Wednesday, August 31, 2011

Ili uwe bora, tafuta kuwa bora kwanza! -2



WEWE ni sehemu ya All About Love, ukiacha kusoma hapa maana yake itakuwa haipo tena. Nimefurahi sana, maana umeendelea kuwa mdau wa ukurasa huu kila siku, safu ambayo kila kukicha inakuongezea kitu muhimu katika maisha yako ya kimapenzi.

Naam! Hata kama ulikuwa na ugomvi wa mara kwa mara na mwenzi wako, kolamu hii inakuongezea ujanja na unakuwa bora kwa mpenzi wako. Kama ni mara ya kwanza kuanza kusoma hapa, hutajuta na ninakukabirisha kwa moyo mkunjufu. Hii ni klabu ya wapendanao, ambao wana werevu wa masuala ya uhusiano na wanakubali kujifunza.

Ngoja nikuambie rafiki yangu, siri ya kuwa bora siku zote ni kujifunza. Karibu sana tujifunze pamoja. Mada ni kama inavyosomeka hapo, tulianza nayo wiki iliyopita, leo tunafikia tamati.

Nazungumzia juu ya mwenzi bora katika maisha ya mapenzi. Baadhi ya watu huwa wanalalamikia wenzi wao kuwa bora, lakini wanasahau jambo moja muhimu; ubora wa mwenzako ni matokeo ya wewe kuwa bora.


Wiki iliyopita nilielezea vipengele vya mwanzo, sasa twende tukamalizie mada yetu. Upo tayari? Bila shaka unajisemea moyoni ndiyo...kazi kwako!

UNAONEKANAJE?
Mwonekano wako unaweza kukuanisha jinsi ulivyo kwa wanaokutazama. Wakati mwingine inawezekana ukatafsirika tofauti na ulivyo kutokana na jinsi unavyovaa na tabia zako nyingine.

Lazima uwe kijana wa kisasa, kwa kuzingatia hilo unapaswa kuwa makini kwa kila kitu kinachoonekana kwa wanaokutazama. Jenga mazoea ya kutambua aina ya nguo na mahali ulipo, usivae nguo za ufukweni ofisini au nguo za mtaani ukavaa ofisini.

Wanaokuangalia wanapata taswira ya jinsi ulivyo kutokana na mavazi yako. Vaa nguo safi kila wakati, labda kama unafanya kazi ambayo inakulazimisha kuwa mchafu, ila baada ya hapo unapaswa kuwa msafi.

Kama huna mpenzi hii ni nafasi nzuri kwako, huenda uliumizwa na mpenzi wako aliyetangulia/waliotangulia, jiweke katika mwonekano mzuri utakaowavutia wengine, huenda ukapata atakayekupenda.

Jiangalie vizuri ulikosea wapi katika uhusiano wako uliotangulia, huenda mwonekano wako ulimchukiza mpenzi wako bila wewe kufahamu hilo. Vaa nguo za heshima kila wakati ili uonekane unajitambua na mwenye kujiheshimu. Rafiki yangu, mavazi nayo yanazungumza!

Kama tayari una mpenzi, unapaswa kutumia nafasi hiyo vizuri sana, utakapovaa kisasa, nguo safi za kupendeza, hata utakapotembea na mpenzi wako, atajisikia huru kuwa na wewe na atajiona yupo na mpenzi makini unayemvutia yeye na wengine wanaokutazama.

UCHAGUZI WA MANUKATO
Unapozungumzia suala la mavazi, unatakiwa pia kuwa mwangalifu katika uchaguzi wa manukato. Lazima uwe mwangalifu kuchagua ‘perfume’ nzuri ambayo haitasumbua pua za mpenzi wako.

Kunukia vizuri a kutakufanya uwe rafiki wa kila mtu. Achana na manukato yenye harufu kali. Utakuta mtu anaingia kwenye daladala kila mtu anageuka na kumwangalia. Hapo kuna mawili, ama ananukia vizuri au ananukia vibaya, sasa lazima ujitahidi usiwe kero kwa wenzako.

ULIMI WAKO
Inakupasa upime kila unachoongea mbele za watu, usiwe na tabia ya kuzungumza bila mpangilio. Kama unadhani jambo linalozungumzwa huna uhakika nalo, siyo vibaya kama utakaa kimya bila kuchangia chochote.

Kukaa kwako kimya hakutakufanya ukaonekana mshamba, badala yake utaonekana makini mwenye kupima kila kinachotoka kinywani mwako. Kimya hakimaanishi kushindwa, bali kunaonesha uungwana na nia ya kujifunza. 

CHANGAMKA
Kama unataka mwenzi wako awe bora, unatakiwa pia uwe mchangamfu. Uchangamfu ambao unaambatana na vituko. Najua hapo nitakuwa nimekuchaganya kidogo, vituko ninavyozungumzia hapa ni vile vya kimahaba.

Ili mpenzi wako akuone bora na asikuchoke, inabidi usiishe kuwa mtu wa vituko. Unapaswa kumtumia sms za mapenzi kila mara, ukimtania au kumsifia kwa mambo fulani ya vituko au kuchekesha. Mfanye achangamke na awe na hamu ya kusoma sms zako kila wakati.

Kimsingi nilicholenga hapo ni jinsi gani unavyoweza kujisogeza karibu na mpenzi wako kila wakati na akakuona unavyomjali na kumfanya mwenye furaha wakati wote. Vituko vyako vitamfanya aone umuhimu wako na kutamani kuwa na wewe kila wakati, hapo naye atakuwa kama wewe. Twende tukamalizie kipengele cha mwisho.

MFANYE MWENYE FURAHA
Mfanyie mambo yanayomfurahisha kila wakati. Katika mambo yatakayomfanya awe na furaha, zingatia kiasi. Hata hivyo, mahali pazuri pa kumfurahisha zaidi mpenzi wako ni kitandani.

Ni wajibu wako kuhakikisha unamfurahisha ipasavyo faragha. Kwa wanandoa, tendo la ndoa ni msingi wa ndoa yenyewe!
Hakikisha unapokuwa faragha na mwandani wako unatumia mbinu mpya na ubunifu wa hali ya juu unaobadilika kila siku ili azidi kuona mabadiliko yako.

R afiki zangu, sina shaka kuna kitu mmejifunza kupitia mada hii. Mpaka hapa, naomba niweke kituo kikubwa. Wiki ijayo nitakuja na mada nyingine nzuri zaidi ya hii, SI YA KUKOSA!

Joseph Shaluwa ni mshauri wa mambo ya mapenzi anayeandikia magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love na Lets Talk About Love vilivyopo mitaani. Kwa makala zaidi tembelea www.globalpublisherstz.com

No comments: