ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, August 28, 2011

Pinda akiri Bunge lilikuwa kali



Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amekiri kuwa Bunge lilikuwa kali ikilinganishwa na la 2005 na 2010 kutokana na michango iliyokuwa ya viwango na iliyofanyiwa utafiti hasa kutokana na idadi ya wasomi, viti vya upinzani kuongezeka na wabunge vijana kuwa wengi.
Alisema hayo wakati alipokuwa akihojiwa na Televisheni ya Taifa(TBC) juzi katika viwanja vya Bunge, mara baada ya kuliahirisha na kutakiwa kutoa maoni yake juu ya mwenendo mzima wa Bunge hilo.
“Sishangai nadhani sababu moja kubwa ni kwamba upande wa upinzani viti vyao vimeongezeka, lakini ndani yake vile vile unakuta wabunge vijana nao wamekuwa wengi,” alisema.
Hata hivyo, alisema mwelekeo unafanana kwani mwaka wa kwanza kila baada ya uchaguzi mkuu wabunge wanatoka majimboni wanakuwa wapya hawafahamiani.

“Nimekuwepo bungeni sasa kwa zaidi ya miaka kumi. Nimeliona lile la mwaka 2000, lilivyo na nimeliona 2005 na sasa tumeingia hili la 2010. Moja ambalo naliona ni kwamba mwelekeo unafanana,” alisema na kuongeza.
“Sasa kilichobadilika hapa ni scale, kiwango kwa safari hii kimekuwa kikali zaidi kuliko cha 2005 na kile cha 2000.”
Akifafanua Waziri Mkuu alisema kwa upande mwingine kiashiria kingine ni kuwepo kwa dalili kwamba wasomi wengi wameingia kwenye bunge… kwa hiyo wanachukua mwanya wa kujifunza mambo mengi na kutafiti vitu vingi kabla hawajazungumza.
“Utaona tu kwenye quality (kiwango) wakati wa michango yao, lakini walio wengi utakuta ni watu ambao wanaonekana kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa utambuzi na kueleza matatizo ambayo wanayaona. This is very good (hii ni nzuri sana) na ni positive element (jambo chanya) kwa upande wa wabunge.” Akizungumzia vyombo vya habari vilivyokuwa vikiripoti habari za Bunge kama vimetenda haki, Pinda alisema kuna televisheni, redio na magazeti na kila chombo kina mvuto wake.
Alisema kwa upande wa televisheni kazi imekuwa nzuri sana na wamejitahidi kuonesha kutokana na shughuli zilivyokuwa zikiendelea.
Hata hivyo, akigeukia magazeti ambapo aliyataka kuonyesha mambo mazuri kwa ajili ya mjadala wa nchi badala ya kujigawa katika makundi na kuonyesha wapi yametoka na yanamfanyia kazi nani.
“Tatizo la magazeti nadhani ni kwa sababu yamejigawagawa hivi katika makundi. Kwa hiyo wakati mwingine hayaku-reflect (kuonesha) sana sana kile ambacho tunadhani kingekuwa fundisho kwa wananchi badala yake yamejibu zaidi mwelekeo wa wapi umetoka na unamfanyia nani hiyo kazi,” alisema.
“Nadhani magazeti jambo hili waende waliangalie waone ni namna gani wanaweza ili waweze ku-reflect (kuonyesha) mjadala na yale mambo ambayo ni mazuri kwa ajili ya mjadala wa nchi yetu,” alisisitiza.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: