ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, August 28, 2011

Wapakistani 43 wauzwa viwandani


  Afisa Uhamiaji amwaga machozi
  Aliyewaingiza sasa akingiwa kifua
  Uhamiaji wamsaka aliyefichua siri
Afisa wa Idara ya Uhamiaji mkoa wa Dar es Salaam amejikuta akimwaga chozi kwenye ofisi za gazeti hili jana baada ya wenzake wanne kumgeuka na kukataa kuambatana naye kwenda kusaka Wapakistani walioingizwa nchini kinyemela na kuajiriwa kwenye kiwanda kimoja Jijini Dar es Salaam.
Hali hiyo inaashiria kuwa kwenye idara hiyo mambo siyo shwari kutokana na zoezi hilo kuvurugika kwa baadhi ya watumishi wake waliotumwa kufanya msako kukataa kwa madai kuwa watu hao hawahusiki na kwamba hawana hatia kwa sasa.

Tayari uchunguzi wa gazeti hili kwa wiki kadhaa sasa umebaini kuwa katika kipindi cha miaka
miwili, watu 43 kutoka nchini Pakistan wameingizwa nchini na kuuzwa viwandani wakiwa na vibali feki.
Idadi hiyo ni kwa kampuni moja tu inayojihusisha na biashara hiyo, Jijini Dar es Salaam ya Altaf &CO.PK ambapo inaelezwa idadi hiyo ni ndogo kulingana na uingizwaji wa watu hao kinyume cha sheria.
Hata hivyo, katika hali inayoonyesha mambo sio shwari ndani ya Idara ya Uhamiaji mkoa wa Dar es Salaam, zoezi la kuwakamata watuhumiwa hao limevurugika jana baada ya baadhi ya watumishi wa Idara hiyo kukataa kwenda kufanya kazi hiyo kwa madai watu hao hawahusiki na hawana hatia kwa sasa.
Afisa huyo (jina tunalihifadhi) katika hali inayoonyesha kukerwa, alitokwa machozi baada ya kusikia wenzake walikataa kwenda kwenye viwanda hivyo licha ya kupewa kibali cha kufanya kazi hiyo.
“Unajua nimefanya kazi kubwa mpaka tumefikia hali hii, leo tumefika hatua ya mwisho wenzangu wananiangusha hawataki kwenda,” alisikika afisa huyo akilalamika huku akitokwa machozi.
Toka awali maafisa hao walionyesha kutokuwa tayari na zoezi hilo baada ya kueleza siku mbili za nyuma walifanya kazi hiyo na baadhi yao walikamatwa kabla ya kuchukuliwa dhamana na waajiri wao.
Kauli hiyo ilipingwa vikali na afisa huyo ambaye alionekana kulifuatilia suala hilo kwa ujasiri mkubwa hadi ilipofika jana ndio ilikuwa siku maalum ya kwenda kuwakamata watu wawili ambao wangetoa picha halisi biashara hiyo.
Hata hivyo imeelezwa Mkuu wa Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam, Abdallah Hamisi alitoa kibali cha kukamatwa kwa watu hao baada ya kutambua kazi nzuri iliyofanywa na afisa huyo katika kuchunguza suala hilo kwa undani.
Katika uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa wiki kadhaa imefahamika kampuni inayotuhumiwa kuhusika na biashara hiyo ya Altaf &CO.PK imejihusisha kuwachukua raia kutoka nchini Pakistani na kuwaingiza nchini na kujikusanyia sh. milioni 430.
Vielelezo ambavyo gazeti hili linavyo vinaonyesha kuanzia mwanzoni mwa mwaka jana hadi Mwezi Mei mwaka huu jumla ya watu 43 (majina tunayo) wameingizwa nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere kwa kutumia vibali bandia.
Imeelezwa wakiwa hapa nchini watu hao walipelekwa katika viwanda vya kutengenezea nondo vya hapa nchini, DRC na Burundi huku kila mmoja alitakiwa kulipa Sh. milioni 10 kwa kampuni hiyo.
Viwanda vya hapa nchini vinavyodaiwa kunufaika na biashara hiyo ni pamoja na Iron Steel, Simba Steel vya jijini Dar es Salaam na Nyakato Steel cha jijini Mwanza.
Aidha biashara hiyo ambayo imeelezwa inamwingizia faida kubwa mfanyabiashara huyo inaelezwa inafanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa baraka za baadhi ya maofisa wa uhamiaji ambao kwa namna moja au nyingine wananufaika na biashara hiyo.
“Wakiingia hapa nchini wanatengezewa vibali na baadhi ya maofisa wa uhamiaji na baadaye wanapelekwa kwenye viwanda husika na kuanza kufanya kazi,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo cha habari kinaeleza Wapakistani hao wanaendelea kufanya kazi katika kampuni hizo bila ya wasiwasi licha ya kubainika ukweli kuwa hawana uhalali wa kufanyakazi hapa nchini.
MMILIKI WA ALTAF&CO.PK AJULIKANA
Mtu ambaye anamiliki Kampuni ya Altaf&Co.PK amejulikana kwa jina la Altaf Hussein ambaye ana uraia wa Pakistani na anafanya kazi katika kampuni ya Iron Steel kama fundi.
Taarifa kutoka Idara ya Uhamiaji inaeleza Altaf anaishi nchini kwa kutumia kibali cha daraja B kama mfanyakazi wa kawaida na sio vinginevyo. Hata hivyo akiwa hapa nchini anajitambulisha kama mfanyabiashara wa usambazaji wa vipuri na mitambo kutoka Pakistani.
Licha ya kuvunja sheria na kuhusishwa na biashara hiyo cha kushangaza Idara ya Uhamiaji imekuwa na kigugumizi cha kumtia mbaroni.
Aidha katika uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwenye kiwanda hicho, ilifahamika kuwa muda mwingi anautumia kwa ajili kusafiri kwenda Pakistani na siku chache zilizobaki ndizo anakuwepo kiwandani hapo.
“Huyu mtu kwa kawaida anakaa hapa kiwandani siku chache sana, mara nyingi anakuwa yupo nje na hatujui anakwenda kufanya nini,” Alisema mfanyakazi mmoja mara baada ya kuulizwa.
ALTAF AFANYIWA MBINU YA KUMUONDOA KWENYE KASHFA.
Katika hali ya kushangaza, taarifa zinaeleza viongozi wa viwanda vinavyotuhumiwa na biashara hiyo wanafanya juhudi kubwa ya kuhakikisha Altaf anatolewa kwenye sakata hilo, badala yake tuhuma zote apewe mtu aliyetoboa siri hizo (Jina tunalihifadhi).
Mbinu hiyo imeonekana kuzaa matunda baada ya Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam kutangaza rasmi kumsaka mtu huyo na kuahidi kutoa zawadi nono kwa mtu atakayefanikisha kukamatwa kwake.
Kutajwa kwa mtu huyo kuwa ni mtu muhimu kwa kuhusika kuwaingiza na kuwapatia vibali watu hao imekuja baada ya Mkurugenzi wa Kiwanda kimoja kutoa ripoti zisizo za kweli kwamba kazi ya kufoji vibali na kuingizwa nchini kwa watu hao imefanywa na yeye wakati alipokuwa akifanya kazi katika moja ya viwanda hivyo.
Hata hivyo, katika nyaraka zote zilizozifikia gazeti hili inaonyesha jinsi jina la mtu huyo lisivyohusika, bali nyaraka zote zinaonyesha jinsi Altaf alivyohusika kikamilifu katika kuwachukua Wapakistani hao kutoka nchini mwao hadi Tanzania kwa kugushi vibali mbalimbali.
Katika baadhi ya vibali hivyo inaonyesha saini ya Altaf na jinsi Kampuni ya Altaf&CO.PK ilivyowarubuni raia hao kwa kuonyesha wanapelekwa Marekani na Afrika Kusini kufanya kazi na badala yake waliletwa hapa nchini na kugawanywa kwenye viwanda hivyo.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: