MAASKOFU na wachungaji wa makanisa ya Pentekoste nchini, wamepinga hatua ya Serikali ya kuwalazimisha kuwasilisha hesabu zao za kila mwaka kwa Wizara ya Mambo ya Ndani wakati hawapewi ruzuku na mamlaka yoyote ya kiserikali.
Wakizungumza katika chakula cha pamoja cha usiku, Mchungaji wa Kanisa la Maombezi GRC Ubungo Kibangu, Anthony Lusekelo na Askofu wa Kanisa la Christian Mission Fellowship, Dk. Mgullu Kilimba, walisema kitendo hicho ni uonevu kwa makanisa hayo.
Chakula hicho kilichoandaliwa juzi kilihusisha wachungaji wa makanisa mbalimbali ya Pentekoste yaliyoko mjini Dar es Salaam kwa lengo la kudumisha umoja miongoni mwao na kuelezana namna ya kuwahamasisha waumini wao washiriki katika masuala mbalimbali ya kitaifa.
“Sisi hawatupi ruzuku kwa nini watudai return (mapato na matumizi) ya hesabu za kanisa…hii sheria ni kandamizi na lazima tuipinge kupitia Katiba mpya,” alisema Mchungaji Lusekelo.
Kwa mujibu wa Sheria namba 337 ya mwaka 1954 ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2002, Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia kwa Msajili wa Vyama vya Kijamii, ina mamlaka ya kuandikisha vyama vya kijamii.
Chini ya sheria hiyo, makanisa na vyama vingine vya kijamii vinatakiwa kuwasilisha hesabu zake za mapato na matumizi kwa msajili wake kila mwaka.
Ni sheria hiyo ambayo Mchungaji Lusekelo aliwaambia wachungaji kuwa ina upungufu kwani kitendo cha kutakiwa kupeleka hesabu wakati hupewi ruzuku ni unyanyasaji unaofanyiwa makanisa.
Kutokana na unyanyasaji huo kwa mujibu wa madai yao, viongozi hao wamehamasishana kupinga sheria hiyo wakati wa mchakato wa kujadili Katiba mpya.
Mchungaji Lusekelo alitaka Serikali ijenge heshima kwa makanisa hayo ambayo alidai yana waumini zaidi ya milioni tatu nchi nzima.
“Hivi sisi tunaokoa ndoa ngapi zisivunjike? Vibaka wangapi wanaacha kuiba kutokana na mahubiri yetu?” Alihoji Mchungaji huyo.
Makanisa hayo yamekuwa yakipata fedha za michango, sadaka na zaka kutoka kwa waumini wao, lakini pia yamekuwa yakipata misaada mbalimbali kutoka nje ya nchi ambayo Mchungaji Lusekelo, alisema fedha hizo za wafadhili zinachangia kuwasambaratisha.
“Hizi fedha ambazo makanisa yanapata kutoka nje kwa wafadhili, ndio chanzo cha kutuvuruga, mchungaji hapa kanisa lake likipata ufadhili tu vurugu zinaanza, jambo hili kwa kweli sio zuri,” alisema Mchungaji huyo.
Kiongozi huyo wa kiroho pia aliwataka wachungaji wa makanisa hayo kuhamasisha waumini wao kuombea mjadala wa Katiba mpya ili kusizuke ghasia na fujo wakati wa mchakato wa kuelekea kuipata Katiba hiyo.
Katika eneo ambalo Mchungaji Lusekelo alitaka waumini wa makanisa hayo waliboreshe ni kupinga Rais kuteua na kuunda Tume ya Uchaguzi ambayo alisema inafanya kusiwepo uchaguzi huru na wa haki.
“Tunahitaji tume huru ambayo Rais ajue kuwa akiboronga anaweza kuondolewa kwa sanduku la kura, hii ya sasa hivi inaonekana kama ya mchezaji na mwamuzi wakati huo huo, haki haiwezi kutendeka,” alidai Mchungaji Lusekelo.
Kwa upande wake, Dk. Kilimba, alitoa mwito kwa wachungaji hao kuhamasisha waumini wao kufanya maombi ili mchakato huo wa Katiba mpya usitawaliwe na jazba wala vurugu.
“Hii ni nchi yetu sote sio ya chama fulani, tuliombee Taifa letu na rasilimali zetu ili zitumike vizuri kwa manufaa ya nchi yetu,” alisema Dk. Kilimba. Wachungaji hao pia wameazimia wakati wa mchakato wa Katiba mpya kupinga kipengele cha sheria kinachoyataka makanisa kusajiliwa kama zinavyosajiliwa kampuni nyingine.
Walisema Tanzania inawahitaji wachungaji waisaidie kwani hali ya kisiasa imebadilika kutokana na kuwepo mwamko mkubwa wa kisiasa kutoka kwa vijana na wasomi.
“Upepo huu wa kisiasa ni mkubwa hivyo sisi wachungaji kazi yetu ni kuomba upepo huu usisababishe vurugu na fujo katika nchi yetu,” alisema Lusekelo.
Pia aliwataka wachungaji hao kusimama kidete wakati wa mchakato wa Katiba mpya wasibaguliwe kama ambavyo imekuwa siku za nyuma.
Alisema licha ya walokole kuwa zaidi ya milioni tatu nchini, lakini wachungaji wao hawapewi hata vipindi kwenye vyombo vya habari vya Serikali kama inavyofanyika kwa madhehebu mengine.
CHANZO:HABARI LEO
No comments:
Post a Comment