ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, May 5, 2011

Mkapa ajitosa rasmi kumtetea Prof Mahalu

Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa
Tausi Ally na James Magai
RAIS mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ameridhia kupanda kizimbani kumtetea aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu na mwenzake aliyekuwa Ofisa Utawala wa ubalozi huo, Grace Martin wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.

Mahalu na mwenzake wanakabiliwa na mashtaka hayo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, wakidaiwa kuhujumu uchumi kwa kuisababishia Serikali hasara ya Euro 2,065,827.60.
Wanadaiwa kusababisha hasara hiyo kupitia mchakato wa ununuzi wa jengo la ubalozi huo, wakati wa utumishi wao.
 Tayari Rais Mkapa amewasilisha mahakamani hapo hati yake ya kiapo akimtetea Profesa Mahalu na mwenzake kuhusiana na tuhuma hizo zinazowakabili.

Kwa mujibu wa wakili wa kina Mahalu, Mabere Marando, ikiwa hati hiyo ya kiapo itakubaliwa na upande wa mashtaka na kisha kupokelewa mahakamani basi itatumika kama kielelezo cha ushahidi kwa upande wa utetezi bila Mkapa mwenyewe kulazimika kufika mahakamani.

Lakini kama hati hiyo ya kiapo itakataliwa na upande wa mashtaka, basi Mkapa ameridhia kuwa yuko tayari kufika mahakamani mwenyewe na kutoa ushahidi wake mbele ya mahakama hiyo.
Katika hati hiyo ya kiapo, Mkapa amemtetea Profesa Mahalu kuwa amefanya naye kazi kwa muda mrefu na anamjua kuwa ni mtu mwaminifu, mtiifu na mchakapakazi. 

Mkapa alieleza katika hati yake hiyo kuwa mchakato wa ununuzi wa jengo hilo ulifanyika wakati wa uongozi wake na kwamba alikuwa akijua kila kilichokuwa kikiendelea kuhusiana na ununuzi huo na kwamba ulifanyika kwa mujibu wa sheria.

Alifafanua kuwa mpango wa ununuzi wa jengo hilo ulikuwa ni utekelezaji wa Sera ya Serikali wa kuwa na majengo yake ya kudumu katika kila ubalozi kwa kununua au kujenga ikiwa ni njia ya kupunguza gharama za upangaji.
Aliongeza kuwa Serikali yake ilimpa Profesa Mahalu mamlaka yote ya kusimamia na kutekeleza mchakato wa ununuzi wa jengo hilo kupitia nguvu ya kisheria aliyopewa na Serikali yake.

Mkapa alisisitiza kuwa kupitia utaratibu wa Serikali alikuwa akijua kuwa  taarifa ya uthamini wa jengo hilo iliyofanywa na Wizara ya Ujenzi ilikuwa ni Dola za Marekani 3.0 milioni wakati Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ilikadiriwa Euro 5.5 milioni

“Kupitia utaratibu wa Serikali nilifahamu kuwa jengo hilo lilinunuliwa kwa gharama ya Dola za Marekani 3.0milioni  sawa na Euro 3,098,741.40,” alisema Mkapa na  kuongeza:
“Kupitia utaratibu wa Serikali nilikuwa nafahamu na hivyo kuidhinisha mchakato wote na taratibu za ununuzi wa jengo hilo lililoko Vialle Cortina d’Ampezzo 185 jijini Rome.”

Mkapa pia alisema kuwa alitambua kuwapo kwa mikataba miwili katika ununuzi wa jengo hilo na kwamba yeye mwenyewe ndiye aliruhusu kufanyika kwa kuwa ilikuwa ni muhimu katika kutimiza maslahi ya taifa.
Pia Mkapa alisisitiza kuwa alikuwa na bado anatambua taarifa ya serikali bungeni ya Agosti 3, 2004  iliyoeleza na kuthibitisha kuwa taratibu zote za ununuzi wa jengo hilo zilifuatwa kwa mujibu wa maelekezo ya Serikali na kwamba dalali alilipwa kikamilifu.

“Kwa kipindi chote ambacho nimefanya kazi na Balozi Mahalu katika nafasi mbalimbali za utumishi wa Serikali ameonesha tabia thabiti na za dhati, uaminifu, utiifu, uchapakazi na ubora," alisema Mkapa.
Alisema kuwa sifa hizo zilimfanya atunukiwe na Rais wa Italia tuzo ya Heshima ya Juu wakati wa kuadhimisha siku ya taifa hilo, muda mrefu baada ya kuwa ameondoka nchini humo. 

Jumla ya mashahidi 10 wanatarajiwa kumtetea Mahalu katika kesi hiyo. Mbali na Mkapa ambaye ameshawasilisha hati yake ya kiapo na kuridhia kupanda kizimbani kumtetea kama atahitajika, pia yumo Rais Jakaya Kikwete.
Hata hivyo, Rais Kikwete ambaye tayari ameshapelekewa taarifa ya nia ya kumwita kufika kutoa ushahidi kwa siku na tarehe ambayo atakuwa na nafasi bado hajajibu kama atakuwa tayari au la.

Mashahidi wengine ni pamoja na Basil Mramba ambaye pia anakabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia Serikali hasara ya Sh11 bilioni pamoja na wenzake wawili, Daniel Yona na Gray Mgonja.
Mahalu na Grace wanadaiwa kula njama na kutenda makosa hayo katika tarehe tofauti na katika maeneo tofauti huko nchini Italia, likiwamo la kumpotosha mwajiri wao katika hati ya matumizi.

Miongoni mwa mashtaka hayo ni kwamba Septemba 23 2002 jijini Rome, washtakiwa wakiwa waajiriwa wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, walisaini vocha yenye namba D2/9/23/9/02 ikionyesha kuwa bei ya ununuzi wa jengo la ubalozi ni Euro 3,098,741.58, maelezo ambayo yalikuwa ni ya uongo na yenye nia ya kumdanganya mwajiri wao.


CHANZO:MWANANCHI

1 comment:

kilitime said...

kipindi cha mkapa ndicho ufisadi umefanyika wa kutisha,kwa hio mmkapa sio mtu safi na hastahili kumtetea mtu yeyote.mkapa tutajie mali zako ni kiasi gani baada ya kuondoka IKULU kama wewe ni mtu safi na unastahili kumtetea huyo jamaa.