.jpg)
Idadi ya watu waliokwama katika kituo cha Kanda ya Ziwa kilichoko wilayani Bunda, wanaokwenda katika kijiji cha Samunge, Loliondo, wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha kwa mchungaji Ambilikile Mwasapila, kwa ajili ya kupata tiba imepungua.
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Francis Isaack, alisema kwa sasa hali ni nafuu tofauti na siku chache zilizopita ambapo hali hiyo inatokana na kuruhusiwa kwa magari mengi yaliyochukuwa idadi kubwa ya watu.
Isaac alisema juzi alitoa vibali na kuruhusu zaidi ya magari 70, yakiwemo mabasi na magari madogo, ambayo yaliondoka juzi asubuhi, na jana asubuhi vilitolewa vibali kwa magari 116 yaliyosafirisha jumla ya watu 2,000.
Alisema utaratibu wa kutoa idadi kubwa ya magari ni kutokana na uongozi wa mkoa wa Mara kuvizuia kwa muda wa siku tatu vituo viwili mkoani humo vya Serengeti na Musoma kuruhusu magari kwenda Loliondo, ili kutoa nafasi kwa kituo cha Bunda kupunguza msongamano.
Aidha, alisema jana asubuhi kulikuwepo na uwezekano mkubwa wa kuruhusu magari mengine zaidi na kwamba ruhusa hiyo itatokana na kupokea maelekezo kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Enos Mfuru, baada ya yeye na Mfuru kupata idadi ya watu inayotakiwa kwenda Loliondo.
Kwa siku mbili tofauti mamia ya wananchi waliokuwa wamekwama kwa siku kadhaa, katika kituo hicho, waliandamana na kufunga barabara kuu ya Mwanza-Musoma wakiitaka serikali iwaruhusu waende kupata tiba.
Wakati huo huo, serikali imetakiwa kuwa makini na kuweka ulinzi madhubuti katika tiba itolewayo na Mchungaji Mwasapila ili kudhibiti matatizo yanayoweza kusababishwa na wanaojitokeza kuanzisha tiba kwa dhumuni la kupingana naye.
Hayo yalisemwa jana, jijini Dar es Salaam na Rais Mtendaji wa Shirika la Tiba Asili na Dawa Asili (Tameto), Sharifu Karama, wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema hofu inayosababisha kuhitajika kwa ulinzi na umakini kutoka serikalini ni kutoka kwa wanaopinga huduma ya Mchungaji Mwasapila na kuanzisha zao hivyo wanaweza kuchanganya aina ya miti ya sumu kwa dhumuni la kuzuiwa kwa huduma hiyo.
Alisema kutokana na ongezeko la watoa huduma ya tiba kwa imani ya kutumia miti asili inayofanana na Mwasapila kuna ulazima watu hao kujisajili ili kuwa na vibali kutoka Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jami katika kitengo cha Tiba Asili.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment