ANGALIA LIVE NEWS

Friday, July 29, 2011

Majambazi yaua polisi kwa risasi

Askari wa upelelezi Wilaya ya Serengeti mkoani Mara namba F,4236 PC, Pendo Jovin Miaka 35 ameuawa kwa kupigwa risasi shingoni na majambazi katika Kijiji cha Genkuru wilayani Tarime wakati wakiendesha msako wa kuwasaka majambazi wanaotuhumiwa kukuhusika katika matukio ya ujambazi wa kutumia silaha za moto.
Askari huyo alikuwa katika msako huo akishirikiana na askari wenzake kutoka Wilaya ya Tarime.
Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Kipolisi ya Tarime/ Rorya, Joackim Massega, alisema: “Tukio hilo la kuuawa kwa askari wetu limetokea saa tisa usiku katika kijiji cha Genkuru Kata ya Goron'ga tarafa ya Ingwe, ambapo tulipata taarifa ya kuwepo kwa majambazi wenye silaha za moto (bunduki) kutoka Kenya wakijiandaa kufanya uhalifu katika maeneo ya vijiji vya Nyamongo, Nyamwaga na Genkuru .” Massega alisema kuwa askari Pendo alifika Tarime kutoka Mugumu Wilaya ya Serengeti kuungana na askari wenzetu katika msako na kwamba kabla mauti haijamkuta marehemu, polisi walimkamata tuhumiwa mmoja.

“Alikuwa akituongoza kwenda kwa majambazi wenzake waliokuwa na silaha na tulipofika huko ndipo majambazi hao walianza kufyatua risasi na ikampata mwenzetu PC, Pendo Shingoni na kumsababishia Kifo,” alisema Massenga.
Alisema kuwa jambazi aliyefyatua risasi na kumuua marehemu alifanikiwa kutoroka na inadaiwa ni raia wa Kenya. Mtuhumiwa mwenzake anayeshikiliwa na polisi jina lake linahifadhiwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa kuwabaini wahusika katika mtandao huo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: