ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, May 17, 2011

Ufanye nini unapogundua mpenzi wako anakusaliti?-GPL

Wanaume wengi wanapobaini kuwa wapenzi wao wanawasaliti, hutunisha misuli  na kuonesha umwamba kwa kuwatwanga makonde wapenzi wao au kuwafanyia ‘mbaya’ wale waliowanasa na wakati mwingine hufikia uamuzi wa kukatiza uhai wao kwa wivu. 
Lakini uchunguzi wa kitaalamu  unaonesha kuwa, ubabe haukomeshi tabia ya usaliti katika uhusiano.


Kuna wengi ambao waliwafumania wake/waume zao, wakawapiga na kuwajeruhi, lakini wakajikuta hawakukomesha tatizo, zaidi ya kuwapa usugu wa kuendeleza usaliti tena kwa dharau huku wakibembelezana kwa maneno haya: “Mzushi kaenda kazini njoo sasa hivi Wapendanao Gesti” au “Vipi  yule bwege alikuuliza jana ulipochelewa kurudi?”

Katika hali ya kawaida usaliti ni jambo linalouma kwa kiwango kikubwa mno. Katika mapenzi hakuna suala la kuazimana mume/mke. Watu huazimana magari,  pesa, au kitu chochote cha thamani lakini siyo wapenzi!

Je, adhabu au kuachana baada ya kufumaniana kunasaidia? Jibu ni hapana  hakusaidii, kwani ukimpiga adhabu inaishia hapo hapo,  kesho yake watakapokutana watakusaliti tena huku wakikuporomoshea matusi ambayo kama utayasikia ni lazima uzirai.

Maamuzi ya kuacha nayo hayasaidii kwani ukimwacha mpenzi wako hujamtibu, utakuwa umetoa mwanya wa yeye kuendelea kukusaliti na kukuumiza zaidi pale macho yako yatakapowaona wameshikana na mwanaume mwingine wakijivinjari mitaani kwa mbwembwe.
Ukiamua kuua na wewe utauawa, huo nao ni uamuzi wa kijinga kwani binadamu wenzako watakucheka kwa uzembe wa kufikiri na kutodhibiti hasira.

Nijuavyo usaliti upo kila siku, si tunawaona wake na wapenzi wa watu wanaingia gesti kujiachia? Ni vema kuwa na akiba ya mawazo kama hujamfuma mpenzi wako leo kuna siku utakutana na mazingira tata au meseji kali itakayokuwa ikibembeleza kwa maneno matamu ambayo hujawahi kumwambia!.

Swali la kujiuliza ni kwamba, utafanyaje baada ya kubaini hivyo?
NJIA NI HII:  Lazima mpenzi wako ajue na awe na uhakika juu ya tabia yake kwamba ukweli wa vitendo vyake unavifahamu tena kwa ushahidi.
Mfano kama umemkuta sehemu akifanya uchafu wake, muoneshe kwamba umemuona, kisha ondoka eneo hilo.

Ukifika nyumbani endelea kunywa maji ili kupoza presha. Akirudi mpenzi wako jitahidi kuzuia hasira zako, mkaribishe kwa bashasha, lakini usimuulize chochote kuhusu fumanizi lako, mwache aendelee kujiuliza mwenyewe utamfanya nini.

Au kama umenasa meseji za kimahaba kutoka kwa mwizi wako, zitume kwenye simu yako kwanza, kisha baada ya kumaliza uchunguzi wako mtumie tena sms hizo mkeo/mumeo kwa lengo la kumjulisha kwamba unajua kinachoendelea halafu usimuulize kitu.
Endelea kumpenda na ikiwezekana ongeza upendo ili kumfanya ahisi utofauti wa siku zote na hivyo kumfanya azidi kuumizwa na usaliti wake.

Ukifanya hivyo mpenzi wako ataingiwa na wasi wasi na kujiuliza kwa nini umpende wakati amekusaliti? Hapo atakosa raha na hataamini kama umemsamehe, atakachofikiria yeye wakati wote ni adhabu ambayo atakuwa akiibashiri kichwani mwake na hivyo kuteseka kisaikolojia.

Wataalamu wa masuala ya mapenzi wanasema adhabu  ya kiwango cha juu  kabisa kwa msaliti ni kuadhibiwa kwa upole si kwa kupigwa kwani kupiga husafisha uovu na kumfanya mtu aliyefanyiwa hivyo azidi kuamini kuwa tayari  ameshalipwa gharama ya kosa alilofanya  na yamekwisha.

Najua kuna baadhi ya watu ambao watapingana na ukweli huu, lakini ni vema wakajaribu ili kuthibitisha ubora kuliko kung’ang’ania kupigana, matokeo yake ni kuua na kuishia kufungwa jela.

Angalizo :
Ukweli utabaki palepale kuwa, yataka moyo wa ujasiri sana kuvumilia usaliti wa mwenza wako juu ya penzi lenu, hivyo ni bora tuzidi kuwa waaminifu katika uhusiano wetu. Lakini njia za kitaalamu ambazo nimezi ainisha hapo juu, ni njia bora na sahihi kabisa kutatua tatizo la usaliti wa mwenza wako. Hivyo ni muhimu kuzingatia na kutekeleza.

Mpaka hapa naamini msomaji wangu nitakuwa nimekupa kitu cha tofauti, nitafurahi kama utakifuata. Nakutakia mema kwenye maisha yako ya kimapenzi. Asante kwa kuwa nami wiki hii!

No comments: