Watu watatu wamejeruhiwa vibaya na mtu mmoja anayedaiwa kupatwa na ugonjwa wa kichaa, akiwa njiani kutoka Loliondo kwa Babu Ambilikile Mwaisapila kupata kikombe.
Mtu huyo ambaye ilielezwa kuwa ana ugonjwa wa akili alikuwa akirejea nyumbani kwake mkoa wa Tanga.
Mtu huyo aliyetajwa kwa jina la Juma Singano mkazi wa mkoa wa Tanga, alifanya tukio hilo katika kituo kikuu cha mabasi yanayoenda mkoani Tanga, akiwa tayari ameshapakiwa kwenye Basi la Ngorika linalotoka Arusha kwenda Tanga
.Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na watu walioshuhudia tukio hilo, Singano alianza kuwajeruhi wenzake baada ya kukata kamba alizokuwa amefungwa na ndugu zake baada ya kuanza kuugua ugonjwa huo unaodaiwa kuwa huenda ukawa ni kichaa .
Mashuhuda hao walisema, Singano aliyepanda basi hilo muda mfupi baada ya kushuka kwenye basi la abiria alilotoka nalo Samunge kwa Babu, alikuwa amekaa katika siti ya basi hilo na muda mfupi kabla ya basi kuondoka, ghafla alikata kamba na kuchomoa kisu ambacho hakuna mtu anayejua kilipotoka na kuanza kuwashambulia watu waliokuwa karibu nae.
Mmoja wa majeruhi hao, ambaye aliumizwa vibaya na kisu katika maeneo mbali mbali ya mwili wake, Benjamini Thomas, mkazi wa Korogwe, alisema kuwa alishtukia akichomwa kisu cha mgongoni na wakati ameduwaa akachomwa kisu kingine kichwani .
“Mimi nilikuwa nimekaa karibu naye akiwa amefungwa kamba na muda wote alikuwa ametulia ghafla nikashtuka kusikia nachomwa kisu mgongoni , sijakaa sawa nikachomwa kingine kichwani na ndipo nikaanza kukimbia nikipiga kelele “alisema kijana huyo ambaye amelazwa katika hosipitali ya Mkoa wa Arusha Mount Meru .
Wengine waliojeruhiwa ambao ni wafanyakazi wa basi la Ngorika wakiwa katika harakati za kuwasaidia abira wao ni pamoja na Juma Joseph maarufu kwa jina la rasta na Tiela Mollel ambaye hali yake ni mbaya na amehamishiwa katika hosipitali ya Seliani .
Kwa mujibu wa watu waliokuwa wamesafiri na Singano, wakati anaaza safari ya kwenda kwa Babu alikuwa hana tatizo lolote na alifika Samunge akanywa dawa vizuri lakini wakati anarudi njiani ndio akapatwa na ugonjwa huo .
Jeshi la polisi limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na Singano amelazwa katika Hosipitali ya mkoa wa Arusha ya Mount Meru akiwa chini ya ulinzi mkali akiwa amefungwa kamba miguu na mikono ili asije akashambulia tena wagonjwa.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment