ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, August 21, 2011

Mkapa aliasa taifa


Rais Mstaafu wa awamu ya tatu,Benjamini Mkapa
Nora Damian
WAKATI mjadala wa Katiba mpya unaendelea kupamba moto nchini, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, aliishauri Serikali kuhakikisha kwamba, maoni ya Watanzania yanapewa nafasi ili kupata katiba inayokidhi matakwa ya wananchi. Rais Mkapa alisema hayo katika Mahafali ya Tatu ta Chuo cha Technolojia cha Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam jana na kuwataka wanataaluma na taasisi mbalimbali kutumia fursa hiyo kutoa maoni yao wakati huu wa kukusanya maoni ili yaingizwe kwenye katiba mpya.
 “Hivi sasa kuna mjadala wa kitaifa kuhusu katiba mpya, hivyo wanataaluma na taasisi mbalimbali mkiwemo nyie (wahitimu) ni wakati wenu kuingia kwenye mjadala huu,” alisema Mkapa na kuongeza:


“Kuna haja ya kuhakikisha haki na wajibu wa kila mtu unakuwepo kikamilifu katika katiba mpya”.
Pia aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi nakutoa mchango wao kuhusu munda kwa katiba wanayoitaka kwa manufaa ya kizazi hili na kijacho na inayokidhi mazingira ya sasa na ujao.
Hata hivyo, Mkapa ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo, alitoa wito kwa watu waheshimu wengine, mamlaka, kuheshimu wazee na kuthamini historia ya Tanzania.

“Tumia lugha ambayo inahimiza umoja wa kitaifa, kuheshimu watu wengine na epuka kutumia lugha yenye kuleta jazba,” Mkapa alisema na kuongeza:
“Lugha yako iwe kipimo cha maneno, sauti… kwani tabia na hoja za zinaweza kumfanya mtu aonekane kuwa ameelimika.”
 
Desemba mwaka jana, wakati wanasiasa na viongozi wastaafu nchini wakiwamo mawaziri wakuu wa zamani, Joseph Warioba na Frederick Sumaye na Jaji Mkuu Mstaafu, Agostino Ramadhan, wakitaka iundwe katiba mpya, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) Frederick Werema, alipinga wazo hilo na badala yake alitaka katiba iliyopo iwekewe viraka zaidi.
Madai ya katiba mpya pia yaliwahi kutolewa mwaka jana na Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini, John Tendwa, ambaye alisema bayana kuwa katiba mpya iandikwe mapema kabla ya mambo kuwa mabaya, huku akitoa mfano wa upungufu wa Katiba ya sasa, kuwa ni pamoja Rais kupewa madaraka makubwa.  Lakini, Werema alisema haoni haja ya kuandikwa katiba mpya badala yake katiba iliyopo iwekewe viraka.

“Kuandika katiba mpya hapana, lakini kufanya marekebisho kwa kuondoa au kuongeza mambo fulani kwenye katiba ruksa,” alisema Jaji Werema na kusisitiza:  "Suala la kubadilisha ibara zinazoonekana kutokidhi haja na kuingiza mambo mapya kwenye katiba, linakubalika na hayo yamekuwa yakifanyika,".

Jaji Werema alitolea mfano mabadiliko ya katiba yaliyoruhusu kuingizwa kwa haki za binadamu.  Hata hivyo, baada ya kuongezeka kwa joto la kuwepo katiba mpya lililokuwa likichochewa na wanaharakati pamoja vyama vya upinzani, Rais Jakaya Kikwete Desemba 31, mwaka jana alitangaza kuwa itauundwa kwa katiba mpya.
Aprili mwaka huu, wakati akitoa maoni yake katika kuboresha muswada wa sheria ya marekebisho ya katiba, Jaji Joseph Warioba, akisisitiza kuwa masuala yaliyoko Sehemu ya Tatu, kifungu cha 9(2), yajadiliwe bila zuio lolote.

Kifungu hicho cha muswada, kinataja mambo 8 ambayo ni marufuku watu kuyahoji au kuyazungumzia wakati tume ya kukusanya maoni ya watu juu ya katiba mpya itakapokuwa ikitekeleza majukumu yake.
Masuala hayo yanayoitwa kuwa ya 'heshima na utukufu', hivyo hayapaswi kuguswa kwa maslahi ya taifa, yameainishwa katika muswada kama ifuatavyo; Kuwepo kwa Muungano wa Tanzania na Zanzibar, kuwepo kwa mihimili mitatu ya dola (bunge, serikali na mahakama), nafasi ya urais, mshikamano wa kitaifa na amani ya nchi.

 Mengine ni; kuwepo kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kuwepo kwa mfumo wa uchaguzi wa kidemokrasia, haki za binadamu, dhana ya utu wa mtu, usawa mbele ya sheria na mfumo unaoweka utaratibu wa kufuata sheria, dhana ya Serikali ya Tanzania kutokuwa na dini na uhuru wa mahakama.
Hata hivyo, baada ya Serikali kuanzisha mchakato huo na kuupeleka kwa wananchi Muswada wa Sheria ya Mapitio ya Marekebisho ya Katiba wa mwaka 2011 , wananchi na vyama vya upinzani walipinga wakieleza kuwa suala hilo linaendeshwa bila ya kuwa na uwazi n kwamba upo katika lugha ya Kiingereza. 
Baadaye Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani, alisema tayari Muswada huo umeshaandikwa kwa Kiswahili na Serikali itatoa ratiba ya elimu kwa wananchi wote nchini kuhusu kilichomo kwenye Muswada ili kuondoa upotoshaji
Katika hafla hiyo, Mkapa aliwataka wahitimu hao kuondoa dhana ya kusubiri kuajiriwa na badala yake wajiajiri wenyewe kwani elimu waliyoipata katika chuo hicho inaweza kuwafanya wajiajiri.

 Mkapa alisema Tanzania ni nchi kubwa yenye ardhi inayosubiri kuendelezwa kwa kilimo na kwamba, kupitia mkakati wa ‘Kilimo Kwanza’ wahitimu hao wanaweza kuisaidia Serikali kufanikisha mpango huo.

Aliwataka wahitimu hao kutoridhika na elimu waliyoipata bali wajiendeleze zaidi kusoma kwani ndiko kutakakowawezesha kupata mawazo mapya.
 “Watu wengi wanafikiri kupata shahada na vyeti ndiyo mwisho wa kusoma na hata baada ya hapo hawajisomei tena,” alisema Mkapa.
Alifahamisha kuwa usomaji wa vitabu nchini uko chini ikilinganisha na nchi nyingine kama ya Kenya na Uganda na kwamba, hata maduka ya vitabu yaliyopo nchini ni machache.

“Niliingia katika darasa moja la wanafunzi 20, nikauuliza kama kuna mmoja wao aliyesoma kitabu mwezi uliopita, hakuna aliyenyoosha kidole.  Miezi mitatu iliyopita hakuna, miezi sita hakuna, na mwisho nilipouliza kama kuna aliyesoma kitabu mwaka uliopita ni mmoja tu alinyoosha kidole,” alisema Mkapa.

 Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo hicho, Padri Arul Raj, alisema chuo hicho kilicho chini ya Shirika la Kimataifa la Mabinti wa Maria Imaculata (DMI)  kilianzishwa mwaka 2004 kikiwa na wanafunzi 221 na kwamba hivi sasa kina wanafunzi 2,574.

Alisema wanatarajia kufungua vyuo vingine kama hivyo katika mikoa ya Mbeya na Mwanza na kwamba tayari wamewekeza Sh3 bilioni kwa ajili ya miundombinu mbalimbali ya chuo hicho.

Katika mahafali hayo jumla ya wanafunzi 172 walitunikiwa Shahada na Stashahada mbalimbali.

Mwananchi

No comments: