Hofu imetanda juu ya usalama wa fedha za wateja katika baadhi ya benki nchini baada ya kugundulika kwa staili mpya ya wizi unaohusu watumishi wa taasisi hizo.
Wizi huu umegundulika baada ya watumishi wasio waaminifu kuhamisha fedha za wateja bila wenyewe kufahamu wizi huo.
Tukio la hivi karibuni kabisa la ubazazi huo liligundulika jana na Jeshi la Polisi mkoani Mwanza, linawashikilia wafanyakazi wawili wa Benki ya Diamond Trust tawi la Mwanza kwa madai ya kugushi nyaraka za benki hiyo na kujipatia isivyo halali kiasi cha Sh. milioni 180 zilizotakiwa kuingizwa katika akaunti ya mteja mmoja.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Nonosius Komba, alithibitisha jana kuwa wafanyakazi hao walikamatwa baada ya mteja kubaini kiasi cha fedha alichoweka katika akaunti yake kilikuwa hakimo licha ya kuwa na nakala ya hati ya kuwekea fedha hizo.
Kamanda Komba alisema jeshi lake limewatia mbaroni watumishi wawili ambao hadi sasa ndio wamebainika kuhusika katika wizi huo wa Sh. milioni 180, lakini hakuwataja majina wafanyakazi hao kwa madai kuwa uchunguzi bado unaendelea.
Wizi huo uligundulika kati ya Mei 12 na 13 mwaka huu, baada ya mteja kufuatilia katika akaunti yake na kukuta kuna upungufu mkubwa wa kiasi hicho cha fedha na baada ya kulalamika kwa uongozi wa benki hiyo na kufuatilia ndipo iligundulika kuwa wafanyakazi hao walihusika na wizi huo na kutiwa mbaroni mara moja.
“Pamoja na kuwakamata na kuwafanyia mahojiano, bado uchunguzi unaendelea, siwezi kuwataja majina yao kwa sasa, lakini hao ndio hadi sasa wamebainika kuhusika na tukio hilo,” alisema Komba.
Taarifa nyingine zinadai kuwa wafanyakazi hao, ambao ni makarani (teller) wa benki hiyo kwa nyakati tofauti walipokea kiasi cha Sh. milioni 150, ambacho walitakiwa kukiweka katika akaunti ya mteja huyo na kiasi kingine cha Sh. milioni 30, ambapo walitoa karatasi iliyoonyesha fedha hizo zimewekwa katika akaunti.
Hakuna kiongozi wa benki hiyo ya DTB tawi la Mwanza aliyekubali kuzungumzia wizi huo kwa madai kuwa wao si wasemaji kwa masuala ya benki na kuwataka waandishi kuwasiliana na Makao Makuu yao yaliyoko jijini Dar es Salaam.
Taarifa hizo zilidai kuwa benki hiyo imeanza kufanya uchunguzi wa kina kufuatilia akaunti mbalimbali za wateja wao ambao wafanyakazi hao wamekuwa wakizihudumia, ili kujua kama pia wamehusika na wizi kama huo kwa mteja mwingine.
Mfanyakazi mmoja wa benki hiyo, ambaye hakupenda kutajwa jina alisema kuwa wanachofanya chini ya usimamizi wa Jeshi la Polisi Kitengo kinachojishughulikia makosa ya kughushi (Fraud), kinafuatilia akaunti za wateja wakubwa ambao walikuwa wakihudumiwa kila mara na watumishi hao ili kujua kama kuna fedha zimepotea.
Hii ni staili mpya ya wizi katika benki nchini, baada ya ule wa mwaka jana wa kuchota fedha kupitia mashine za kutolewa fedha (ATM) ambao uliwahusisha wazungu wawili.
Kadhalika, kumekuwa na wizi mwingine kwa njia ya mitandao na kiasi kikubwa cha fedha kimekwisha kuchotwa kwa njia hizo.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment