Ni Alhamisi nyingine wasomaji wangu, safu hii ya Mashamsham bado inakudondoshea zile dalili tano za kumtambua mwanaume anayetembea na hausigeli.
Naamini wengi mnakumbuka tulipoishia wiki iliyopita, lakini kwa wale ambao hawakumbuki niwadokeze kidogo; tuliishia hivi…
Kwa hiyo, kina baba wengi sasa hukwepa sebule na kwenda chumbani kwa msichana, stoo, bafuni, jikoni kama liko pembeni na uani, hasa maeneo yenye vificho kama nyuma ya karo au kama kuna sehemu kumesimamishwa vitu chakavu.
Chooni si sana kwa sababu ni eneo linalofikwa na watu kila wakati karibu usiku kucha.
Sasa hatari ipo hivi; mke asiyejua haya, kama mumewe ataendelea kutoka kimapenzi na hausigeli, itafikia wakati watahama nyumba. Namaanisha kwamba, hufika mahali wakitaka kukutana kimwili, wanakwenda gesti.
Gesti zao mara nyingi, ni nyuma ya nyumba au mtaa wa pili. Huwa hawaendi mbali sana kwa kuogopa muda wa msichana kufanya kazi za ndani.
Leo tunaendelea na dalili ya tatu kama nilivyoahidi.
DALILI YA TATU
Wanaume wengi ambao wapo kwenye uhusiano wa kimapenzi na wasichana wa kazi, hupenda kuwa wa mwisho kutoka nyumbani.
Mfano, wewe mke na mumeo wote mnafanya kazi, kila asubuhi mnatoka kwenda kupanda basi au gari lenu, zamani mumeo alikuwa akitangulia na kukusubiri nje, lakini ghafla akaanza tabia ya kuwa wa mwisho.
Hapa namaanisha kuwa, wewe ukishatoka baada ya dakika mbili na yeye ndiyo anatoka, hufanya hivyo ili kupata nafasi ya kuwasiliana na mpenzi wake huyo, pengine hata kumpiga busu la kwaheri.
Unaweza kumwona mumeo amejiandaa kila kitu, lakini anajizungusha-zungusha mpaka wewe unatoka, hata ukimwambia twende, mara atarudi chumbani, mara ataingia bafuni mpaka wewe utoke.
Kwa upande wa hausigeli, kama anajua kuwa lazima aagane na baba asubuhi, walio wengi kama wanaoshea vyombo nje huwa hawaendelei na shughuli hiyo bali hufanya usafi sebuleni ili kumpa nafasi baba aweze kuagana naye.
Sasa, kama ikitokea siku mumeo ana tabia hiyo, fuatilia kwa karibu sana utajua nini kipo kati ya wawili hao.
DALILI YA NNE
Dalili hii ya nne ni kubwa sana na iko wazi kwa mke mwenye ufahamu wake. Mume kama ana uhusiano wa kimapenzi na msichana wa kazi, ikitokea mke amesafiri ni nafasi kubwa sana kwao kujiachia.
Ni katika kipindi hicho, hausigeli ataweza kuingizwa hadi chumbani na kulala. Tena wengine hujiachia vibaya, kwani hata akiamka asubuhi anaweza kuacha khanga yake ikiwa imeandikwa; Paka Akitoka Panya Hutawala.
Sasa mke utaijuaje tabia hii? Ni rahisi sana, ukiwa safarini utashangaa ukimpigia simu mumeo saa kumi na mbili jioni na kumuuliza aliko atakujibu nyumbani wakati kawaida yake hurudi saa nne mpaka tano usiku.
Asubuhi, kama kawaida yake kwenda kazini ni saa moja utashangaa kumsikia mpaka saa mbili kasoro hajaondoka na sababu anazokupa hazina maana.
Wakati mwingine pia, ukimpigia simu usiku atachelewa kupokea au akipokea maongezi yake yanaashiria kutaka mmalize haraka. Ni kwa sababu yupo na msichana wa kazi pembeni.
Mapenzi ya aina hii yakifikia hapa, mke ndani ya nyumba anakuwa anaishi katika hatari kubwa ya talaka au ugomvi wa mara kwa mara. Na kama msichana huyo wa kazi amejaaliwa uzuri, hakika ndoa hupinduka na yeye kuchukua nafasi.
Wapo wanawake kibao mitaani ambao ndoa zao zilipinduliwa na wasichana wa kazi. Hufika mahali akitaka kwenda kuwaona watoto anakuwa mwizi, anafikia nyumba ya jirani na kuwaita.
Nakupa mfano mmoja; huu ulitokea wilayani Korogwe, Tanga. Dada mmoja (jina ninalo) aliolewa na kubahatika kuzaa watoto wawili wa kiume.
Lakini alichokosea ndani ya nyumba yake, alimwachia msichana wa kazi kuendesha kila kitu. Mume akirudi anakumbana na huduma kutoka kwa dada, asubuhi akitaka kwenda kazini anakumbana na huduma za hausigeli, mwishowe wakajenga uhusiano wa kimapenzi.
Imekwenda, mke hajui, ikafika mahali mume akamrudisha mke kwao kwa kisa kidogo tu, alimjibu jeuri. Akiwa nyumbani kwao, mke akapata habari kwamba, mumewe amefunga ndoa na msichana wa kazi tena akiwa mjamzito.
Ikawa mke huyo akienda kuwaona watoto wake anakaribishwa na msichana wake wa kazi, anamuandalia chumba cha kulala ambacho awali alikuwa akilala yeye. Mama akawa hana chake.
Haya yote ni madhara ya kuwaachia wasichana wa kazi wafanye kila kitu kwa waume ndani ya nyumba. Ni hatari kuliko inavyofikiriwa.
Wiki ijayo tutaangalia dalili ya tano na ya mwisho. Asanteni sana.

No comments:
Post a Comment