TFF yaomba mechi Stars, Algeria ichezwe Taifa
Simba yateua Tanga, Yanga kutumia Morogoro
Simba yateua Tanga, Yanga kutumia Morogoro
Afisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu alisema kuwa klabu yao imeamua kuutumia Uwanja wa Jamhuri, Morogoro kwa ajili ya mechi zao za nyumbani wakati habari za ndani zimesema klabu ya Simba imeteua Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga kuwa wa nyumbani.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) nalo, jana liliiandikia barua Serikali kuomba wautumie uwanja wa Taifa kwa ajili ya mechi ya Taifa Stars ya kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika. dhidi ya Algeria Septemba 3.
Juzi, Serikali ilitangaza kuufunga uwanja huo kwa ajili ya matengenezo hatua iliyopelekea TFF kuchanganyikiwa na kutangaza kuwa mechi ya Stars itachezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, kabla ya jana kubadilika na kuomba vinginevyo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Afisa Habari wa TFF Boniface Wambura alisema kuwa TFF imeamua
kuiomba Serikali kuutumia Uwanja wa Taifa kwa mechi ya Stars kwakuwa tayari walishatoa taarifa kwa Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) kuwa mechi hiyo itachezwa kwenye uwanja huo.
"TFF imekaa na kufikiria upya na kuona kuna sababu za msingi kwa mechi ya Stars kuchezwa kwenye Uwanja wa Taifa kwa kuwa tayari tumetoa taarifa CAF pamoja na kwa wenzetu Algeria. Tumeiandikia barua Serikali kuomba kuutumia uwanja huo," alisema Wambura.
Alisema kuwa mbali na sababu hiyo, pia wameomba mechi hiyo ichezwe kwenye Uwanja wa Taifa ili kukwepa gharama za kuzisafirisha timu zote mbili, viongozi na waamuzi kwenda kucheza Mwanza.
Wambura alisema vilevile kuwa wamelazimika kuomba mechi hiyo ichezwe Dar es Salaam kwa kuwa tayari maofisa wa Algeria walishakuja nchini na kufanya maandalizi ya mchezo huo, ikiwa ni pamoja na kukagua hoteli watakayofikia.
PAZIA LA LIGI
Wakati klabu za Ligi Kuu zikipewa Sh. milioni 26.3 kila moja kwa ajili ya nauli na mdhamini wa ligi hiyo, kampuni ya huduma za simu ya Vodacom, msimu mpya wa ligi unaanza leo ambapo viwanja vitano vitatumika kwa timu 10 kati ya 14 za kuanza mbio za kuwania ubingwa wa ligi kuu msimu wa 2011/2012.
Kwenye uwanja wa Mkwawani mkoani Tanga, wageni wa ligi hiyo waliopanda daraja msimu huu, Coastal Union watawakaribisha Mtibwa Sugar wakati kwenye uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera, wenyeji Kagera Sugar wataonyeshana kazi na maafande wa Ruvu Shooting.
Kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, wenyeji Toto Africans watawakaribisha Villa Squad wakati kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, Polisi Dodoma watapambana na African Lyon ambao wataruhusiwa kucheza mechi hiyo endapo tu watawalipa wachezaji wao wawili, Abdul Masenga na Godfrey Kombo ambao wanaidai timu hiyo baada ya kuvunjwa kwa mikataba yao.
Kesho, timu iliyoshika nafasi ya tatu msimu uliopita ya Azam FC wataanza kuutumia kwa mara ya kwanza uwanja wao mpya uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam kwa kucheza dhidi ya Moro United. Wageni wa ligi hiyo, timu changa iliyoanzishwa miaka mitatu iliyopita ya ‘maafande’ wa JKT Oljoro watawakaribisha Simba kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha katika mechi ambayo ‘Wekundu wa Msimbazi’ watamkosa beki wa kati Kelvin Yondan aliyeachwa jijini Dar es Salaam baada ya kupatwa na jeraha la kidole kidogo cha mguu.
Mabingwa watetezi, Yanga watashuka dimbani kesho pia kucheza dhidi ya JKT Ruvu kwenye uwanja waliouteua kwa mechi zao za nyumbani wa Mkwakwani jijini Tanga. Katika hatua nyingine, TFF imeteua marefa 16 na wasaidizi 34 kwa ajili ya kuchezesha ligi hiyo ambayo bingwa huiwakilisha Tanzania Bara katika Ligi ya Klabu Bingwa Afrika huku mshindi wa pili akishiriki Kombe la Shirikisho.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment