WATU watano wameuawa na wengine kujeruhiwa katika mapambano kati ya polisi na raia wanaodaiwa kuvamia mgodi wa North Mara Barrick, wilayani Tarime jana alfajiri kwa lengo la kupora mawe ya dhahabu.
Watu wapatao 800 walivamia mgodi huo kwa lengo la kuchukua dhahabu kutoka kinu cha kusagisha mawe hali iliyowalazimu polisi kutumia risasi za moto.
Licha ya waliouawa, watu 10 wakiwamo polisi walijeruhiwa katika mapambano hayo ambayo wananchi walikuwa wakitumia silaha za jadi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tarime/Rorya, Constantine Massawe, alisema jana kuwa, kundi hilo la wavamizi lilikuwa na mapanga, marungu, makombeo na mawe.
Alisema, alituma kikosi cha Polisi waliokuwa na mabomu kuongeza nguvu katika mapambano na wavamizi hao waliojihami kwa mawe na marungu.
Alisema, polisi walilazimika kutumia risasi za moto baada ya kuzidiwa nguvu na kundi hilo.
Aliwataja waliouawa kuwa ni Chacha Ngoko (25) mkazi wa Kewanja Nyamongo, Emmanuel Ghati (19) wa kijiji cha Nyakunguru, Chacha Mwasi (23) wa Bisarwi Komaswa.
Wengine wawili majina yao hayajambuliwa ingawa zipo tetesi kuwa ni wakazi wa Serengeti.
Miili imehifadhiwa katika hospitali ya wilaya ya Tarime ikisubiri kuchukuliwa na ndugu zao.
Majeruhi waliolazwa katika hospitali ya wilaya wodi namba 7 wakiwa na majeraha ya risasi, ni pamoja na Samwel Nyangoye (35) mkazi wa Sirari aliye mahututi baada ya kupigwa risasi begani na kutokea kifuani.
Majeruhi wengine ni Mwikwabe Marwa, Frank Joseph (20) mkazi wa Kewanja Nyamongo aliyepigwa risasi kiunoni, Nyangi Mkenye (30) wa Matongo aliyepigwa risasi mguu wa kushoto na kuvunjika.
Wengine sita wanatibiwa katika hospitali ya Sungusungu, Nyamongo. Kamanda Massawe aliwataja askari wanne waliojeruhiwa kuwa ni Simon Mrashan ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Kuzuia Wizi wa Mifugo wa Wilaya ya Tarime aliyepigwa mawe ubavuni kwa kombeo. Alisema hali yake ni mbaya.
Askari wengine ni Hassan Maya ambaye pia hali yake ni mbaya. Askari wengine wa kawaida ambao majina hayakutajwa, walikatwa mapanga na kupigwa mawe.
Katika mtafaruku huo, magari ya Polisi na ya mgodi yaliharibiwa kwa kuvunjwa vioo kwa mawe. Hilo ni tukio la tatu mgodi huo kuvamiwa katika kipindi cha siku nne.
Alhamisi wiki iliyopita, Polisi ilisema watu zaidi ya 500 wa vijiji jirani na mgodi huo, walivamia kwa lengo la kupora mawe ya dhahabu.
Uvamizi mwingine ulifanyika Jumamosi. Miongoni mwa watu waliozungumzia hali hiyo ni pamoja na aliyekuwa Diwani wa eneo hilo lenye mgodi, Augustino Neto, aliyeishauri Serikali itafute utaratibu wa kuwapa wananchi maeneo ya kuchimba dhahabu ili kuepusha chuki iliyojengeka baina ya jamii dhidi ya mgodi huo.
Kutoka Moshi, Arnold Swai, anaripoti kwamba watu wanne wameuawa na Polisi mkoani Kilimanjaro wakituhumiwa kutaka kupora katika Klabu ya usiku ya Malindi na duka la silaha mjini humo.
Wakizungumza na gazeti hili mashuhuda wa tukio hilo walisema majambazi hao walifika kwenye klabu hiyo juzi saa 7 usiku na kupora fedha za mauzo ya siku hiyo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Lucas Ng’hoboko aliwambia waandishi wa habari kuwa majambazi hao waliuawa na polisi wa doria baada ya msamaria mwema kutoa taarifa.
Alisema waliuawa katika eneo la kampuni ya kuuza matairi ya General Tyre, meta chache kutoka ilipo klabu hiyo.
Aliwataja waliouawa kuwa ni Nicodemas Kinyaa ‘Samora’ (37) mkazi wa Pasua Matindigani ambaye ni dereva teksi, Juma Sanga (27) fundi seremala mkazi wa Njoro Makaburini, Musa Sekuye kondakta wa daladala na Stephano Kivuyo ‘Msumbiji au Dogoo’ (25).
Kwa mujibu wa Kamanda, walipopekuliwa walikutwa na bunduki moja aina ya shotgun iliyokatwa kitako, ikiwa imefutwa namba za usajili na ikiwa pia na risasi nne. Walikutwa pia na mapanga mawili na simu nne za mkononi.
Walikuwa wakitumia gari aina ya Toyota Corolla namba T 224 AMW, inayofanya biashara ya teksi mjini humo. Ina namba za ubavuni Tax 715, na mmiliki wake ni Rose-Line Shirima (37) ambaye ni muuguzi wa Hosptali ya Rufaa ya KCMC.
“Dereva anayetambulika kwenye hii teksi ni Evans Sebastian, ambapo yeye alimkodishia dereva mwenzake Kinyaa baada ya kumwomba gari hilo alitumie kuchukua wageni wake,” alisema Kamanda Ng’hoboko.
Kamanda alisema, katika upekuzi waligundua simu tatu walizokamatwa nazo wakiwa wamezipora Mei 12 eneo la Soweto na kupora Sh 1,276,600 kwa kutumia bunduki.
Evans ambaye alikodisha gari hilo kwa watu hao anashikiliwa na Polisi kwa mahojiano zaidi. Miili imehifadhiwa katika hospitali ya mkoa ya Mawenzi mjini Moshi.
Abby Nkungu, anaripoti kutoka Singida Polisi mkoani Singida inawashikilia watu watatu, kwa mauaji ya watu wanne katika matukio mawili tofauti yaliyotokea mwishoni mwa wiki.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Celina Kaluba, alieleza kuwa katika tukio la kwanza lililotokea Mei 15 saa 4 asubuhi Itigi, Juma Rashid (32), ambaye ni dereva wa pikipiki alikodiwa na Geu Njongani ili ampeleke kijiji cha Tura, mkoani Tabora.
Inadaiwa kuwa, walipofika njiani, Njongani alimuua mwenye pikipiki kwa kumkata shingo kwa kutumia kitu chenye ncha kali na kumpora pikipiki namba T 962 BNF.
Muda mfupi baada ya kupora pikipiki hiyo, huku akiwa anaitumia kwenda Tura, mtu huyo alipata ajali na kuumia.
Kamanda Kaluba alisema, kuumia huko kulimlazimisha Njongani, ambaye ni mkazi wa Tura, kurudi Itigi ili akatibiwe Hospitali ya Misheni St Gaspar. "Alipofika Itigi, wananchi walimshitukia na kutaka kumpa kipigo.
Kuona hivyo, Njongani alikimbilia jengo la benki ya NMB ili kujisalimisha kwa askari waliokuwa kwenye lindo" alisema Kamanda huyo.
Kamanda Kaluba alisema, wananchi waliwazidi nguvu askari waliokuwa zamu, wakaingia ndani ya uzio wa benki, kisha wakaanza kumpiga mtuhumiwa kwa mawe na marungu hadi kusababisha kifo chake papo hapo.
Katika tukio hilo, watu wawili, Mohammed Masudi (24) na David Nicodemo (25) wote wa Itigi wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma ya kuwarushia askari mawe wakati wa tukio hilo.
Katika tukio la pili, Raymond Erasto (26) mkazi wa Ngimu Singida Vijijini kuwa na matatizo ya akili, anatuhumiwa kuwaua baba na mama yake mzazi na kumjeruhi mdogo wake mwenye umri wa miaka mitatu.
Aliwakata kwa panga mwilini. Tukio hilo lilitokea juzi saa moja usiku ambapo waliouawa ni Erasto Kilakuno (78) na Frida Dule (57) wakati Ester Elihuruma alijeruhiwa. Mtuhumiwa Raymond anashikiliwa na polisi.
CHANZO:HABARI LEO
No comments:
Post a Comment