani Afrika, Cairo, Misri chini ya Kaimu Katibu Mkuu wa CAF, Hichan El Amrani pamoja na Mkuu wa Mashindano ya Kombe la Dunia na Olimpiki wa FIFA, Gordon Savic.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo iliyotolewa jana, Tanzania itaanzia nyumbani kati ya Juni 3,4 na 5 na mchezo wa marudiano utafanyika kati ya Juni 17,18 na 19.
Tanzania imeingia hatua ya pili baada ya kuifungisha virago Cameroon kwenye hatua ya kwanza kwa mikwaju ya penati 4-3 baada ya kutoka sare ya magoli 3-3 katika michezo miwili.
Timu nyingine zilizopangwa kucheza kwenye hatua hiyo ya pili ni pamoja na Algeria iliyopangwa kucheza na Zambia, Morocco iliyopangwa dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakati Gabon itacheza na Mali. Mechi nyingine kwa mujibu wa ratiba hiyo ya CAF Sudan itacheza na Misri, Benin itapambana na Afrika Kusini huku Tunisia ikicheza Senegal ambapo Gabon imepangwa kucheza na mshindi wa mchezo kati ya Ivory Coast na Liberia.
Mchezo wa marudiano kati ya Ivory Coast na Liberia ulisogezwa mbele na sasa umepangwa kuchezwa Aprili 20.
Akizungumza jana na gazeti hili, kocha wa vijana hao, Jamhuri Kihwelu 'Julio', alisema kuwa timu yake haiwahofii Wanigeria na kuongeza kwamba ushindani walioupata dhidi ya Cameroon umewaimarisha na sasa wataendelea kupambana ili kufuzu michuano hiyo kwa mara ya kwanza.
Julio alisema kuwa katika dunia ya sasa kwenye soka hakuna lisilowezekana kwa sababu kila timu inafanya maandalizi ya kushinda tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.
"Hakuna ubabaishaji, nia, uwezo na malengo ya kufanikiwa tunayo," alisema kocha huyo wa zamani wa Simba.
Wakati huo huo, timu hiyo ya Tanzania ya U-23, inaondoka nchini leo kwenda Kampala kwa ajili ya kuwavaa wenzao wa huko katika mchezo wa kuwania nafasi ya kushiriki michuano ya All African Games baadaye mwaka huu.
Alisema pia safari yao ya kuelekea Kampala ambayo awali ilipangwa kuwa kesho imebadilika kutokana na mechi hiyo kuelezwa kwamba itafanyika Jumamosi badala ya Jumapili.
"Tumeamua kundoka kesho (leo) badala ya Ijumaa baada ya kuelezwa kwamba mechi ni Jumamosi, kwa hiyo tumeona ni vyema tuwahi ili vijana wapate muda wa kupumzika na kufanya mazoezi ya mwisho," alisema Julio.
Alisema kuwa kikosi chake kitakuwa na wachezaji 21 na kitaondoka nchini saa 9:00 Alasiri na kitarejea nyumbani Jumapili mchana.
Alisema kuwa wanatarajia kwenda kufanya vizuri katika mechi hiyo ya kwanza ili mchezo wa marudiano utakaofanyika Aprili 30 kwenye uwanja wa Taifa hapa nyumbani kuwa mwepesi.
Baada ya kuwaondoa Cameroon, timu hiyo ilipumzika siku moja na Jumatatu iliendelea na mazoezi huku kikosi hicho kikipata faraja ya kuwa mazoezini na kipa wao, Shabani Kado.
CHANZO: NIPASHE

No comments: