ANGALIA LIVE NEWS

Friday, August 12, 2011

Kanuni zatumika kumzuia Mnyika asimbane Pinda


Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, amesema kuwa imekuwa kawaida kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kutoa majibu ya upotoshaji katika kipindi cha maswali  ya papo kwa papo bungeni.
Mnyika aliyasema hayo bungeni jana, wakati akiomba mwongozo kwa Spika kwa kutumia kanuni  namba 68 (7) na 133 mara baada ya kipindi cha matangazo.
“Kanuni 133 (1) mbunge yoyote anaweza kutoa taarifa ya maandishi hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, kwa mujibu wa kanuni ya ya 53A, kumekuwa na kawaida katika kipindi cha maswali na majibu  kwa Waziri Mkuu kwa Waziri Mkuu kutoa majibu yenye upotoshaji,” alisema.
Mnyika hakuweza kuendelea kwani Naibu Spika, Job Ndugai, alisema kanuni hiyo inamtaka mbunge kupeleka bungeni taarifa ya maandishi. “Kama ndivyo, unatakiwa kuleta taarifa ya maandishi huwezi kutumia fursa hiyo hiyo badala ya kuleta maandishi ukasema humu humu ndani, usitikise kichwa.”
 Ndugai alimtaka kutumia kanuni ya 68 (7) na kumtaka Mnyika aisome  tena kanuni ya 133 kama ndiyo anayotaka kuitumia.
 Hata hivyo, Mnyika aliposimama alimuomba Ndugai kumsikiliza kwanza na kisha akainukuu tena kanuni ya 133 (A), “Mbunge yeyote anaweza kutoa taarifa ya maandishi kwa Spika ya kutaka kuleta hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu kwa mujibu wa Ibara ya 53A ya Katiba.”
 Hata hivyo, Ndugai alimtaka Mnyika kukaa chini. “Kila mwenye kanuni yake aisome tena kanuni hiyo,” alisema Ndugai.
 “Nawaomba Mheshimiwa Mnyika na wabunge wengine tuheshimiane, ni vizuri kuzitumia kanuni kwa kadri zinavyotakiwa zitumike,” alisema na kisha kuisoma mwenyewe.
 Baadaye Ndugai alisema kuwa kutokuwa na imani kwa Waziri Mkuu, haimaanishi kuwa kutokuwa na imani kwa Mizengo Pinda. “Kutokuwa na imani kwa Waziri Mkuu inamaanisha Bunge hili likiunga mkono halina imani kwa serikali nzima tafsri yake kwamba likipita lazima serikali hii ivunjwe, Rais atumie utaratibu wake wa kikatiba kama kuita uchaguzi mwingine au kuteua serikali mpya,” alisema Naibu Spika na kuongeza:
 “Lakini langu mimi hapa ni la utaratibu tu, yanayofuata ni suala lingine kwa hiyo si suala dogo la kulibeba na kunyanyuka kila mtu anapotaka kama tunavyofikiri, lakini unaweza kutokuwa na imani kwa Waziri Mkuu, Naibu Spika au Spika lipo kwenye kanuni hizi hizi, kutokuwa na imani na Rais wa nchi lakini ukitaka kutumia jambo hili lazima uwe umejiandaa,  unapokuwa hauna imani na waziri mkuu in amaana utatoa taarifa ya maandishi na kuleta katika ofisi na kwa hakika tutaipokea.”
 Alisema taarifa hiyo iwekwe sahihi na kuungwa mkono na wabunge wasiopungua asilimia 20 ya wabunge wote na kwamba ili kukidhi masharti ya kanuni hiyo ni lazima kuwe na wabunge  wasiopungua 72.
 Alisema utaratibu unaofuata ni kuingizwa kwa hoja hiyo ndani ya Bunge ambapo itajadiliwa na kisha wabunge watapiga kura za siri na kwamba maamuzi yake yatakuwa ya mwisho.
CHANZO: NIPASHE

No comments: