
Tupo kwenye mada yetu na hii ni sehemu ya tatu. Lengo la hapa ni kukutaka ujitambue ili kukuwezesha kuwa kamili kimapenzi. Anza leo kujichunguza, ni wapi upo imara, shikilia hapo, sehemu yenye udhaifu shunghulikia.
Ni kosa kubwa kuishi ndani ya makosa kwa muda mrefu. Katika hili ndipo unapohitaji kwa nguvu kubwa kujisoma na kujijadili wewe mwenyewe ili ujue njia sahihi za kuishi ukihitaji kuwa bora.
Uhusiano wa kimapenzi ni kama kanuni za hesabu. Ikiwa huwezi kuzidisha kwa njia ya mkato, tumia ndefu. Mwisho jibu litakuja lile lile. Wewe si hodari wa romansi, basi hakikisha huchoki haraka ili ukimaliza kiwe kimeeleweka kwa pande zote mbili.
Ni kosa kubwa kushindwa kumuandaa vema mwenzi wako. Matokeo yake unakimbilia kupanda kwenye tuta wakati yeye hisia zake zipo mbali. Utachekwa, utaonekana hujui kazi.
Wanasema siku hazigandi, kwa hiyo baadaye mwenzi wako huyo anaweza kukutana na mtu mwingine ambaye ataonesha uhodari wa hali ya juu. Utajisikiaje utakapobaini kuwa shamba lililokushinda wewe, mwenzako mwenye jinsi kama yako ameliweza na linatoa mavuno?
Jitume kupigana na uvivu, onesha uwajibikaji wako, weka hai hisia zako. Kuna watu huonekana kero kwenye mapenzi kwa sababu ya kutaka kuonekana hawasikii chochote wawapo faragha.
Mwenzako anajituma nawe unaganda kama gogo, baadaye anaanza kujifikiria kuwa pengine hakuridhishi. Anatafuta mwingine, wewe pia unakaribisha mpenzi mpya lakini naye ataondoka kwa sababu huoneshi hisia za kimapenzi uwapo naye faragha.
Jitahidi kusoma kasoro zako na ujirekebishe. Unatakiwa uwe wa kwanza kugundua uchafu unaokukabili. Kama kuna maungo yako yanatoa harufu mbaya, basi yazingatie na jitahidi kuyaweka safi.
Pengine ni mtu mwenye hasira halafu mwenzi wako ana asili ya kupuuzia mambo. Hapa namaanisha kuwa endapo utashindwa kutambua kasoro yako ya kuwa na hasira za haraka, si ajabu ukawa unalala mzungu wa nne na mwenzako kila siku.
Dawa ya hiyo ni kuweka mbali hasira zako. Unapaswa kutambua kuwa uliyenaye ni binadamu, siyo malaika. Izoee tabia yake ya uzembe na inapobidi basi mweleweshe kwa sauti ya upole ambayo inaweza kupenya barabara masikioni mwake.
Ikiwa utaendelea na hulka ya kukasirika kila mara hata kwenye jambo dogo, utamfanya akuogope, hivyo mapenzi ya kweli kwako yataondoka. Hasara itakayokuja kwako ni kukukimbia au kutafuta mtu wa pembeni ambaye atampa tulizo la moyo analohitaji.
Una kasoro kwamba ukikaa baa unajisahau na kurudi nyumbani usiku wa manane. Hilo linapaswa kuwa tatizo la kuchukulia hatua. Kwa nini kila siku ugombane na mwenzi wako ambaye anakugombeza kwa tabia yako ya kuchelewa?
Mada hii iguse kila eneo ambalo unaona linakufunga. Siku zote unatakiwa uishi ukitambua kuwa watu wengi ambao tunaishi nao wanapoteza mvuto, wanaachwa kwa sababu hawajitambui.
Wanaishi kwa kurudia makosa yao ya siku zote. Kuwa mwelewa, kwa hiyo usirejee upungufu huo. Fumba macho, tafakari mapito yako na utambue pale ambapo haupo sawa.
Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine.
No comments:
Post a Comment