Raia waua askari Polisi, wamjeruhi mwingine vibaya
Wananchi wavamia familia, waua baba, mama, mtoto
Basi lapata ajali laua watatu, lajeruhi abiria 20
Wananchi wavamia familia, waua baba, mama, mtoto
Basi lapata ajali laua watatu, lajeruhi abiria 20.jpg)
Wananchi wa Kata ya Mwakashanhara Tarafa ya Puge wilayani Nzega, Mkoa wa Tabora wamemuua askari polisi namba E 9530 PC Joseph na kumjeruhi askari mwingine namba G 246 PC Juma Hussein baada ya kuwashambulia kwa mapanga.
Askari hao walikuwa wakifanyakazi katika Kituo cha Puge kilichopo katika tarafa hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Liberatus Barlow, alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa nne asubuhi katika kata hiyo. Alisema askari aliyejeruhiwa hali yake ni mbaya.
Hata hivyo, Kamanda Barlaw alisema kwa jana hakuwa na taarifa zaidi kuhusiana na tukio na kuahidi kuzungumza baada ya kupata taarifa kamili.
Kamanda huyo alisema kuwa Jeshi la Polisi mkoani Tabora linaendelea na uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo.
Haya hivyo, habari kutoka katika Kata ya Mwakashanhara zinaeleza kuwa chanzo cha mauaji hayo ni askari wa kituo hicho kwenda kufanya operesheni ya kukamata bangi ambayo inalimwa na baadhi ya wakazi wa eneo hilo.
Habari kutoka kata hiyo zilieleza kuwa oparesheni hiyo ilikuwa na askari watano ambao watatu walifanikiwa kujinusuru na kukimbia na wawili kudhibitiwa na wananchi hao.
Inadaiwa kuwa askari hao walizidiwa nguvu na kusababisha kifo cha mmoja wao na kumjeruhiwa vibaya mwingine ambaye amelazwa katika Hospitali ya misheni ya Ndala.
Inadaiwa kuwa sababu nyingine iliyosababisha tukio hilo ni mahusiano mabaya kati ya polisi na wakazi wa kata hiyo kutokana na polisi kukamata mara kwa mara pikipiki zao na matukio mengine ya kuwanyanyasa.
Mganga Mfawidhi wa Hospital ya Ndala, Dk. Reuben, alisema PC Juma Hussein alijeruhiwa vibaya kichwani kwa mapanga na mkono wa kushoto umevunjika mara mbili.
WATATU WAUAWA KIKATILI SUMBAWANGA
Katika tukio lingine, watu watatu wa familia moja ambao ni wakazi wa kijiji cha Miombo, Kata ya Namanyere, wilayani Nkasi mkoa wa Rukwa wameuawa na miili yao kuchomwa moto baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana.
Inadaiwa kuwa marehemu wanahusishwa na kifo cha mtoto wa miaka minne, mkazi wa kijiji hicho.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Isunto Mantage, alisema tukio hilo lilitokea juzi usiku wa manane, baada ya kundi la wananchi kuvamia nyumba ya Luciano Chole (62) na kuwashambuliwa wanafamilia yake kwa kutumia silaha mbalimbali na kuwasababishia mauti hayo.
Kamanda Mantage aliwataja wanafamilia waliouawa kuwa ni Luciano Chole (62) na mkewe, Adelina Mulele (54) na mtoto wao, Jailos Silvanus (29).
Kamanda Mantage alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa siku tatu kabla ya tukio hilo, mtoto mwenye umri wa miaka minne, Geminus Kwimba, alitoweka nyumbani kwao katika mazingira ya kutatanisha na siku iliyofuata mwili wake ulikutwa umetupwa kwenye dimbi la maji baada ya kuuawa an watu wasiojulikana.
Alisema baada ya tukio hilo, wakazi wa kijiji hicho walihisi kuwa mtoto huyo aliuawa na Jailos Silvanus na kupanga kumuua kama njia ya kulipiza kisasi.
Mantage alisema usiku wa kuamkia juzi kundi la wananchi lilizingira nyumba ya wanafamilia hao na kumshambulia Jailos hali iliyowalazimisha wazazi wake kuingilia kati kwa lengo la kumuokoa.
Alisema hali hiyo iliwafanya wananchi hao kuwashambulia wote hadi wakafariki dunia kisha miili yao kuchomwa moto.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, baada ya kufanya unyama huo, watu hao walikimbia na kuongeza kuwa Jeshi la Polisi linawasaka.
AJALI YA BASI LA NEW FORCE YAUA WATATU, 20 WAJERUHIWA
Wakati huo huo, watu watatu wamekufa papo hapo na wengine zaidi ya 20 kujeruhiwa vibaya baada ya basi la Kampuni ya New Force kugongana uso kwa uso na gari dogo la mizigo katika eneo la Wang’ing’ombe barabara ya Iringa-Mbeya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Evarist Mangalla, akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu, alisema kuwa ajali hiyo ilitokea jana saa 2:30 asubuhi na kuyahusisha magari mawili na wapanda baiskeli.
Aliyataja magari hayo kuwa ni basi la Kampuni ya New Force lenye namba za usajili T 666 BCR lililokuwa likitokea mkoani Mbeya kwenda jijini Dar es Salaam na gari dogo la mizigo aina ya Toyota Pick Up namba T 273 ACP.
Akizungumzia mazingira ya ajali hiyo, Kamanda Mangalla alisema dereva wa basi la New Force aliyekuwa katika mwendo kasi alimgonga mwendesha baiskeli na mwenzake waliyekuwa wamepakizana ndipo alipojikuta akihama barabarani na kuhamia upande mwingine na kuigonga Pick up hiyo na kusababisha vifo hivyo.
“Kama ulivyopata taarifa toka kwa mashuhuda wa ajali hiyo huko Wang’ing’ombe ni kwamba basi la New Force limesababisha ajali iliyoua watu watatu baada ya kugongana na gari dogo aina ya Toyota Pick up,” alisema Kamanda Mangalla na kuongeza:
“Dereva wa basi alikuwa kwenye mwendo kasi akashindwa kulimudu gari na akagonga baiskeli iliyokuwa imebeba watu wawili halafu akahama saiti yake akaenda kugongana na hiyo Pick up.”
Hata hivyo, Mangalla hakuwataja waliokufa katika ajali hiyo wala majeruhi, ingawa alisema kuwa walipelekwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Njombe ya Ilembula.
Imeandikwa na Lucas Macha, Tabora; Godfrey Mushi, Iringa na Mwandishi Wetu Sumbawanga.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment