ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, August 20, 2011

Kenya wapata wawakilishi kambi ya Man U Tanzania



Yosso wanne wa soka wameteuliwa kuiwakilisha Kenya katika kambi ya vijana ya klabu ya Manchester United ya England itakayoanza nchini Oktoba na kushirikisha chipukizi wenye vipaji kutoka katika nchi za Afrika.
Naim Ashraf kutoka Shule ya Sekondari Nairobi Milimani, Mzee Ali Rama (Tononoka High School), Naomi Njeri (Matuu Memorial) na Emily Auma kutoka Jera Girls, ndio waliopata fursa ya kuhudhuria kambi hiyo ya Man U itakayofanyika nchini Tanzania.
Yosso hao wa Kenya walipatikana baada ya kuonyesha kiwango cha juu katika mashindano ya Shule za Sekondari za Kenya iliyofahamika kama “The Airtel Rising Stars” na kufanyika katika viwanja vya Moi Forces Academy jijini Nairobi.

Kambi itakayofanyika Oktoba nchini Tanzania itaandaliwa kwa ushirikiano kati ya kampuni ya simu za mkononi ya Airtel na klabu ya Manchester United, mabingwa mara 19 wa Ligi Kuu ya England, ili kuwaibua na kuwalea yosso wenye vipaji vya soka wa Afrika Mashariki.
“Kwangu mimi, hii ni ndoto iliyogeuka kuwa ya kweli. Nimekuwa shabiki mkubwa wa Manchester United na baada ya kuchaguliwa na kocha “Ghost” (Jacob Mulee) nilifurahi kujua kwamba nitapata nafasi ya kujifunza soka katika klabu bora kabisa duniani,” alisema Rama.
Jopo la makocha wanne, wakiongozwa na kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’, Jacob “Ghost” Mulee lilisema kuwa timu zote 16 zilionyesha vijana wenye vipaji katika fainali hizo.
“Mashindano yalikuwa makali. Tunaamini kwamba wachezaji hawa wanne watakuwa mabalozi wazuri wa soka la Kenya kwenye kambi hiyo,” alisema Mulee.
Makocha wengine walioshiriki mchakato huo walikuwa ni Twahir Muhiddin, mwanasoka wa zamani wa kimataifa Micky Weche na nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya vijana wa Kenya ‘Harambee Starlets’, Florence Adhiambo.
Wachezaji Ryan Giggs, Paul Scholes, David Beckham, Gary Neville, Phil Neville na Nicky Butt ni miongoni mwa nyota wa soka waliotokana na shule ya kukuzia vipaji ya Manchesetr United.
CHANZO: NIPASHE

No comments: