ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, May 10, 2011

Wafanyabiashara wa bara wachomewa maduka Z`bar

Martin Fredrick, akiangalia mabaki ya eneo lililounguzwa moto na watu wasiojulikana kwenye duka lake ambapo mali zake zote ziliteketea kwa moto huo eneo la Pwani Mchangani, Kiwengwa, Zanzibar.
Watu 120 ambao ni wenyeji wa Tanzania Bara hawana mahali pakuishi baada ya nyumba zao kuchomwa moto katika kijiji cha Pwani, Mchangani katika Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Baadhi ya waathirika wa tukio hilo wamesema moto huo pia umetekekeza maduka na mali mbalimbali, zikiwemo bidhaa za mapambo ya utamaduni kama vile vinyago, nguo na pombe za aina mbali mbali.

Walisema wanakadiria kuwa moto huo umesababisha hasara ya Sh. milioni 400 baada ya nyumba hizo kuchomwa moto na watu wanaodaiwa kuwa ni wakazi wa kijiji hicho.
Walioshuhudia tukio hilo walisema kabla ya kuchomwa moto, nyumba na maduka hayo yalimwagiwa petroli na watu waliokuwa wamebeba mapanga na marungu.
Nyumba hizo na maduka yanamilikiwa na wafanyabiashara kutoka mkoa wa Arusha na Kilimanjaro, ambao walianza kuwekeza katika biashara hiyo tangu miaka ya 1990, sekta ya utalii ilipoanza kushamiri Zanzibar.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mselem Mtuliya, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na Jeshi la Polisi Zanzibar limeanza kufanya uchanguzi kutokana na tukio hilo.
Kamanda Mtulya alisema tukio hilo limetokea Jumamosi saa 10 jioni na kwamba polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.
Alisema tayari watu saba wamekamatwa na taratibu za kuwafikisha mahakamani zinaendelea.
Wakizungumza na NIPASHE waathirika wa tukio hilo, walisema walipojaribu kuokoa mali zao walizuiwa na kutishiwa kupigwa mapanga na marungu na watu wanaodhaniwa kuwa ndio waliochoma nyumba na maduka yao.
Waathirika waliokumbana na vitisho hivyo ni pamoja na Naisura Kurunde Lingido, Mariaeli Langaeli Ayo na Rashidi Ismail ambao ni miongoni mwa wamiliki wa mali zilizoungua.
Ayo alisema karibu nyumba 80, zenye maduka ya bidhaa za mapambo ya utamaduni ambazo soko lake ni watalii wanaotembelea ukanda wa pwani katika mkoa wa Kaskazini Ungugja, zimechomwa moto.
Alisema yeye na baadhi ya waathirika wengine wa tukio hilo wanawafahamu watu waliofanya kitendo hicho.
“Mara kwa mara walikuwa wanatuambia tufunge biashara na kuondoka kijijini hapa,” alisema na kuongeza kuwa: “Sisi hatukubaliani na hatua hiyo kwa sababu inakwenda kinyume na Katiba ya Tanzania.”
Ayo alisema ameshangazwa na kitendo cha viongozi wa jimbo kushindwa kuchukua hatua za kuzuia nia ya kufukuzwa kwao kijijini hapo wakati wana haki kufanya biashara kihalali katika eneo hilo.
Mwathirika mwingine, Gabriel Charles, alisema yeye na wenzake wamebaki na nguo walizovaa siku hiyo baada ya mali zote kuteketea.
“Tumebaki na nguo tulizovaa tu… mali zote zimeteketea moto kwa sababu walimwaga petroli na nyumba hizi za makuti na moto ulikuwa mkali tulishindwa kuokoa mali,” alisema Charles.
Waathirika hao wameomba serikali kuwashukulia hatua kali wahusika kwa vile vitendo walivyovifanya vinakwenda kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano ambayo imetoa haki kwa kila Mtanzania kuwa huru kuishi sehemu anayotaka na kufanyakazi halali.
Katibu wa Halmashauri ya wilaya ya Kaskazini A, Yahya Jabir Mwadini, alisema halmashauri haina taarifa juu ya kuwepo mpango wa kufukuzwa wafanyabiashara hao na ndio maana inawapa leseni za biashara.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji (sheha), Hemed Muhidini Kenge, alisema ameshangazwa na tukio hilo kwani serikali haijawahi kujadili suala la kuwafukuza wafanyabiashara kijijini hapo.
Alisema serikali ya kijiji kwa kushirikiana na serikali kuu itahakikisha suala hilo linashughulikiwa kwa kuzingatia sheria za nchi na kuwataka wananchi waache kuchukua sheria mkononi.
“Kwa upande wangu sina taarifa zozote za zoezi la kuchoma nyumba moto na watu kufukuzwa…. ni jambo jipya kwa upande wangu,” alisema Diwani wa Pwani, Mchangani, Haji Kidali na kuongeza kuwa kilichofanyika ni uvunjaji wa sheria.
Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai, Zanzibar (DCI), Muhidini Juma Mshiri, aliwataka wananchi wawe watulivu wakati Jeshi la Polisi likiendelea na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo.
“Vitendo vilivyofanyika ni uvunjaji wa sheria, lazima wahusika wakamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria,”alisema.
Hata hivyo, wananchi hao jana walianza kupokea msaada wa vyakula, ikiwa ni pamoja na mchele, unga wa sembe, maharage ambavyo vilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Pembe Juma Khamis.
Mkuu huyo wa Mkoa pia aliahidi serikali itaendelea kuchukua hatua mbali mbali ili kurejesha amani katika eneo hilo.
Wakati huo huo, Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd, aliwataka waathirika waorodheshe thamani ya mali walizopoteza ili serikali iangalie njia za kuwasaidia.
Balozi Seif pia ameagiza waathirika hao wapewe eneo jipya la kuishi na amekemea suala la ubaguzi, akisema kila raia wa Tanzania ana uhuru wa kuishi sehemu yoyote nchini Tanzania.
Balozi Seif alisema serikali imekasirishwa na kitendo hicho na kuviagiza vyombo vya sheria kuwakamata wote waliohusika na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.
Mapema mwaka huu baa tano, nne mkoa wa Mjini Magharibi na moja mkoa Kusini Unguja zilichomwa moto, lakini mpaka sasa hakuna aliyekamatwa na kufikishwa mahakamani.
Wakati huo huo, jijini Dar es Salaam vibanda 65 vya wafanyabiashara ndogondogo katika soko la Mchikichini vimeteketea kwa moto usiku wa kuamkia jana.
Chanzo cha moto huo hakijajulikana hadi sasa ingawa hasara kubwa imepatikana kutokana na mali zote zilizokuwemo kuungua.
Akizungumza na waathirika hao jana, Ofisa Masoko wa Manispaa hiyo, Athumani Mbelwa, aliwapa pole na kuwaambia kuwa halmashauri ya manispaa ya Ilala itawasaidia.
Hata hivyo, Mbelwa hakusema aina ya msaada watakaowasaidia, lakini alisema Meya wa Manispaa ya Ilala aliutaka uongozi wa soko hilo kuandika mchanganuo wa mali zilizoteketea na kuuwasilisha kwake ili ujadiliwe katika kikao cha madiwani kitakachofanyika leo.
Alisema Manispaa ikishapata mchanganuo huo itaujadili kwa kushirikiana na madiwani ili kuona namna gani wafanyabiashara hao watasaidiwa.
Kuhusu wamachinga hao kuhamia katika soko la Machinga Complex, Mbelwa alisema suala hilo liko nje ya uwezo wake kwa kuwa jengo hilo linamilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Naye Diwani wa Kata ya Mchikichini lilipo soko hilo, Gharib Riyami, aliliambia NIPASHE kuwa wakati wa tukio hilo la moto mali nyingi ziliibwa na vibaka waliokuwa wametanda katika eneo hilo huku wakilaghai kuwa wanatoa msaada wa kuokoa vitu.
Alisema yeye hana uwezo wa kifedha wa kuwasaidia wafanyabiashara hao akidai kwamba posho ya Sh. 200,000 anazolipwa kwa mwezi haziwezi kusaidia kitu kwani hasara iliyopatikana ni kubwa.
Aliongeza kuwa hiyo ni mara ya tatu kwa soko hilo la wamachinga kuungua moto na alitaka hatua zaidi za kiuchunguzi zichukuliwe ili kumaliza tatizo hilo katika siku za usoni.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa soko hilo, Deo Mkali aliliambia NIPASHE kuwa wamachinga hawana mpango wa kuhama katika soko la Mchikichini kwenda Machinga Complex.
Alisema mjadala wa kuhamia ama kutohamia Machinga Complex ulifungwa tangu mwaka jana na kwamba msimamo wa wafanyabiashara wote katika soko hilo ndiyo huo kwamba hawako tayari kuhama.
Alisema moja wa sababu zinazowafanya washindwe kuhamia katika jengo hilo jipya na la kisasa ni kutokana na serikali kutenga vibanda vidogo ambavyo havitoshi kwa mtu hata kusimama na kufanya biashara. (Soma Maoni Yetu ukurasa wa sita).
Imeandikwa na Mwinyi Sadalah Zanzibar na Richard Makore, Dar es Salaam.
CHANZO: NIPASHE

No comments: