ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Valentino Mokiwa amesema anafanya kazi zake za kila siku huku akisubiri kukamatwa, lakini anajua hakufanya dhambi ya aina yoyote wala hakumfanyia mtu mabaya.
Amesema, alichokifanya ni kutimiza wajibu wake kama Askofu Mkuu kumsimika Askofu Stanley Hotay, lakini hahusiki na mgogoro wa Kanisa la Anglikana mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza na gazeti hili jana, Askofu Mokiwa alisema, amri ya kukamatwa kwake hajaipokea rasmi, bali aliisikia kupitia vyombo vya habari jana.
"Nikamatwe kwa kosa gani, sikumtendea mtu dhambi, sina kosa lolote lakini mwacheni Mungu aitwe Mungu na nuru ya kweli itajulikana, hivyo nasubiri amri ya mahakamani ili nikamatwe".
Naye Katibu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Mchungaji Dk. Dickson Chilongani, alisema si Askofu Mokiwa wala Kanisa hilo walioidharau Mahakama kwa kumwapisha Mchungaji Hotay kuwa Askofu.
Dk. Chilongani alifafanua kuwa Kanisa linaheshimu Mahakama na kuitii na kwa kufahamu umuhimu huo, Jumapili walisitisha hatua ya kumkabidhi kiti Askofu Hotay badala yake walimweka wakfu pekee.
Juzi, Jaji Kakusulo Sambo wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, alitoa hati ya kukamatwa Askofu Mokiwa, kwa kukiuka amri ya Mahakama iliyozuia kumwapisha Hotay kuwa Askofu wa Dayosisi ya Mount Kilimanjaro na pia iliagiza Hotay naye akamatwe, baada ya wakili wa upande wa mashitaka, Meinrad D’Souza, kuwasilisha maombi maalumu mahakamani hapo.
Hati hiyo ya kukamatwa ilitolewa siku moja baada ya Kanisa kumsimika Hotay mjini Arusha, kitendo kilichoelezwa na Mahakama kuwa ni kudharau amri ya mhimili huo, iliyotolewa Juni 10 kusitisha kuapishwa hadi pingamizi lililofunguliwa na waumini watatu wa Kanisa la Mtakatifu James, Arusha, litakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Pingamizi hilo linadai kuwa Katiba ya Kanisa hilo haikufuatwa katika kumchagua Hotay ambaye wanadai alikuwa na umri wa miaka 38 wakati umri anaopaswa mtu kuwa Askofu kwa mujibu wa Katiba ya Kanisa hilo ni kuanzia miaka 40.
“Hatujavunja amri ya Mahakama kwa kuwa hatukumweka uaskofu wa Dayosisi ya Mount Kilimanjaro, bali Askofu wa Kanisa Anglikana Tanzania, nimepokea simu nyingi za waumini wakitaka kuchukua hatua, lakini tumewatuliza, tunaamini haki itapatikana,” alisema Dk. Chilongani.
Alisema mawakili wao (Joseph Thadayo na Issa Mavura), walijaribu kuieleza Mahakama juzi kuwa kwa tamko la Mokiwa hawakuingilia mwenendo wa kesi hiyo, ili itupilie mbali hati hiyo ya kukamatwa Mokiwa na Hotay lakini bila mafanikio.
Akifafanua, Dk. Chilongani alisema utaratibu wa ibada ya kuwekwa wakfu Askofu una hatua mbili kuu, moja ni kumweka wakfu kuwa Askofu na pili ni kumtawaza (kumweka kitini) kwa kumkabidhi kiti cha uaskofu wa Dayosisi.
“Hatua ya pili ya kumpa Dayosisi haikufanyika, maana tulijua Mahakama imekataza, ingawa hata hati hiyo ya kukataza hatukuipata, kwa kuwa ilipelekwa Mount Kilimanjaro badala ya makao makuu ya Kanisa yaliyoko Dodoma wakati shauri hili linahusu maaskofu wote na si mmoja,” alisema Dk. Chilongani.
Katibu huyo alisema hata Mahakama haikupaswa kutoa hati ya kumkamata Mokiwa peke yake, kwa kuwa waliomweka wakfu Hotay, ni maaskofu 13 kwa niaba ya maaskofu 21 wa Anglikana nchini, hivyo wote wanapaswa kukamatwa.
Aliongeza kuwa ikiwa watamkamata, watatii na baadaye watafuatilia dhamana, lakini alidai kuwa hatua ya kuwakamata maaskofu hao inaweza kusababisha maandamano ya waumini wa Anglikana nchini, ambao tayari wanamsumbua kwa simu kutaka kujua msimamo wa Kanisa.
“Siingilii Mahakama, ila masuala haya ya kiimani yanapaswa kutazamwa kwa uangalifu, uchaguzi ulifanyika Aprili 11 na wagombea wote watatu akiwamo Hotay walikubali matokeo na kushikana mikono. “Lakini maandalizi yalikuwa yamefanyika na wageni wengine wametoka Ulaya, siku mbili kabla ya kuapishwa, wanatokea watu kuweka pingamizi, ngoja tuisubiri Mahakama,” alisema Dk. Chilongani.
Alisema endapo Mahakama itaamua vizuri, watafanya ibada maalumu ya kumweka kitini (kumtawaza) Hotay kuwa Askofu wa Mount Kilimanjaro lakini ikiamuliwa vinginevyo, Kanisa litamtafutia kazi ya kufanya.
Kwa mujibu wa Dk Chilongani, utaratibu wote wa kumteua Hotay kugombea uaskofu ulipitishwa na Halmashauri Kuu ya Kanisa hilo nchini baada ya kuridhika kuwa ana sifa, huku cheti cha kuzaliwa na hati ya kusafiria ya karibuni, vikionesha alizaliwa mwaka 1969 na si 1972. Waumini waliofungua shauri hilo ni Godfrey Mhone, mume wa mwimbaji wa Injili nchini, Beatrice Mhone, Lothi Oilevo na Frank Jacob.
CHANZO:HABARI LEO
No comments:
Post a Comment