ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, August 31, 2011

Igunga: Mkapa apata kombora la kwanza


Aambiwa ni mchafu asiyestahili kusimama jukwaani
  Kafumu naye apigwa kombora lake, ajibu mapigo
Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa
Wakati Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimemteua Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, kwenda Igunga kuzindua kampeni za chama hicho za uchaguzi mdogo wa ubunge wa jimbo hilo unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2, mwaka huu, Chama Cha Wananchi (CUF) kimesema kiongozi huyo mstaafu amezingirwa na kashfa nyingi hivyo si mtu sahihi kusimama jukwaani katika kampeni hizo.
Akizungumza jana kutoka Igunga, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara, Julius Mtatiro, alisema Mkapa ni kati ya marais walionufaika na sekta ya madini, inayosimamiwa na mgombea wa CCM katika kinyang’anyiro hicho, Dk. Peter Kafumu, ambaye pia ni Kamishna wa Madini nchini.
Mtatiro alisema tambo za CCM katika kinyang’anyiro hicho, zinaonyesha namna ambavyo kisivyokuwa makini kwa kuwa Mkapa kama kada wa CCM, alijimilikisha kinyemela mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira kwa bei ya kutupa.

Mkapa anadaiwa kuuchukua mgodi huo kwa kulipa Sh. milioni 70, badala ya Sh. milioni 700 alizotakiwa kulipa.
Hata hivyo, taarifa zaidi zinaeleza kwamba wakati Mkapa akijimilikisha kwa bei chee, mgodi huo ulikuwa na thamani ya zaidi ya Sh. bilioni nne. Mkapa anadaiwa kujimilikisha mgodi huo kupitia kampuni ya ANBEN kwa kushirikiana na aliyekuwa waziri wake wa Nishati na Madini, Daniel Yona. Hata hivyo, Julai mwaka 2009, Serikali ilitangaza kuuchukua mgodi wa Kiwira na kwamba ingeanza mchakato wa kupata utaratibu wa kuuendesha mradi huo kama ilivyokusudiwa, ikiwamo kuingia mkataba wa uendeshaji na kampuni itakayopewa mamlaka ya kujenga na kuundesha.
Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, alitangaza uamuzi huo bungeni, huku akieleza kuwa chini ya mkataba wa uendeshaji, mkandarasi atapewa jukumu la kujenga uwezo wa mashirika ya Shirika la Madini la Taifa (Stamico) na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), ili yamiliki na kusimamia mradi.
Serikali ilitangaza pia kuanza mazungumzo na Serikali ya China iliyoanzisha na kuendesha mradi huo, ili kupata mkopo wa kufufua mradi huo na kuhakikisha uzalishaji wa umeme wa megawati 200 ungeanza mapema, lakini hakuna uwekezaji uliofanyika hadi sasa.
Hata hivyo, serikali haikukanusha wala kugusia tuhuma zinazomwandama Mkapa kwamba alikuwa mmiliki wa mgodi huo.
Badala yake, ilielezwa kwamba baada ya kampuni ya TanPower Resources (TPR), kuendesha mgodi wa Kiwira chini ya jina la KCPL, mwanahisa mmoja kati ya watano ambaye ni ANBEN Limited yenye hisa 200,000 alijitoa.
ANBEN ilidaiwa kumilikiwa na Mkapa na mkewe ambayo nayo ilishatangazwa kufilisiwa.
Wanahisa wengine waliokuwa na hisa TPR ni DevConsult International Limited, Universal Technologies Limited, Choice Industries Ltd na Fosnik Enterprises Ltd.
Ujenzi wa mgodi wa Kiwira ulifanyika kati ya mwaka 1983 na 1988 kwa gharama ya Sh bilioni 4.29 kwa ushirikiano wa Tanzania na China na Oktoba 1988 iliundwa kampuni ya KCML, ikiwa ni kampuni tanzu ya Stamico kwa ajili ya kuendesha mgodi huo.
Makaa ya mawe yalitumika kuzalisha umeme kwa mgodi wenyewe na kuuzwa kwa kiwanda cha saruji cha Mbeya na cha karatasi cha SPM Mgololo huku ziada ya umeme ikiuzwa Tanesco.
“Mkapa ni kati ya marais waliotumia sekta ya madini kujinufaisha yeye mwenyewe kama rais wa nchi na kujijengea utajiri kupitia madini ya Watanzania,” alisema Mtatiro.
Mtatiro alifafanua kwamba: “Leo Mkapa analetwa kumnadi Dk. Kafumu ambaye ni mmoja wa watu wanatumika kuua sekta ya madini na kuwafanya Watanzania wawe maskini wa kudumu ndani ya nchi yenye rasilimali hizi nyingi.”
Alimshambulia Dk. Kafumu kwamba ameshindwa kuisimamia vyema sekta hiyo kwa manufaa ya Watanzania na badala yake, imeendelea kuwanufaisha wageni.
“Mkapa si msafi kama alivyo Kafumu, wote wametumika kuua uchumi wa nchi hawawezi kuwadanganya watu wa Igunga,” alisema Mtatiro.
Alisema hata mishahara ya baadhi ya wafanyakazi wa Kitanzania wanaofanyakazi migodini ni midogo ikilinganishwa na ile ya wageni wanaolipwa kwa Dola ya Marekani, jambo ambalo kama Kamishna wa Madini ameshindwa kulisimamia.
Tangu alipozushiwa tuhuma hizo na Mbunge wa zamani wa Vunjo (CCM), Aloyce Kimaro, Mkapa aliamua kukaa kimya hadi leo.
DK. KAFUMU AMJIBU MTATIRO
Dk. Kafumu alipoulizwa na NIPASHE kuhusiana na tuhuma zilizotolewa na Mtatiro dhidi yake, alisema hazina msingi wowote kwa kuwa majukumu ya Kamishna wa Madini, ni kusimamia sheria zinazoongoza sekta hiyo, sera, kutoa leseni, biashara ya madini na kumshauri waziri.
“Unapozungumzia ajira hilo ni suala ambalo lipo nje yangu kabisa, wala mikataba mimi hainihusu, mimi nasimamia sheria kuhakikisha zinafuatwa na wale wanaowekeza kwenye madini, labda Kamishna wa Madini anaweza kuingia kwenye tuhuma hizo kama sheria za nchi zitabadilishwa na kumwongezea majukumu,” alisema Dk. Kafumu.
Alisema kuna tuhuma zimeandaliwa dhidi yake na kwamba ni mambo anayoyategemea hasa kutoka kwa wapinzani wake wa kisiasa, lakini akatahadharisha kwamba waelewe kwanza majukumu ya kazi yake.
Uchaguzi wa Igunga unafanyika kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Rostam Aziz, aliyejiuzulu wadhifa huo pamoja na ujumbe wa Halmashauri Kuu ya taifa (NEC) ya CCM kupitia Mkoa wa Tabora Julai 13, mwaka huu, kwa kile alichoeleza kwamba ni kuchoshwa na siasa uchwara, fitina na kuandamwa ndani ya chama hicho.
Kampeni za uchaguzi huo zinatarajiwa kuanza Septemba 7, mwaka huu baada ya kufungwa kwa zoezi la kuchukua fomu za kugombea litakalositishwa Septemba 6.
Kamati Kuu ya (CC) ya CCM ilikutana jijini Dar es Salaam juzi chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, na kumteua rasmi Dk. Kafumu kugombea kiti hicho na pia kumkabidhi Mkapa jukumu la kuzindua kampeni za CCM za kumnadi mgombea huyo.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa NEC ya CCM, Nape Nnauye, alisema kuwa CCM ilimpa Mkapa heshima hiyo kama Mwenyekiti Mstaafu wa chama hicho.
CHANZO: NIPASHE

No comments: