
Didas Masaburi
Meneja wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda), Victor Milanzi, aliyesimamishwa kazi kwa tuhuma za ubadhirifu , amekanusha kuhusika na ubadhilifu wa Sh.millioni 200 zilizopotea na badala yake amemtaka Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Didas Masaburi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam jana, alisema Masaburi anaficha ukweli kwa sababu anashirikiana na mmiliki wa Kampuni ya Simon Group Robert Kisena kumchafua ili malengo yao yatimie.
“Meya Masaburi akishirikiana na wamiliki wa Simion Group ambao ni vigogo mbalimbali akiwemo Waziri wa muda mrefu wameapa kuichukua Uda kwa nguvu ili waigeuze Container Terminal ili kukidhi matakwa yao binafsi,” alisema Milanzi.
Milanzi alisema Meya Masaburi aliitisha kikao Juni 10 mwaka huu na kubariki maamuzi ya bodi ya Uda kwa kufanya kikao na mmiliki wa kampuni ya Simon Group huku akijua kuwa bodi ilikosea kwa kuwa ilikuwa haikuwahusisha wanahisa wakubwa.
Aidha, Milanzi alisema Meya katika kikao hicho alipitisha maamuzi hayo akijifanya yeye ni Mwenyekiti na Robert Kisena mmiliki wa Simion Group kuwa katibu na kufanya maamuzi batili bila ridhaa ya baraza la madiwani na wanahisa wakubwa.
Hata hivyo, uchafu huo ulikamilika pale alipomkabidhi kampuni ya Uda siku hiyo hiyo Simion Kisena kwa vile alilipa milioni 285 sawa na asilimia 12.5 ya hisa zote za Uda na kumtangaza mbele ya wafanyakazi.
Alidai kuwa mmiliki wa kampuni hiyo Juni 22, saa 2:00 ya usiku alivunja ofisi za umma za Meneja Mkuu wa Uda na kuiba nyaraka muhimu zikiwemo hati miliki ya majengo na kuitaka serikali isikae kimya wakiangalia mali za Uda zikiporwa kwani wao ndio mmiliki.
Awali Meya alitangaza kuunda tume mbili kwa ajili ya kuchunguza fedha zilizopotea Uda na mkataba uliopo pia kuchunguza matatizo yanayopatikana katika kituo cha Ubungo na kwamba zitagharimu milioni tisa hadi watakapo maliza uchunguzi.
Meya alisema Sh. milioni 200 zilikuwa zimepotea na hazikuonyesha matumizi yake yoyote na ameipa tume mwezi mmoja ili kuweza kujua ukweli wa jambo hilo.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment