ANGALIA LIVE NEWS

Monday, May 16, 2011

CAF yairudisha Simba Afrika, kuivaa Casablanca

Shirikisho la soka la Afrika, CAF, limeirudisha Simba kwenye Ligi ya Klabu Bingwa Afrika baada ya kukubali rufaa ya mabingwa wa zamani hao wa Bara dhidi ya TP Mazembe kufuatia mchezo baina ya timu hizo mbili Machi mwaka huu.
Taarifa ya CAF iliyotolewa jana Jumamosi imesema TP Mazembe imeondolewa kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Klabu Bingwa kwa kosa la kumchezesha mchezaji haramu.

Taarifa hiyo ilisema nafasi ya Mazembe itachukuliwa na timu itakayoshinda mchezo wa mtoano, utakaofanyika katika uwanja usio na mwenyeji, kati ya Simba na Wydad Casablanca.
"Kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa na Simba Sports ya Tanzania baada ya mechi namba 68 ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika, Shirikisho la Soka la Afrika lilifanya uchunguzi wa madai ya TP Mazembe kumchezesha mchezaji haramu aitwaye Janvier Besala Bokungu," taarifa hiyo ilisema.
Matokeo ya uchunguzi huo yaliwasilishwa kwa kamati ya uendeshaji ya mashindano ya klabu ya CAF.
"Kutokana na majibu ya uchunguzi huo, kamati ya mashindano imeamua kuitupa nje TP Mazembe" kutokana na kuvunja kanuni za mashindano, taarifa hiyo ilisema.
Mazembe iliitoa Simba kwa jumla ya mabao 6-3 kabla ya kuingia hatua ya makundi kwa kuifunga Casablanca jumla ya magoli 2-1.
Kama Simba itaitoa Casablanca itaingia hatua ya makundi kwa mara ya pili baada ya 2003, na kuungana na timu za Moloudia Club d’Alger, Esperance, Raja Casablanca, Al Ahly, Enyimba, Al Hilal na Coton Sport de Garoua.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI


No comments: