
Kocha wa timu ya Bafana Bafana, Pitso Mosimane (kushoto) akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mechi yao ya leo dhidi ya Taifa Stars.(Picha: Omar Fungo)
Timu ya taifa ya soka, Taifa Stars, leo inaikaribisha Afrika Kusini 'Bafana Bafana' katika mechi yao ya kimataifa ya kirafiki itakayochezwa kuanzia saa 12:00 jioni kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Katika mechi hiyo, timu zote mbili zitashuka dimbani bila ya nyota wake wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi na hiyo imetokana na ukweli kuwa mechi hiyo inafanyika katika siku isiyotambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Akizungumzia mechi ya leo, kocha wa Stars, Mdenmark Jan Poulsen, alisema kuwa mechi hiyo itakuwa ngumu kwa sababu wachezaji wa timu zote watataka kuonyesha viwango vya juu ili wasake nafasi katika vikosi vya kwanza baada ya nyota wanaocheza nje ya nchi zao kutokuwepo.
Poulsen alisema kuwa wachezaji wake ambao wamemaliza ligi tangu Aprili 10, wamefanya mazoezi ya kujijengea stamina kwa muda mrefu ili kukabiliana na ushindani wa Bafana na anaamini kwamba wataonyesha kiwango bora na hatimaye kupata matokeo mazuri.
Alisema kuwa mechi hiyo ni muhimu kwao kwa ajili ya kukiimarisha kikosi chake kinachojiandaa na mechi ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.
"Afrika Kusini ni moja ya timu kubwa barani Afrika, mechi itakuwa ngumu lakini tutapambana nao na kuwaonyesha kwamba nasi tunaweza," alisema Poulsen.
Aliongeza kwamba licha ya kuwakosa nyota wake wanaocheza nje ya nchi na Mrisho Ngassa na Stephano Mwasika walio majeruhi, wachezaji wake wengine wana nafasi kubwa ya kufanya vizuri.
Kocha wa Bafana, Pitso Mosimane, alisema kuwa kikosi chake kitashuka dimbani bila ya nyota wake 14 wanaocheza soka la kulipwa Ulaya huku pia ikiwakosa wachezaji wengine nane ambao wanazichezea klabu za Ajax Cape Town, Orlando Pirates na Kaizer Chiefs zilizokataa kuwaruhusu kutokana na kukabiliwa na mechi muhimu za ligi kuu ya kwao, Kombe la Shirikisho na Ligi ya Klabu Bingwa Afrika.
"Ukicheza siku ambayo haitambuliwi na FIFA ni tatizo, ila wachezaji nilionao watatumia nafasi hii kunionyesha kwamba wanaweza na hata katika wale wanaocheza nje, ni sita tu ndio wana nafasi kwenye kikosi chetu cha kwanza," alisema Mosimane.
Aliwataja wachezaji wake ambao wako kwenye kikosi cha kwanza na leo watashuka dimbani kuwa ni pamoja na Itumeleng Khune (kipa), Reneilwe Letsholonyane na mfungaji wa bao la kwanza kwenye fainali zilizopita za Kombe la Dunia, nahodha Siphiwe Tshabalala ambaye ndiye aliyechaguliwa kuwa nahodha wa timu hiyo.
Mosimane alisema kuwa wakali anaowakubali zaidi ndani ya kikosi cha Stars ni winga Mrisho Ngassa, beki Shadrack Nsajigwa na kipa Juma Kaseja aliowahi kuwaona katika mechi tofauti zilizowahi kuonyeshwa na televisheni ya Super Sport.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment