ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, May 14, 2011

CCM Rorya wazidi kuparaganyika

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilson Mukama
Wakati Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilson Mukama, akitarajiwa kuanza ziara ya siku tano mkoani Mara, hali si shwali ndani ya chama hicho wilaya ya Rorya, baada ya baadhi ya viongozi kumtaka Mwenyekiti wa chama hicho wilayani humo kujiuzulu.
Walimwomba achukue uamuzi huo kabla ya ujio wa Katibu Mkuu wa CCM kuwasili katika wilaya hiyo kwa ziara ya kukiimarisha chama.

Akizungumza na NIPASHE jana, Katibu wa Siasa, Itikadi na Uenezi  wa wilaya ya Rorya, Samweli Gerald, maarufu kwa jina la Namba 3, alitaja sababu za kumtaka mwenyekiti wake kujiuzulu kuwa ni kutokana na kushindwa kuwanadi wagombea  wa CCM wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 huku akimtuhumu kutumia nafasi hiyo kuwapigia kampeni wagombea wa Chadema.
Alisema sababu nyingine ni kushindwa kuhudhuria vikao sita vya kamati ya siasa ya wilaya na vitatu vya halmashauri kuu ya CCM wilaya vilivyofanyika wakati wa kampeni na baada ya kumalizika kwa uchaguzi.
Alidai kuwa kiongozi huyo alifikia hatua baada ya kuchukizwa kwa kutochaguliwa kwa watu anaodaiwa  kuwataka katika kura za maoni ndani ya chama hicho.
“Sisi tunamshauri mwenyekiti ajivue gamba mwenyewe badala ya kungoja aje avuliwe kwa nguvu mbele ya Katibu Mkuu..Hatuko tayari kuwa na kiongozi kama huyo, kata saba zilikwenda upinzani, kampeni hizo alizifanya yeye kwa kukipinga chama chake huku akiwapinga mgombea ubunge na urais wa CCM.
 Alisema tathmini iliyofanywa ndani ya chama kuanzia ngazi ya matawi ilionyesha wazi jinsi mwenyekiti huyo alivyochangia kupotea kwa kata zaidi ya hizo saba kati ya 21 kwa kushindwa kufanya kampeni za kuwanadi wagombea wake.
Hata  hivyo, Mwenyekiti huyo, Yuda Ambonyo, alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusu tuhuma hizo,alijibu kuwa hayo ni mambo ya chama na si ya waandishi wa habari hivyo hawezi kueleza chochote kisha kukata simu.
CHANZO: NIPASHE

No comments: