ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, April 20, 2011

Unaishi na mawifi wakorofi? -2

MAMBO vipi marafiki? Bila shaka ni wazima wa afya njema kama nilivyo mimi. Karibuni tena katika safu yetu nzuri ambayo hukuongezea maarifa juu ya uhusiano na mapenzi. Nazungumzia juu ya mawifi wakorofi ikiwa ni sehemu ya pili baada ya kuanza wiki iliyopita.

Rafiki zangu, kabla sijaendelea napenda kuwajulisha jambo moja muhimu sana katika mapenzi. Nimeamua kuwashirikisha jambo hili, maana kuna msomaji mmoja alinipigia simu wiki iliyopita akaniambia kwamba yupo katika ugomvi mkubwa na mpenzi wake.


Katika kutafuta chanzo cha tatizo, akagundua kwamba yeye ndiye mwenye makosa, lakini anaogopa kumwomba msamaha mpenzi wake, eti anahofia kwamba atamdharau kwa kuwa yeye ni mwanaume.

Nilizungumza naye, lakini naamini wapo watu wengi wa aina hii katika jamii yetu ndiyo maana nikaona ni vyema nawe ujue ukweli juu ya jambo hili.

WEWE UKOJE?
Hebu jichunguze kwanza mwenyewe, ukoje? Ukikosewa na mpenzi wako, unakubali kosa na kuomba msamaha au unafanya kiburi? Nani amekuambia kuwa unapomwambia mpenzi wako ‘samahani’ unajishusha? Hujishushi ila unatengeneza mwanzo mzuri wenye mafanikio katika mapenzi yenu.

Ndiyo maana nimezoea kusema kuwa ndoa hulindwa na mwanandoa na ndoa hiyo hiyo huharibiwa na wanandoa wenyewe! Neno hilo lina maana kubwa sana kwa wanandoa, lazima utambue kuwa wewe ndiyo mwenye uwezo wa kutengeneza na kubomoa nyumba yako.

Kwa maana hiyo basi ili ndoa yako iweze kudumu na kuwa na maisha marefu, jukumu la kuiweka hai unalo mwenyewe, anza kuitengeneza ndoa yako sasa! 
Yes! Sasa tunaendelea pale tulipoishia. Tuliona jinsi msomaji wangu aliyewasiliana nami kwa njia ya simu anavyopata usumbufu katika ndoa yake mpaka anafikiria kuachana na mumewe.

Kikubwa nilichoelekeza wiki iliyopita ni matumizi ya busara wakati unapozungumza na mumeo juu ya suala la ndugu zake. Hata kama hujakumbwa na tatizo la mawifi wakorofi, ukisoma hapa utapata mwanga wa kukabiliana na tatizo kama hili pindi litakapokukuta. Twende tukajifunze kwa undani zaidi.

MWANZO ULIKUWAJE?
Wanasaikojia wanaamini kuwa jinsi unavyoanza kitu ndivyo unavyomaliza, hii inamaanisha kuwa kama ukivurunda kitu kuanzia mwanzo, tarajia kuharibu mpaka mwisho. Kinachotokea mwishoni ni kupunguza madhara ya tatizo ambalo tayari limeshatokea na lina madhara makubwa.

Inawezekana tangu ulipokwenda kijijini kwa mumeo (ukweni) ulishaona baadhi ya tabia zake mbaya ambazo kwa namna moja ama nyingine zilikukwaza. Kwanza mumeo atakapokupa taarifa ya ujio wa wifi yako, usioneshe kukasirika, kwa sababu kama ukionesha umekasirika, anaweza akahisi jambo fulani baya kwako.

Pengine atahisi humpendi dada yake hivyo hata siku akikukosea na kumwambia ataamini ni fitina au chuki zako binafsi. Siku wifi yako anapokuja nyumbani, kuwa wa kwanza kumkumbusha mumeo kwenda kumpokea kituoni, weka maandalizi motomoto na onyesha furaha ya ujio wake.

Mkikutana kituoni mkumbatie na uoneshe kuwa unajisikia furaha sana kumuona. Ukimfanyia hayo, hata kama alikuwa na lake moyoni, atajisikia vibaya kukufanyia kwa kuhofia mema uliyomfanyia. Hata hivyo, kama ana ukorofi wa asili haiwezi kuwa dawa, anaweza akatafuta visa vitakavyokuudhi baadaye.

MALIZENI WENYEWE
Kitu cha kwanza kabisa kufanya baada ya kuona wifi yako amekukosea ni kuzungumza naye. Inawezekana ghafla alianza kuwa na maneno ya hapa na pale au alianza kuwa na wivu usioeleweka, pengine alimwambia mumeo (kaka yake) kuwa una tabia mbaya au vyovyote katika kukuharibia ndoa yako. Usionyeshe chuki, zungumza naye taratibu.

Mweleze jinsi unavyompenda na kuuthamini uhusiano wenu. Ikiwa utatumia lugha nzuri naamini atakuelewa lakini kama siyo muelewa ataendelea na chokochoko zitakazokukera. Unajua kitu cha kufanya? Soma hapo chini.

MSHIRIKISHE MUMEO
Kama yote hapo juu hayakufua dafu, unapaswa kukaa chini na mumeo na kumweleza juu ya jambo hili. Kukaa kwako kimya na kumvumilia kutakuwa hakuna maana, kwa sababu ni rahisi ndoa yako kuvunjika.

Usimfiche chochote, hata kama aliwahi kukutolea maneno machafu kwa mumeo, usijali, zungumza taratibu bila jazba huku ukitumia hoja kuliko maneno matupu! Nyumba ni kwa ajili yako na mumeo. Kuolewa hakumaanishi kwamba umeolewa na ukoo mzima na kila mmoja anaweza kukudhihaki na kukutana!

Lazima utambue haki yako na kama mumeo ana mapenzi ya dhati kwako,lazima atakupa kipaumbele na kufanya maamuzi sahihi kwa heshima na sababu ya kuilinda ndoa yenu ambayo ni muhimu sana.

Ngoja nikuambie kitu kimoja dada yangu, wanaume si watu wa kukurupuka, mara zote kama utazungumza naye kistaarabu ukitumia hoja ni wazi kuwa atakuelewa na kutafuta njia mbadala za kutatua tatizo.

Kumbuka ukitumia kauli chafu au kukaripia, utamfanya ahisi kuwa una chuki na ndugu yake na unataka kuwagombanisha. Usiruhusu fikra hizo akilini mwake. Kama ulianza vizuri, atashawishika kukuamini maana atajaribu kufikiria jinsi ulivyokuwa ukimkirimu ndugu yake tangu awali kisha atalinganisha na madai yako.

Kumbuka kwamba mumeo atakuwa anamfahamu vizuri zaidi dada yake, kama ana matatizo hayo atakuwa anayafahamu kabla, hivyo utatuzi wake kuwa mzuri usio na migogoro!   

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi ambaye anaandikia magazeti ya Global Publishers, kwa sasa ameandika vitabu vya True Love, Secret Love na Lets’s Talk About Love vilivyopo mitaani. Unaweza kumtembelea kwenye mtandao wake; www.shaluwanew.blogspot.com au jiunge naye kwenye facebook.

No comments: