Mbunge wa Kilindi, (CCM), Beatrice Shellukindo, ambaye hivi karibu aliibua kashfa iliyomsimamisha kazi Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, David Jairo, amekosoa serikali kwa kumtelekeza Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi.
Alisema ‘udhalilishaji’ huo ulitokea wakati wa maadhimisho ya miaka 10 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) yaliyofanyika mjini Arusha Juni mwaka huu.
Shellukindo aliyasema hayo jana wakati akizungumza kwenye semina ya wabunge kuhusu masuala ya mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) mjini Dodoma.
Shellukindo ndiye alilipua bungeni kashfa ya taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati na Madini kutakiwa kuchanga Sh. milioni 50 kufanikisha kupitishwa kwa bajeti ya wizara hiyo. Wiki iliyopita pia alimtuhumu Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo kwa kupalilia ukabila katika idara ya Wanyamapori ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Katika semina ya jana iliwashirikisha mawaziri, manaibu mawaziri, wabunge na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Spika wa Bunge, Anne Makinda na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta. Shellukindo alisema pamoja na kuwa Serikali inahimiza ushirikiano katika Jumuiya hiyo, ni aibu kwa jumuiya kushindwa kutimiza wajibu wake wakati wa maadhimisho hayo yaliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa jumuiya hiyo.
“Serikali inasisitiza ushirikiano wa Afrika Mashariki, lakini wizara yenyewe haionyeshi kujali ushirikiano huu. Hivi karibuni yalifanyika maadhimisho ya miaka 10 ya Jumuiya na maadhimisho yenyewe yalifanyika Arusha,“ alisema na kuongeza:
“Katika maadhimisho hayo, marais ambao ndiyo waliokuwapo wakati jumuiya hiyo inaanzishwa walialikwa, kwetu alialikwa Mzee Mwinyi, Kenya alialikwa Moi na Uganda alikuwa amealikwa Museveni. Museven hakuja bali alituma mwakilishi wake, Moi alikuja mwenyewe na hapa kwetu alihudhuria Mzee Mwinyi.”
Alisema: “Wakati tukiwa pale Mount Meru Hoteli, Moi akatua na helkopta, chwaaaaaa na kupelekwa katika hoteli ambapo alikodishiwa floor nzima. Sisi Mwinyi alikuja na ndege, lakini jambo la ajabu ni kwamba, maandalizi ya Mwinyi hayakuwa mazuri kwa sababu hata fedha hazikuwapo na Mama Kate Kamba ni shahidi hapa.”
Kate Kamba ni mbunge wa Afrika Mashariki.
Alisema baada ya hali hiyo kuonekana, ikabidi wabunge wa Tanzania walioko katika jumuiya hiyo wachangishane fedha ili kukabiliana na gharama zilizokuwa zikihitajika kwa sababu utaratibu ulikuwa ni kila nchi kumgharamia rais wao aliyealikwa.
“Sasa haya mambo gani haya, tunataka jumuiya wakati sisi wenyewe hatuko tayari kuunga mkono, hii ni aibu kwa sababu Mzee Mwinyi ilimbidi kukaa katika chumba chake na kuagiza chakula ndani huku waalikwa wengine wakiwa katika hafla iliyoandaliwa mahali hapo,” alisema.
Akizungumza baadaye nje ya ukumbi wa Msekwa na waandishi wa habari kutoa ufafanuzi wa tukio hilo, Shellukindo alisema kuwa aliyekuwa Katibu wa wabunge wa Tanzania ni mtoto wa Mzee Mwinyi, Abdallah Mwinyi.
“Hili tukio lilimkera hata Mtoto wa Mwinyi kwa sababu baada ya kuona Wizara yetu ya Afrika Mashariki hatukuandaa chochote, ilibidi aje atwambie nasi tukashangaa sana mambo yalivyokuwa yameandaliwa,” alisema.
NAIBU WAZIRI AMKANA
Hata hivyo, Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Abdallah Juma Sadala, alikanusha madai ya ya Shellukindo na kusema siku hiyo kila kitu kilikuwa kimepangwa vizuri.
“Siku hiyo anayosema Mheshimiwa Mbunge mimi nilikuwapo, walikuwapo wabunge wa CCM na wale wa Upinzani. Kwa kweli protocol (itifaki) ilithibitishwa na mimi ndiye niliyeithibitisha. Ulinzi ulikuwapo wa kutosha na pia Mzee Mwinyi aliingia na magari yapatayo 10 au 15 hivi,” alisema.
Akifunga semina hiyo, Waziri Mkuu Pinda aliwataka viongozi wenzake wa serikali kukubali hoja zilizotolewa na wabunge na kwamba hakubaliani na dhana ya serikali kupenda kujitetea.
Alisema ni vyema Tanzania ikajipanga kutumia fursa zilizopo ikiwemo Bandari ya Dar es Salaam ili kuongeza mapato ya nchi. Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck Ole Medeye, alisema anakerwa na tabia ya nchi jirani ya kutangaza kuwa madini ya tanzanite ni ya kwao wakati sio kweli.
Alisema kwa bahati mbaya hajaona kifungu katika mkataba wa EAC ambacho kinakataza nchi kutangaza mali ni ya kwao kumbe si kweli.
Alitaka kuwepo kifungu cha sheria kinachokataza nchi ndani ya jumuiya hiyo kutangaza kwamba mali fulani ni yao wakati siyo ya kweli.
Mbunge wa Ngara (CCM), Deogratius Ntukamazina, alieleza wasiwasi wake kuhusiana na suala la lugha katika jumuiya akisema kuwa Tanzania ikubali ama isikubali, lakini inalazimika kuimarisha lugha ya Kiingereza kwa kuwa ni lugha ya kibiashara.
Alisema aliwahi kushiriki katika mahojiano ya kazi katika EAC, lakini Watanzania wengi walishindwa kutokana na kutomudu vizuri lugha ya Kiingereza.
Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Leticia Nyerere, alisema mfumo wa elimu wa Tanzania sio mzuri kwa sababu mtoto anafundishwa kukariri badala ya uwezo wa kufikiri na kuchanganua mambo.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment