.jpg)
Mwandishi wa habari mwandamizi, Timothy Kahoho, amewasilisha ombi chini ya hati ya dharura la kuomba Wakurugenzi wa kampuni za kufua umeme za Dowans Holdings SA na Dowans Tanzania Limited, wakamatwe na kupelekwa gerezani kwa kudharau amri ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Gazeti moja la kila siku la Mei 21, mwaka huu, lilichapisha habari kwamba mitambo ya Dowans imeuzwa kwa kampuni ya Symbion Power ya Marekani kwa thamani ya dola za milioni 120 za Marekani.
Wakati Machi 3, mwaka huu, Jaji Emilian Mushi, anayesikiliza kesi ya kuomba kusajiliwa kwa tuzo ya Dowans, alitoa amri ya kutaka pande zote mbili katika kesi hiyo kuacha mambo yote kama yalivyo na endapo watataka kufanya jambo lolote, wanapaswa kuomba kibali cha mahakama kwanza.
Pia alisema uuzwaji wa mitambo Dowans haukuomba kibali mahakamani.
Kahoho ambaye naye ni miongoni mwa wanaopinga Tuzo ya Dowans waliyopewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC) isisajiliwe na Mahakama Kuu ya Tanzania, aliwasilisha ombi hilo jana mchana mahakamani hapo, ambapo kwa mujibu wa hati ya maombi hayo ambayo NIPASHE inayo nakala yake, mahakama itoe amri ya kuwataka wadaiwa hao waweke dhamana dola milioni 120 za Marekani kama dhamana, na walipe gharama za kesi hiyo aliyoifungua jana.
Hata hivyo, ombi hilo ambalo limewasilishwa chini ya hati ya dharura bado haijapangiwa jaji wa kuanza kuisikiliza.
Kesi ya kupinga kusajiliwa tuzo ya Dowans itatajwa Julai 28, mwaka huu mbele ya Jaji Mushi.
Mbali na Kahoho, wengine wanaopinga tuzo hiyo isisajiliwe ni Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Shirika la Umeme nchini (Tanesco).
Januari 25, mwaka huu, Dowans iliwasilisha ombi lake la kutaka Mahakama Kuu ya Tanzania iisajili tuzo waliyopewa na Mahakama ya ICC.
Hata hivyo, siku chache baadaye, Tanesco, LHCR, Kahoho, waliwasilisha hati ya nia ya kupinga ombi hilo la kutaka tuzo hiyo isajiliwe.
Mahakama ya ICC, ilitoa hukumu ya kesi ya Dowans dhidi ya Tanesco, Novemba 15, mwaka jana, ambapo mahakama ilitia hatiani Tanesco kwa kosa la kuvunja mkataba na Dowans na ikaiamuru iilipe fidia ya Sh. bilioni 94.
Hata hivyo, hukumu hiyo imezua mjadala mkali hapa nchini kuanzia kwa viongozi wa serikali, vyama vya siasa na makundi mengine ambapo wengine wanataka Dowans ilipwe huku wengine wakitaka isilipwe.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment