ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 21, 2011

Wanne kortini kwa kula njama, kutaka kumuua Dk. Chegeni

Mbunge wa Busega wilayani Magu, Dk. Raphael Chegeni.
Watu wanne, jana walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza, wakituhumiwa kula njama na kutaka kumuua aliyekuwa Mbunge wa Busega wilayani Magu, Dk. Raphael Chegeni.

Wakili wa Serikali, Pascal Malungu alidai kuwa katika tarehe tofauti Februari na Machi, watuhumiwa hao; Dismas Zacharia (47), Erasto Kombe (48), Queen Joseph Bogohe (37) na Hellen Joseph Bogohe (37), kwa nyakati tofauti walikula njama ya kutenda kosa la mauaji.


Pia alidai watuhumiwa hao kwa tarehe tofauti kati ya miezi hiyo, mkoani hapa na sehemu nyingine nchini Tanzania, walikula njama ya kutaka kumuua Dk. Chegeni.

Hakimu Mkazi Mfawidhi, Angelius Lumisha, alisema washtakiwa hawatakiwi kujibu lolote kwani muda umemalizika na bado hawajui kama shitaka hilo litasikilizwa na Mahakama Kuu au la.

Alisema kesi hiyo itapelekwa tena mahakamani hapo kesho asubuhi na washitakiwa wote watakwenda rumande suala lao la dhamana litakapojadiliwa.

Awali, wakili wa washitakiwa Kabona aliomba wateja wake wapewe dhamana kwani hata polisi, ambao ndio wanaendesha upelelezi wa suala hilo, wamewaamini na kuwapa dhamana.

Hata hivyo, Wakili wa Serikali, alipinga ombi hilo kwa kusema washitakiwa wakiwa nje, wataweza kuvuruga upelelezi wa kesi hiyo kwa kutumia simu zao za mikononi.

Kabona alidai tayari simu zote za washtakiwa tangu wakamatwe zimezuiliwa na polisi kwa hiyo hawawezi kuvuruga upelelezi wowote.

Taarifa za kipolisi zilidai kuwa watu hao walikamatwa Machi 13 na kuhojiwa na polisi kwa siku kadhaa kabla ya jana kupelekwa mahakamani
CHANZO: NIPASHE

No comments: