ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 14, 2011

Mshauri wa Rais abebwa na Polisi

Msaidizi wa Rais Jakaya Kikwete wa mambo ya siasa, Rajabu Luhwavi, amefikishwa mbele ya Baraza la Maadili chini ya ulinzi wa polisi kujibu tuhuma za kushindwa kufika kwenye Baraza hilo Jumatatu wiki hii. Sekretarieti ya Maadili ilimpelekea Luhwavi wito wa kufika kwenye Baraza hilo ili ajibu kwanini hakuwasilisha matamko ya mali zake, lakini hakufika na hakutoa sababu zozote za kushindwa kufika.

Jana Luhwavi alihojiwa na majaji watatu wanaounda Baraza hilo sababu za kutofika kwake na yeye alijitetea kuwa hakupata barua ya wito.
Majaji wote watatu ambao ni Mwenyekiti wa Baraza hilo, Jaji Mstaafu Damian Lubuva, Jaji Hamis Msumi na Jaji Gidious Tibakweitira, walikuwa wakimhoji maswali mbalimbali kwa saa kadhaa. Jaji Lubuva alimweleza Luhwavi kuwa Baraza hilo limeundwa kisheria hivyo lina mamlaka ya kumkamata mtu yeyote anayekaidi wito wake bila kutoa sababu zozote.
“Tarehe 11 mwezi huu tulitoa hati ukamatwe kwa kupuuza wito tuliokuletea, sheria namba 13 ya Maadili ya Viongozi wa Umma kifungu cha 24 (4) inatupa mamlaka ya kutoa taarifa kwa vyombo husika kumkamata na kumleta kwetu mtu yeyote ambaye tumemwita kwa njia za kawaida na akakaidi. Wewe tulikuita hukuja na hukutoa sababu zozote ndiyo maana tuliagiza ukamatwe na leo umefikishwa hapa mbele yetu, kwa hiyo wewe umeletwa hapa kwa nguvu tofauti na wenzako, sasa tueleze kwanini hukuja hadi ukamatwe,” alisema Jaji Lubuva.
Baada ya maelezo ya Jaji Lubuva, Luhwavi alianza kujitetea kwa kuomba radhi kwa usumbufu wowote ambao umesababishwa naye kwa kutofika mbele ya Baraza hilo.
Alisema anatambua hadhi na mamlaka ya Baraza hilo hivyo kutokufika kwake si kupuuza bali kulitokana na kukosa taarifa za wito kwa kuwa barua iliyotumwa na Sekretarieti ya Maadili haikumfikia.
“Machi 20 nilipata taarifa ya sms kutoka kwa rafiki yangu kuwa ameona jina langu kwenye Sekretarieti kuwa mimi ni miongoni mwa viongozi ambao hawajawasilisha matamko ya mali zao hivyo akanieleza kuwa naweza kuitwa, baada ya sms hiyo nikawauliza wasaidizi wangu kama wamepata barua ya mimi kuitwa mbele ya Baraza wakasema hapana, nikapiga simu Sekretarieti kuulizia kama wameniandikia barua ya wito wakasema hapana, nikawauliza kama jina langu ni miongoni mwa viongozi ambao hawajawasilisha mali wakasema kweli limo, nikawauliza nitaitwa lini wakasema Baraza litatuandikia barua wakituhitaji,” alisema Luhwavi.
“Waheshimiwa nawaomba radhi kwa yaliyotokea, mimi binafsi yamenifedhehesha sana na familia yangu kuona naandikwa hadi magazetini kuwa natafutwa, sikukatarajia hali hii itokee, ningepata barua ya wito ningekuja mwenyewe bila kusubiri nguvu itumike,” alijitetea Luhwavi.
Baada ya maelezo hayo, Jaji Lubuva alimwonyesha Luhwavi barua ya wito iliyowasilishwa ofisini kwake Machi 15, mwaka huu na kusainiwa na katibu muhtasi wake.
Luhwavi alikataa kuwa saini hiyo si yake wala katibu muhtasi wake hivyo hajui hao waliosaini na kupokea barua hiyo ni watu wa wapi.
Luhwavi: Hii sahihi sio yangu na wala siyo ya mtu yeyote wa ofisini kwangu.
Jaji: Hivi ofisini kwenu hakuna utaratibu wa kupokeleana barua kama haupo mtu anachukua kwa niaba yako?
Luhwavi: Utaratibu huo upo ila huwa zinasambazwa kwa register, ila kama ni barua binafsi ya mtu inatakiwa asaini yeye mwenyewe au katibu muhtasi wake.
Jaji: Una uhakika huyu aliyesaini hapa sio sekretari wako?
Luhwavi: Nina uhakika siyo.
Jaji: Unasema ukweli kwamba taarifa za wito wetu hapa huna kabisa kabisa?
Luhwavi: Sina mheshimiwa ningekuwa nazo lazima ningekuja hapa na hata nisingekuja ningetoa taarifa siwezi kudharau chombo hiki muhimu. Unajua barua zinakuwa na umuhimu unaotofautiana kuna zenye umuhimu wa juu kabisa, umuhimu wa kati na zile za kawaida, sasa inawezekana yule aliyepokea hakujua umuhimu wa ile barua na huenda hadi sasa amekaa nayo,” alijitetea.
Jaji: Mbona wote waliopelekewa barua wamezipata na wamefika hapa, iweje wewe tu ndo hukupata barua?
Luhwavi: Mimi ni mtumishi wa umma nimekula kiapo cha kusema ukweli mtupu, hii saini hapa si yangu wala sekretari wangu hili nina uhakika nalo kabisa, nakuhakikishia ningeipata barua ningekuja mwenyewe nisingesubiri niletwe mbele yenu kwa nguvu za dola na kwa umri wangu huu siwezi kukubali mambo hayo yanitokee.
Mwanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Getrude Cyriacus, alisema barua ya wito iliwasilishwa ofisini kwa Luhwavi Machi 18, mwaka huu na ilikabidhiwa kwa katibu muhtasi wake.
Alisema kwa kuwa Luhwavi anadai kuwa hajapata barua basi malalamiko dhidi yake yasisikilizwe ila badala yake apewe nakala ya malalamiko dhidi yake ili ayasome na aandae majibu. Baada ya maelezo hayo, Jaji Lubuva alisema ingawa Baraza hilo lilipanga kumaliza shughuli zake kesho, shauri la Luhwavi litasikilizwa Jumatatu ijayo.
Alimwonya Luhwavi kuwa ahakikishe yaliyotokea hayajirudii na kama itatokea basi ajiandae kwa adhabu kali.
“Haya yaliyotokea naomba iwe mwisho usirudie, ikijirudia tena ujue hayataishia hapahapa, nyie viongozi ndio tunatarajia muwe mfano mzuri kwa wengine sasa mkifanya hivi mnaleta taswira mbaya, haipendezi wewe kwa hadhi yako unaletwa hapa na polisi,” alisisitiza Jaji Lubuva.

SPIKA AWATAHADHARISHA WABUNGE
Spika wa Bunge, Anne Makinda, amewatadhaharisha wabunge ambao hawajajaza fomu za tamko la raslimali na madeni kuwa watafukuzwa.
Spika alitoa tahadhari hiyo jana bungeni na kusema kuwa orodha ya wabunge wasiojaza fomu hizo ni ndefu na kwamba mwisho wa kuzijaza ulikuwa ni Desemba mwaka jana.
“Miezi mitatu sasa imepita tangu muda uliopangwa kwisha…kuna orodha ndefu ya waheshimiwa wabunge ambao hawajajaza mkazijaze hatua inayofuata ni kuwafuta ubunge,” alisema na kuongeza: “Kama hujipendi endelea kukaa bila kujaza.”
Bila kusema ni lini adhabu hiyo itatekelezwa endapo hawatakuwa wamezijaza, Makinda alisema wabunge watakaojaza hivi sasa itawabidi kujielezea kwanini hawakujaza wakati huo.
Sheria ya Maadili ya Uongozi wa Umma inawataka wabunge na viongozi wa umma wanapoingia madarakani na kuondoka kutaja mali walizonazo.
WAZIRI CHIKAWE AFAFANUA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Mathias Chikawe, alisema kuanzia wiki ijayo ataanza kushughulika na wabunge wasiojaza fomu na kuwaonya kuwa wasidhani kuwa tangazo lililotolewa na Spika ni la mzaha.
CHANZO: NIPASHE

No comments: