ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, August 20, 2011

Misri itaondoa balozi wake Israil-BBC

Misri inasema kuwa imeamua kumuondosha balozi wake nchini Israel kwa sababu ya kuuwawa kwa askari wake wa usalama.
Wapalestina wanaangalia uharibifu kutokana na shambulio al Israil Gaza
Askari hao watano waliuwawa wakati wanajeshi wa Israil walipowaandama wapiganaji wa Palestina, ambao waliishambulia Israil Alkhamisi.
Huku nyuma Wamisri wameandamana mbele ya ubalozi wa Israil na kuchoma moto bendera ya Israil.
Misri imeilaumu Israil na imetaka kufanywe uchunguzi.
Israil imesema wanajeshi wake hawakuwa na makosa na kwamba itachunguza tukio hilo.

Taarifa ya serikali ya Misri inasema balozi wa Misri ataondoshwa hadi Israil itapochunguza vifo vya askari watano wa usalama wa Misri.
Jeshi la Israel limeahidi kufanya uchunguzi.
Misri imesema yaliyotokea ni kinyume na mkataba wa amani baina ya Israil na Misri.
Balozi wa Israil mjini Cairo ameitwa Wizara ya Mashauri ya Nchi za Nje kwa majadiliano zaidi.
Huku nyuma, waandamanaji nje ya ubalozi wa Israil mjini Cairo, wameipuuza taarifa iliyotolewa, na walipiga kelele na kuchoma moto bendera ya Israil.
Baadhi ya waandamanaji walibeba picha ya Hayati Rais Gamal Abdel Nasser, ambaye akijulikana kuwa dhidi ya Israil, na akitaka umoja wa nchi za Kiarabu.
Tangu mashambulio ya Alkhamisi, ndege za Israil zimeshambulia eneo la Gaza mara kadha, huku wapiganaji wa Kipalestina wameirushia Israil makombora zaidi ya 20.

No comments: