ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, May 3, 2011

Magari ya mitumba yaitikisa Chadema

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa
Leon Bahati
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimekiri kwamba suala la ununuzi wa magari yaliyotumika lilizua mjadala kwenye kikao chake cha Kamati Kuu kilichomalizika Jumatatu wiki hii.
Maelezo ya mvutano huo yalitolewa jana na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari baada ya gazeti hili toleo la Jumatatu kuandika juu ya suala hilo.
Hata hivyo, Dk Slaa alisisitiza kuwa mvutano huo ulikuwa wa kawaida hasa ikizingatiwa kuwa ni suala ambalo haliepukiki penye mjadala wa watu wengi akisisitiza kwamba demokrasia ndiyo iliyoamua.

Gazeti hili liliripoti kuwa mkutano huo ulitokana na baadhi ya wajumbe kupinga na wengine kuunga mkono suala la ununuzi wa magari yaliyotumika yenye thamani ya Sh480 milioni.
Baadhi ya waliokuwa wanapinga mkakati huo walisema kuwa ulikuwa unalenga kumnufaisha Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe ambaye alikuwa achukue nafasi hiyo kukiuzia chama magari ambayo tayari ameyatumia.
Miongoni mwa wajumbe wa Baraza hilo, Profesa Mwesiga Baregu na Dk Kitila Mkumbo walinukuliwa wakisema kwamba isingekuwa sahihi kwa chama hicho kinachopinga ufisadi kufanya ufisadi kwa kununua magari chakavu wakati wamekuwa wakiibana serikali.
Akitoa ufafanuzi huo jana, Dk Slaa alisema msuguano huo ulikuwa ni wa kawaida na ulikuwa sehemu ya kuwezesha demokrasia kuchukua mkondo wake. Alikiri kuwa kwenye mchakato huo, Mbowe ana magari matatu ambayo chama kinataka kuyanunua.
Alisema hoja hiyo ilimalizika kwa Baraza kuamua kuwa Mbowe aendelee kushawishiwa ili akubali kukiuzia chama magari hayo. Alielezea kuwa magari hayo aliyanunua na yakaanza kutumiwa na chama kwenye kampeni za uchaguzi uliopita.
"Magari hayo Mheshimiwa Mbowe aliyanunua kwa ajili ya biashara zake lakini kwa kuwa chama kilikuwa katika matatizo ya usafiri, akakubali kuyatoa yakisaidie ili baadaye tumrejeshee," alisema Dk Slaa na kuongeza kuwa magari mawili yanaendelea kutumiwa na chama hivyo ni vyema wayanunue.
Kuhusu chama hicho kununua vitu vilivyotumika wakati kimekuwa kikiipinga vikali serikali kutumia vitu vilivyotumika, Dk Slaa alisema njia inayotumiwa na Chadema iko wazi zaidi ukilinganisha na ile ya serikali.
Alidai kuwa kwenye michakato ya ununuzi serikalini kuna mazingira mengi yanayoruhusu ufisadi hasa katika kujadili bei lakini suala la kununua magari ya Mbowe, suala kama hilo haliwezi kupata nafasi.

Mshahara wa Dk Slaa
Katika hatua nyingine, Mbowe alisema kuwa chama hicho kimeamua kumlipa Dk Slaa mshahara na maslahi yanayolingana na anayopata mbunge.Alisema hiyo ni kwa sababu chama hicho ndicho kilichokuwa kimemshawishi aache kugombea ubunge katika Jimbo la Karatu, Arusha ambako alikuwa na nafasi kubwa ya kushinda na kumtaka agombee urais ambao mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete alitangazwa kuwa mshindi.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mbowe alisema uamuzi huo ulifuata taratibu zote ikiwa ni pamoja na vikao vikuu vya chama hicho, kama vile Kamati Kuu na kisha  kuidhinisha malipo hayo.
"Itakumbukwa kuwa Mheshimiwa Dk Slaa hakuomba nafasi ya kugombea uraisi, aliombwa. Tunajua alikuwa mbunge na alikuwa na nafasi kubwa ya kushinda tena nafasi hiyo, lakini akakubali ombi la chama," alisema Mbowe na kuongeza: "Hii siyo mchezo! Uamuzi wa namna hiyo ni wa kujitoa. Ndiyo maana Kamati Kuu ikakubali apate mshahara na marupurupu sawa na yale ya mbunge."
Mbunge anakadiriwa kuwa anapata mshahara pamoja na marupurupu yanayokaribia kufikia Sh7 milioni kwa mwezi.
Chadema kilitumia Sh1.3 bilioni kusaka urais 2010
Akizungumzia Uchaguzi Mkuu uliopita, Mbowe aliwaambia waandishi wa habari kuwa chama chake kilitumia Sh1.3 bilioni katika kampeni za uras.
Alivitaja vyanzo vya fedha hizo kuwa ni Sh 338.9 milioni za ruzuku, Sh 235.9 milioni kutoka kwa marafiki, Sh32 milioni michango mbalimbali ya wanachama na mali mbalimbali za watu zenye thamani ya Sh719.7 milioni.

CHANZO:MWANANCHI

No comments: