ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, May 17, 2011

Yanga yalipa mil. 15/- kuvunja mkataba wa Asamoah

Uongozi wa mabingwa wa soka Tanzania Bara, Yanga, jana ulituma fedha kwa klabu ya FC Jagodina ya Serbia kwa ajili ya kuvunja mkataba wa mshambuliaji Kenneth Asamoah ili awe huru kujiunga na klabu hiyo ya Jangwani.
Jana asubuhi, kiongozi mmoja wa Yanga aliyekuwa ameambatana na Asamoah, walionekana wakiingia katika benki ya katikati ya jiji la Dar es Salaam na taarifa kutoka ndani ya uongozi wa Yanga zilithibitisha kutumwa pesa kwa Jagodina ili kuvunja mkataba wa Asamoah uliobaki miezi sita.
Yanga walituma dola za Marekani 10,000 (Sh. milioni 15) ikiwa ni gharama za kuvunja mkataba wa Asamoah.

Chanzo kilisema kwamba baada ya Yanga kufanya mazungumzo na Jagodina, walikubaliana kulipa kiasi hicho cha fedha ili kumtwaa mchezaji huyo aliyewahi kutua nchini Julai mwaka jana na kuonyesha kiwango cha juu wakati akijaribiwa na wanajangwani.
"Ni kweli tumelipa kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kuvunja mkataba na klabu hiyo ya Serbia uliokuwa umebakia miezi sita tu kumalizika," alisema mmoja wa viongozi wa Yanga.
Aliongeza kuwa baada ya kukamilisha mazungumzo hayo, sasa hivi wanachosubiri ni muda rasmi wa kipindi cha usajili ili watekeleze taratibu za uhamisho wa mshambuliaji huyo wa kimataifa kutoka Ghana.
Mwaka jana, Yanga walikosa kibali cha kumtumia Asamoah kutokana na madai kwamba taarifa zilizokuwa zikitumwa kwa mtandao kati ya Yanga na Jagodina zilikuwa zikitofautiana.
Mbali na Asamoah, nyota wengine wapya wanaotarajiwa kuichezea Yanga msimu ujao ni Pius Kisambale, Godfrey Tahita na kipa Saidi Mohamed.
CHANZO: NIPASHE

No comments: