ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, May 10, 2011

Dk Slaa aitupia CCM kombora jingine

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa
Boniface Meena, Sumbawanga
KATIBU Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amedai kuwa chama chake kina waraka wa CCM ambao chama hicho tawala kinakiri kuwa kimechoka na kimepoteza ladha na kuporomoka kwa kiasi kikubwa.

Alisema hayo jana kwenye mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Msakila mjini hapa. Alisema waraka huo ndiyo unaochangia hatua ya kuvuana magamba akidai kwamba umeeleza kuwa kitajibadilisha kutokana na mambo yaliyotokea... "Kujibadilisha kwenyewe ndo huko wanamtoa Makamba mkubwa na kumuweka Makamba mdogo," alisema.

Alidai kuwa waraka huo unaeleza kuwa CCM hivi sasa kimepoteza ladha na kimepoteza kura na kuporomoka kwa kiwango kikubwa."CCM Inashangaa kwamba mtu amekuja kwa miezi mitatu anatuporomoposha kwa asilimia 20!"alisema Dk Slaa.Alidai kuwa CCM katika waraka huo kinasema kuwa kimepoteza tunu za taifa ya uaminifu na uadilifu kwa kuwa hakikuchukua hatua suala la ufisadi haraka.

Dk Slaa alisema CCM kinaeleza kuwa kitajitahidi kirudi kwa wananchi kwa kuwa kilijisahau, lakini akasema Chadema kinawaeleza kuwa Watanzania hawahitaji tena mikutano yao.Alidai kuwa waraka huo haujazungumza chochote kuhusu ni jinsi gani chama hicho kitamtatulia Mtanzania matatizo yake ya maisha.

Akizungumzia Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Dk Slaa alisema sasa ni wakati wa kuacha kuzungumzia suala la kuchakachuliwa kura na kuanza kazi moja."Hakuna atakayekubali kuchakachuliwa tena na hivi sasa tunaanza mabadiliko ambayo yanahitaji mshikamano," alisema Dk Slaa.

Kuhusu mfumuko wa bei alisema walizungumza kuhusu hali ya bei ya sukari wakiwa Mwanza na kutoa siku sita kwa Rais Jakaya Kikwete kuhakikisha sukari imeshushwa na akafanya hivyo... "Kwa nini Chadema waseme ndipo atekeleze?" alihoji.

Alishutumu hatua ya serikali kutaka sukari ishushwe bei kwa nguvu huku ikiwaonya wafanyabiashara wadogo kutouza sukari kwa bei juu bila kuangalia kodi wanayowatoza... "Lazima kodi ishushwe viwandani na si kuwabana wafanyabiashara wakati kodi ikiwa chini na bei itashuka. Lakini pamoja na alichofanya bado tunahitaji bei ishuke."

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe alisema Taifa limepasuka kwa mujibu wa kipato cha mtu kutokana na hali mbaya inayoendelea kuizingira nchi.

Alisema jitihada lazima zifanywe ili kupunguza pengo lililopo kati ya maskini na matajiri kwa lengo la kuirudisha nchi katika mstari.Alisema hali ni mbaya na inawezekana maskini wakafika milioni 16 ifikapo mwaka 2015 kutokana na matajiri kuendelea kuwa matajiri na maskini kuendelea kuwa maskini.

"Lazima tupunguze huu wigo na ndicho kitu alichokuwa akikizungumza Dk Slaa wakati akigombea urais katika uchaguzi uliopita," alisema Zitto.

Katika suala la uchaguzi uliopita aliwaonya watu kusema kuwa walichakachuliwa kwenye uchaguzi mkuu hakubaliasni nazo kwa kuwa kama ilikuwas hivyo basi tume iliyomtangaza Silinde kuwa mbunge wa Mbozi Magharibi, ndiyo ililiyomchakachua mgombea wa CCM jimbo hilo.

Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Regia Mtema alisema licha ya Rais Kikwete kutamba kwamba uchumi wa nchi umekuwa kwa asilimia 7.2 lakini inashangaza kuona bado wananchi wa Tanzania ni maskini.

"Uchumi umekuwa kwa nani, mbona wanachi hali zao ni maskini, hii inamaanisha kuwa uchumi umekuwa kwa Rais na wafanyabiashara wakubwa na si kwa wananchi wa kawaida," alisema Mtema.Alisema CCM kimewaletea Watanzania umaskini na kuwataka waache kudanganywa kwa fulana, kofia na pombe ili kukichagua.

Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi alisema wananchi wa Sumbawanga na Tanzania nzima hawana haja ya kukichagua CCM tena.Alisema hali ya CCM ni mahututi kwa kuwa ugonjwa wa ufisadi unakiteketeza na kukichagua ni kuzidi kuisababishia Tanzania umaskini.

Hotuba hizo za viongozi na wabunge hao wa Chadema, zilikuja baada ya maandamano makubwa yaliyoanzia Kiwanda cha Unga.Maandamano hayo ya amani yalipambwa kwa pikipiki, magari na baiskeli huku wananchi wakiwa wametanda pembezoni mwa barabara hadi katika uwanja huo.



CHANZO:MWANANCHI

No comments: