ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, May 10, 2011

CUF, TLP wasema Mbowe anawakejeli

Na Gladness Mboma

BAADHI ya viongozi wa vyama vya upinzani wamesema kuwa kauli aliyotoa  Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Freeman Mbowe kuvialika
vyama hivyo kuungana kwa lengo la kutetea maslahi ya nchi ni kejeli na kwamba haongei kutoka moyoni.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, huku kila chama kikitamba kutetea maslahi ya wananchi, wapinzani hao kutoka vyama vya CUF, Tanzania Labour (TLP) na Sauti ya Umma (SAU), walisema hawaamini kama kweli Bw. Mbowe anamaanisha anachosema.

Juzi, akihutubia mkutano wa hadhara mjini Tunduma mkoani Mbeya, Bw. Mbowe alitaka wafuasi wa chama hicho kuwashawishi wafuasi wa vyama vingine, wakiwamo wa CCM, kushirikiana kutetea 'maslahi ya wananchi' badala ya kupingana wao kwa wao.


Akizungumza jana Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mkuu (Bara) wa Chama cha Wananchi (CUF), Bw. Julius Mtatiro alisema kuwa maneno anayozungumza na Mwenyekiti huyo cha CHADEMA na uhalisia ni vitu viwili tofauti.

Alisema kuwa CUF hawana ubaguzi na kipindi chote walichokuwa bungeni waliunda kambi moja ya upinzani, lakini wanashangazwa na CHADEMA walipoingia bungeni waliamua kubagua na kuwa na kambi ya peke yao bila ya kushirikisha vyama vingine vya upinzani.

"Mbowe ananishangaza sana kutaka tushirikiane kutetea maslahi ya nchi, mbona hiyo kazi ndiyo tunayoifanya CUF, kama wameshindwa kuwaunganisha wabunge wote wa vyama vya upinzani bungeni kwa lengo la kutetea maslahi ya watu bungeni anatualika kuungana kwa lipi," alihoji.

Bw. Mtatiro alisema kuwa CUF hawakubagua, hivyo wataendelea na programu zao za kila siku za kutetea ''maslahi wananchi' na siyo propaganda kama wafanyavyo CHADEMA na kuwataka waendelee na 'hamsini zao' kwani na wao wako kwa ajili ya kutetea maslahi ya nchi na si vinginevyo.

Naye Mawenyekiti wa Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Dkt. Paul Kyara alisema kuwa kuungana ni kitu cha maana na msingi kwa vyama vya upinzani, lakini alimtaka Bw. Mbowe kuonyesha kwanza vitendo na dhamira ya kweli kama anataka kufanya kazi pamoja na vyama hivyo.

Alisema kuwa anachozungumza Bw. Mbowe anaamini kwamba hataweza kutekeleza kutokana na jinsi chama hicho kilivyojijengea tabia ya kufanya kazi peke yake bila kupenda kushirikisha vyama vingine miaka yote, licha ya kutakiwa kufanya hivyo.

Naye Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Bw. Augustino Mrema alisema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi imeundwa na madiwani wa CHADEMA na TLP na CCM na kwa kuwa wanapigania maslahi ya wananchi TLP na CHADEMA walikubaliana kuunganisha nguvu.

Alisema kuwa cha kushangaza na kusikitisha licha ya kuingia makubaliano hayo na kuungana ngazi ya chini, walipofika bungeni, CHADEMA iliwanyanyapaa, hali inayoonyesha kwamba kauli ya Bw. Mbowe ni propaganda zao wenyewe.

"Kwanza chama changu siku zote kipo kwa ajili ya kutetea 'maslahi a wananchi' wa Tanzania, sasa sijui Mbowe anataka tutetee maslahi gani mengine, labda kama kuna kitu kingine," alisema.

Alisema kuwa kazi zake nzuri ndizo zilizomfanya achaguliwe tena kuwa mbunge wa Vunjo na kupewa nafasi mbalimbali, na kusisitiza kwamba vigezo vyote vya kiongozi anayepigania maslahi ya wananchi anayo na anajivunia historia yake.


CHANZO:MAJIRA

No comments: