Tuesday, May 3, 2011

Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kuwa ajenda ya kuwataka viongozi wanaokichafua kuwajibika ilijadiliwa katika vikao vyake vya Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na kwamba ilikuwa ni moja ya mazimio 26 ya NEC.
Ufafanuzi huo ulitolewa jana na Katibu Mkuu wa CCM, Willison Mukama, jijini Dar es Salaam alipokutana na wahariri wa vyombo vya habari kwa ajili ya kufahamiana nao.

Mukama ambaye aliongozana na wajumbe wa Sekretarieti ya chama hicho, ambao ni Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, Katibu wa Siasa na Mambo ya Nje, January Makamba na Katibu wa Uchumi na Fedha, Mwigulu Mchemba, alisema wanaodai kuwa ajenda hiyo haikujadiliwa wala kutolewa kwa azimio hilo wanapotosha ukweli. Tangu kumalizika kwa vikao hivyo, baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakikaririwa wakisema kuwa NEC haikutoa azimio hilo.
Alisema azimio hilo linasema kuwa chama kiendelee na mapambano dhidi ya ufisadi na kwamba viongozi wanaotuhumiwa watafakari, wapime na kuchukua hatua wenyewe kwa mustakabali wa chama.
Mukama alisema kuwa mbali na azimio hilo la NEC, hotuba ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, ya kufunga mkutano wa NEC ilizungumzia suala hilo kwa msisitizo mkubwa.
Mukama, alisema katika hotuba hiyo, Rais Kikwete, alisema chama kimekubaliana kutokuwa na ajizi katika mapambano dhidi ya rushwa na kuwataka viongozi wanaotuhumiwa kutafakari, kupima na kuchukua hatua wenyewe.
Akitoa mfano jinsi Rais Kikwete alivyo na nia ya dhati ya kuendeleza mapambano dhidi ya ufisadi, Mukama, alisema ameagiza kuibadili Kamati ya Maadili ya chama hicho kuwa Tume na kuiongezea wajumbe kutoka 12 hadi 14. Hata hivyo, alipotakiwa kueleza lini watuhumiwa wa ufisadi watakabidhiwa barua za kuwataka kujiwajibisha kabla chama hakijawachukulia hatua, Katibu Mkuu huyo wa CCM, hakutaka kujibu badala yake alisema kuna upotoshaji.
Alisema watu wanaosema kuwa watuhumiwa wamepewa siku 90 wakati vikao cha NEC hufanyika mara tatu kwa mwaka, hivyo NEC itakutana tena baada ya siku 120. Mukama alisema kuwa njia mbalimbali zinaweza kutumika kuwaondoa katika chama viongozi wanaokwenda kinyume cha maadili, mojawapo ikiwa ni uchaguzi wa chama hicho unaotarajiwa kufanyika mwakani.
Kuhusu madai kuwa hakuna majina yoyote ya viongozi wa CCM ambayo yaliyotajwa kwamba wanakabiliwa na tuhuma za ufisadi wakati wa vikao vya CCM na vilivyofanyika mjini Dodoma kuanzia Aprili 8 hadi 11, mwaka huu, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema katika vikao hivyo wajumbe walitajana kwa majina.
“Kwenye vikao tulitajana kwa majina ukiwa ni utaratibu wa kujiwajibisha,” alisema Nape na kuongeza kuwa kama mtu amejiwajibisha serikalini hana budi pia kujiwajibisha katika chama.
Mukama alipotakiwa kufafanua sababu za kutowachukulia hatua viongozi wa chama na serikali waliotajwa katika orodha ya mafisadi mwaka 2007 na Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, alisema
Dk. Slaa anaweza kutoa orodha yake, lakini CCM kinajiendesha kwa misingi yake. “Slaa alimtaja Sumaye, lakini kesho yake akasema amekosea”.
Kwa mujibu wa Mukama, mageuzi yaliyoanzishwa na CCM yametokana na utashi baada ya kuona haja ya kufanya hivyo kutokana na mazingira ya sasa duniani.
CHANZO: NIPASHE

No comments: