ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, August 20, 2011

Mganga hawezi kukupa mume/mke sahihi, makala haya ni dawa - 2



Na Luqman Maloto
Huu ni mfungo mtakatifu wa Mwezi wa Ramadhan. Kiislamu ni moja kati ya nguzo tano lakini yenye thawabu nyingi kuliko nyingine nne zilizobaki. Hakika wema wa Mungu ni mkubwa kuliko chochote.

Hiki ni chungu cha 20, zimesalia siku 9 au 10 kieleweke. Karibu msomaji wangu ili tuelimishane kuhusu mambo mbalimbali yanayohusu mapenzi. Yanatuhusu wote, kwa hiyo ni vema tugawane elimu ndogo tuliyonayo.

Mada ni ile ile. Mganga hawezi kukupa mume/mke sahihi, makala haya ni dawa. Lengo ni kupeana muongozo ili kila mmoja wetu afurahie maisha ya uhusiano.

 Iweje wengine waingie kwenye ndoa na baadhi yetu tuikose?
Kuna msomaji wangu alinipa changamoto baada ya mada ya wiki iliyopita. Aliniambia kuna baadhi ya  watu ambao hawapati ndoa kwa sababu ya mipango ya Mungu lakini siyo hulka. Namuahidi kuwa nitaangalia makundi yote. 


Nilianza na kundi la kwanza wiki iliyopita. Hili kama nilivyoeleza ni kwamba linahusu aina ya watu ambao ni rahisi kuwaita vimbelembele ili kueleweka kwa upesi zaidi. Ni mwanamke lakini anaamini ana nguvu nyingi kuliko mwanaume.

Hajui kushuka chini daima, yeye ni mtu wa kupanda juu. Anasimamia dhana ya jino kwa jino. Hoja ya asilimia 50 kwa 50 inammeza. Badala ya kutambua haki zake na za mwenzake, anataka kuthibitisha ubabe wake.

Ni mwanamke lakini anataka awe na sauti yenye mamlaka na kumkoromea mwenzi wake anavyotaka. Akikaa na marafiki zake, anazungumza namna anavyoweza kukabiliana na wanaume kwa ubavu na kuwamudu. Anadhani sifa kumbe anaharibu sifa yake.
Kimsingi, mwanamke ambaye anapenda hulka za kibabe, mvuto wake hupungua kwa kiasi kikubwa. Wanaume humuogopa kwa hofu inayotokana na dhana kwamba mafahari wawili hawakai zizi moja.
Fikiria kwamba bado ni mnafahamiana lakini hata kucha hifichi. Jambo dogo, unanyukana na watu tena mbele yake. Anapokutuliza, badala ya kuona aibu au uache ugomvi kwa kumhofia, wewe ndiyo kwanza unamjibu: “Na wewe nipishe!”
KUNDI LA PILI

Linagusa aina ya watu ambao hawajui maana ya staha. Mtu hajui kutuliza miguu. Kama anafanya kazi ndiyo kabisa. Akitoka asubuhi kurudi ni usiku wa maneno. Muda mwingi anautumia kumbi za starehe na baa.

Hata kama wewe ni  mwanaume kwa mwanamke ambaye anafikiria zaidi maisha ya kifamilia, atakuona wewe siyo rafiki wa maendeleo. Atakuogopa, kwa hiyo utashangaa unazeeka bila ndoa.

Kwa maumbile ya binadamu, mwanaume anaendelea kubebwa na mfumo dume kwamba hata kama ni mtu wa kukesha baa lakini akiamua kuoa, atakataliwa na wawili wanaomjua, wa tatu ambaye haifahamu tabia yake atamkubali na ataitwa mume.

Kwa mwanamke ambaye ana hulka za kukesha baa ni msiba. Atasahauliwa na kila mwanaume ambaye atakutana naye. Hata wale ambao anakutana nao na kugongesheana glasi za kinywaji, siku wakitaka kuoa wataangalia kwingine.

Umri unapokwenda, atafikiria kuzaa kabla ya ndoa. Kundi hili ni baya, kwa hiyo inashauriwa mwanamke kudhibiti tabia yake ya ‘kukata kinywaji’. Kama hawezi kuacha, basi ni vema akapunguza na kusitisha tabia ya kukaa baa.

Mwanamke siku haipiti bila kuhudhuria klabu. Tena anajieleza waziwazi kwamba anahusudu kupita kiasi kwenda muziki nyakati za usiku na kurudi nyumbani alfajiri. Wanasema majogoo kwa lugha ya kimjini mjini. Hiyo ni hasara kubwa.

KUNDI LA TATU
Kuna aina ya watu ambayo inaamini kuwa fedha ni kila kitu. Wanaume ni wengi zaidi, kwa maana huamini kwamba uwezo wao unaweza kuwafanya wapate aina yoyote ya mwanamke. Hujidanganya sana.
Aina hii ya watu huwa hawapati mapenzi ya kweli. Huchunwa kama mabuzi. Hata wale ambao itawezekana kufunga nao ndoa, watakuwa nao kwa sababu ya malengo mengine si mapenzi. Kuchuma fedha na kuondoka.

Inawezekana mwanamke akawa kama kondoo kwenye uhusiano wake. Kila kitu atatii kwa unyenyekevu mkubwa. Si kwa sababu ya kuridhika na uhusiano uliopo, bali ni kwa suala zima la fedha. Ndoa ya namna hiyo siyo halisi.

Mwanamke wa aina hiyo anapoona amekamilisha kazi yake ya kuchuna buzi, huanza kufikiria jinsi ya kutoka kwenye ndoa. Anaweza kutafuta sababu kwa kulianzisha au kumtega mume wake, kwani hana cha kupoteza. Hakuwa na mapenzi ya kweli.

Aghalabu, hata kama hawataachana lakini mwanamke husika atakuwa na uhusiano na mwanaume mwingine nje ya ndoa yake. Sababu ni kwamba hana upendo wa dhati, kwa hiyo hawezi kuridhika na mume wake.
Kwa mwanamke ambaye atakuwa anaamini katika fedha zake ndiyo mtihani mkubwa. Anaweza kujenga kiburi kwa hisia kuwa anaweza kumnunua mwanaume yeyote. Watu wa aina hiyo wamefeli.

Tupo kwenye jamii moja, tunawaona wanawake wengi ambao wamekosa mapenzi ya dhati kutokana na fedha zao, wanakuwa watu wa kubeba vijana wadogo. Wanakosa heshima, wanaanza kuitwa mashugamami.
Itaendelea wiki ijayo.

www.globalpublishers.info

1 comment:

Anonymous said...

Bwana Luqman,
Mada yako imelenga kwenye kuwakejeli wanawake. Sioni tatizo la mwanamke kwenda Bar labda tu uniambie wanaume ndio pekee wanaostahili kwenda Bar. Kwenye suala la fedha. Kama huna fedha mwatakani kuoa? Mwanamke ana mambo mengi, vipozi, vigauni, nywele shurti zitengenezwe kimtindo yote hayo yataka fedha. Mke mzuri sabuni ya roho; wanapojipamba ni kwa ajili yetu SISI kinababa sasa kosa lao nini? Chanzo cha wanaume wengi kutafuta vimada ni kwasababu hawataki kuwapamba wake zao. Hakuna tabia isiyo na dawa!