Mambo bado ni mazito ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, baada ya Kamati ya Siasa kumpa karipio Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan, kutokana na kuwahusisha viongozi na vitendo vya ufisadi.
Katika karipio hilo, Azzan ametakiwa na Kamati ya Siasa kuacha tabia ya kutumia vyombo vya habari kutoa tuhuma.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Katibu wa Siasa na Uenezi Mkoa wa Dar es Salaam, Juma Simba Gaddafi, alisema kamati ya siasa ilikutana juzi na kujadili masuala mbalimbali, zikiwemo tuhuma ambazo zilitolewa na Azzan.
Gaddafi alisema adhabu iliyotolewa imezingatia kanuni za uongozi na maadili ibara ya nane kifungu cha tatu pamoja na adhabu hiyo, kamati ya siasa imetoa barua kwa Azzan.
Alisema kamati imetoa barua kwa mbunge huyo kwa mujibu wa hoja alizozitoa na kumtaka afuate taratibu za kuwasilisha tuhuma kwenye chama na sio kutumia vyombo vya habari.
Hata hivyo, alisema kutolewa kwa adhabu hiyo kwa Azzan hakumfungi kuendelea kutoa tuhuma hizo isipokuwa kutumia vikao.
Aidha, Gaddafi alisema adhabu kwa mbunge huyo haina lengo la kumsafisha kiongozi yeyote.
Alisema kuwa katika kikao hicho Kamati ya Usalama na Maadili ilitaka mbunge huyo achukuliwe hatua baada ya kutuhumu mamlaka za vikao vya chama katika vyombo vya habari.
Gaddafi alisema Azzan alitakiwa kufuata taratibu zilizopo katika chama kwa kuwasilisha tuhuma ili zijadiliwe na hatimaye kupatiwa ufumbuzi katika vikao.
Alisema kamati imeridhika kuwa mbunge huyo alitenda kosa kwa kuzungumza na waandishi wa habari na kutuhumu vikao vya sekretarieti na kamati ya siasa.
"Baada ya kamati za siasa kujadili kwa kina tuhuma hizo na kumpa nafasi Azzan ya kumtaka ajitetee kwa mujibu wa katiba ya CCM ibara ya 14 (4), kamati iliridhika kuwa mbunge huyo alifanya kosa la makusudi, tena kwa chuki binafsi na kuamua kuchafua mamlaka nzima ya chama,” alisema Gaddafi.
Aidha, alisema Aprili 20, mwaka huu, walimuandikia Azzan barua ya kumtaka kufuata taratibu na kumsihi aache kutumia vyombo vya habari, lakini alikaidi.
Alisema jambo hilo liliilazimu kamati ya maadili kukutana na kumhoji kuhusu kutumia vyombo vya habari kuzituhumu mamlaka za vikao vya mkoa badala ya kuwasilisha tuhuma zake ili zijadiliwe kwenye kikao.
“Katika mjadala na tafakari, Kamati ya Siasa iliona kwamba Mheshimiwa Azzan ametumia madaraka yake vibaya kutoa taarifa kwenye vyombo vya habari na kufanya hivyo amevunja miiko ya uongozi kama ilivyoelekeza katiba ya CCM ibara ya 18 (1) na ahadi ya mwanachama kama ilivyoelekezwa kwenye katiba ya CCM,” alisema Gaddafi. Alisema kamati hiyo imeona kuwa kutoa shutuma nzito kama vile ufisadi, rushwa na kushindwa kutekeleza wajibu kwenye vyombo vya habari dhidi ya mamlaka za vikao ni kukipaka matope chama.
Hivi karibuni, Azzan alitoa siku 10 kwa sekretarieti hiyo kuandaa kikao kwa ajili ya kujadili tathmini ya mwenendo mzima wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana vinginevyo atawalipua kwa kuanika madudu yanayofanywa na watendaji hao.
Azzan alisema sekretarieti hiyo haijafanya kikao chochote na hakuna matarajio ya kuitisha kikao wakati katiba inawataka wafanye hivyo.
Azzan pia, aliishutumu sekretarieti na kuitaka ijiuzulu na kuahidi kuanika uozo unaofanywa na wajumbe wake ndani ya siku 10.
Alisema viongozi wa mkoa wamekuwa na utendaji mbovu hali ambayo ilisababisha kuwepo kwa makundi ndani ya CCM tangu mwaka 2007 ulipofanyika uchaguzi wa ndani wa chama.
“Kuna makundi mawili yamegawanyika ndani ya chama hali ambayo ilisababisha kuchukuliwa kwa majimbo yetu kwani walikuwa wanafanya ufisadi mkubwa wa kuwaweka watu wao wagombee wakati halikuwa chaguo la wananchi,” alisema.
Aliitaka sekretarieti ya mkoa kujivua gamba kwa madai kuwa wajumbe wake wamekuwa wakifanya ufisadi mkubwa wa kukiangamiza chama.
Jana, Azzan akizungumza na televisheni ya TBC1 alieleza kushangazwa na hatua zilizochukuliwa na kamati hiyo kwa kusema watuhumiwa wanaamua kesi inayowahusu.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment