ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, July 30, 2011

Uhuru wenye mipaka katika mapenzi hujenga uhusiano imara-2

Na Luqman Maloto
Wengi wanaachana kwa sababu ya kutozingatia uhuru na mipaka yao. Hawajui wajibu na uhuru wa wenzi wao.
Hilo litatambulika na kuzingatiwa kama kila mmoja atapokea matukio kwa jinsi inavyotakiwa.
Hii ndiyo mantiki ya wiki iliyopita kukutaka uwe na akili hai. Itashangaza umepata habari kwamba mwenzi wako yupo gesti na mpenzi mwingine halafu unatabasamu.


Sumu hatari inayosababisha mmomonyoko wa ndoa au uhusiano wa kimapenzi kwa watu wengi ni kushindwa kujipanga kimaeneo. Ratiba za ofisini kuingiza nyumbani. Marafiki kuathiri taratibu za mapenzi yenu, ingawa kila kitu kina umuhimu wake kulingana na wakati husika.

Umeudhiwa na wafanyakazi wenzako kazini, unatakiwa kuweka hekima mbele. Unarudi nyumbani ukiwa na imani kwamba huko utakutana na mwenzi wako na ndiye mfariji wako. Kichwa kizito, basi mueleze mwenzio ajue kinachokusibu kuliko kumpa majibu ya mkato. Itakuharibia badala ya kukusaidia

Ninachosisitiza hapa ni kuwa uhusiano wa aina yoyote unadumishwa na mawasiliano.

 Lugha yako mbele ya mwenzi wako ina nafasi kubwa ya kukufanya uendelee kufurahia penzi lake. Kinyume chake unaweza kujikuta ni kero kwake. Atakuvumilia mwisho atachoka kwa sababu hujui kubembeleza, unapenda kuamrisha.

Ni suala la kudhibiti uhuru wako. Fahamu kuwa una kikomo chako ambacho kinaruhusu mwenzi wako awe huru. Ukitambua hayo, utaweza kujua wajibu wako ambao ukiutekeleza, utaufanya uhusiano wako uwe imara kweli kweli. 

Nilishasema kuwa kabla ya kuingia kwenye uhusiano wa kimapenzi ni lazima uwe umejiandaa kupenda, kuheshimu, kulinda, kunyenyekea na kadhalika. Kama hujajiweka tayari kwa vitu hivyo, usithubutu kumcheza shere mwenzako. Mapenzi yanabeba uhai wa mtu, hayajakufika tulia au uliza usimuliwe.

Inatokea mara nyingi mtu anapoteza mvuto wake wa kimapenzi kwa sababu ya kushindwa kuchagua maneno ya kuzungumza na mwenzi wake. Maongezi ya wawili, wewe unapayuka mpaka majirani wanasikia. Kama ni nyumba za kupanga, unakuwa kituko na kutolewa mifano kila wapangaji wenzako wanapopiga soga.

Haikubaliki hata kidogo! Unapaswa kujifunza lugha laini, ufanye mazoezi na uzoee ikiwa unataka kuboresha mvuto wako wa kimapenzi. Usichopenda kuambiwa, usimtamkie mwenzako kwa maana maumivu unayoweza kuyapata pengine yeye ni zaidi. Tengeneza mzani wa maneno.

Maneno ni sumu, wengi wamejikuta wakisalitiwa kwa sababu ya kushindwa kuelewana lugha na wenzi wao ndani ya nyumba. Kisaikolojia, inapotokea mvurugano wa mara kwa mara kati ya wawili wanaopendana, anayejiona anatendwa huanza kutafuta tiba.

Inatoa fundisho kwamba mtu anapoudhiwa na mwenzake na hali hiyo kudumu kwa muda mrefu, anapokutana barabarani na mtu wa jinsi nyingine ambaye atamsabahi kwa utulivu, ghafla mawazo yake husafiri na kumfikia mwenzi wake nyumbani. Atamlinganisha halafu atamshusha thamani.

Mathalan, mwanamke amekutana na mwanaume mcheshi, akamsalimia kwa upole. Kwa kuotea, akamuona mnyonge, hivyo akamuuliza: “Anti una matatizo gani? Naweza kukusaidia?” Kauli hizo za jamaa wa barabarani zitamsababisha amuone mume au mpenzi wake ni wa kiwango cha chini kimapenzi. 
Itaendelea wiki ijayo.

Chanzo:www.globalpublishers.info

No comments: