Kago ruksa kucheza, Jangwani watishia nyau
Hata hivyo, Kago aliyesaini mkataba wa kuichezea Simba Julai 13 mwaka huu akitokea klabu ya Olimpic Real de Bangui ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, amepata ruhusa ya kuichezea Simba leo tu na sio kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara itakayoanza Jumamosi hadi pale uhamisho wake utakapokamilika kwa kutumia mfumo mpya wa mtandao (TMS) unaotakiwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Akizungumza jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF, Alex Mgongolwa, alisema kuwa kamati yake imefikia maamuzi ya kumruhusu mchezaji huyo kwa kuzingatia mambo matatu, ambayo ni; mechi hiyo kuwa maalumu kwa ajili ya kuichangia jamii (Ngao ya Jamii) na vilevile kuwa ni ya kufungua msimu mpya wa ligi ya Bara.
Mgongolwa alisema vilevile kuwa sababu nyingine iliyofanya kamati yake imruhusu Kago kucheza leo ni nia iliyoonyeshwa na Simba ya kufanya usajili wa mchezaji huyo kwa njia ya mtandao (TMS) kama kanuni za uhamisho wa kimataifa zinavyoelekeza.
Alisema kwamba Simba ambayo pia imelipeleka FIFA suala la usajili wa Kago, itatakiwa kukamilisha usajili wa mchezaji huyo wakati wa kipindi cha dirisha dogo kama ibara ya 2 (2) ya kanuni za uhamisho za FIFA zinavyoeleza na wala si vinginevyo.
Alisema kuwa Simba inalazimika kutumia mfumo wa TMS kwa sababu imemsajili Kago kama mchezaji wa kulipwa na si ridhaa, na kuongeza kwamba kauli ambazo zilikuwa zinatolewa na uongozi wa klabu hiyo kwamba Jamhuri ya Afrika ya Kati haijaanza kutumia TMS si sahihi.
"Kanuni za FIFA ziko wazi, Zinaeleza kwamba wachezaji wa kiume watahamishwa kwa TMS, ni lazima uhamisho mwingine hautatambulika," alisisitiza Mgongolwa.
Naye Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alisema kwamba juzi jioni shirikisho hilo lilipokea barua kutoka Simba, ikionyesha ni jinsi gani walikuwa wakifanya jitihada za kumhamisha Kago kwa njia ya TMS, lakini klabu aliyotoka mshambuliaji huyo ikishindwa kujaza taarifa walizotakiwa.
KAULI YA SIMBA
Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema kwamba klabu yake imefurahishwa na maamuzi yaliyotolewa na TFF juu ya mshambuliaji wao na kuongeza kwamba leo kikosi chao kitashuka uwanjani kikiwa kamili kwa ajili ya kusaka ushindi.
Kamwaga alisema kuwa hivi sasa, Simba hawana pingamizi na wanawaomba mashabiki wa soka nchini kujitokeza uwanjani kwa wingi ili kushuhudia watakavyolipiza kisasi cha kufungwa na Yanga wakati walipokutana kwenye fainali ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame).
Aliongeza kwamba ili kuhakikisha kwamba wanamaliza utata wa usajili wa Kago, jana, mwenyekiti wao Ismail Aden Rage aliondoka nchini na kwenda Jamhuri ya Afrika ya Kati kukamilisha zoezi hilo na hatimaye Kago apatiwe leseni ya kuichezea timu yao.
Rage aliiambia NIPASHE kwa njia ya simu kutokea Jamhuri ya Afrika ya Kati jana mchana kuwa tayari ameshaanza mazungumzo na viongozi wa klabu ya Olimpic Real de Bangui ili kukamilisha zoezi hilo chini ya msaada wa maafisa wa FIFA ambao wanalifahamu suala hilo.
Alisema anaamini kuwa upo uwezekano FIFA ikatoa ITC na Kago akaichezea Simba kwenye msimu ujao na si kusubiri hadi kipindi cha usajili wa dirisha dogo.
YANGA WATISHIA NYAU
Huku kukiwa na taarifa zinazothibitisha kuwa klabu za Yanga na Simba zilipokea malipo yao yote ya mechi ya leo ambazo ni Sh. milioni 80 kwa kila moja, uongozi wa Yanga ulitishia nyau jana kwa kusema kuwa hautapeleka timu yao uwanjani kama hawatalipwa fedha wanazoidai TFF.
Akizungumza jana kwenye makao makuu ya klabu hiyo, Afisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu, alisema kuwa wanaitaka TFF iwalipe fedha hizo kabla ya saa 5:00 asubuhi leo na kwamba, kinyume chake hawatacheza mechi hiyo ya Ngao ya Jamii.
Sendeu alisema kuwa fedha hizo wanazoidai TFF ni malimbikizo yao yaliyotokana na mashindano ya Kombe la Kagame na kiasi kingine ni fedha anazostahili kupata kipa wao, Yaw Berko, aliyeibuka kipa bora wa msimu uliopita ambao Yanga walitwaa ubingwa.
Alipoulizwa kuhusu madai hayo ya Yanga, Osiah alisema hawajapata taarifa rasmi ya jambo hilo.
MAKOCHA SIMBA, YANGA
Makocha Moses Basena wa Simba na Sam Timbe wa Yanga, kila mmoja ameahidi kwamba timu yake itacheza kwa umakini ili iibuke na ushindi.
Basena alisema kwamba ushindi katika mechi ya leo utasaidia kurudisha morari ya kikosi chake na itakuwa ni dalili njema kwa msimu mpya.
Timbe alisema kuwa mechi ya leo itakuwa ngumu kama mechi nyingine walizocheza dhidi ya Simba na hiyo inatokana na kila upande kuwa na maandalizi mazuri.
WAAMUZI
TFF imesema kuwa mmoja kati ya marefa Oden Mbaga na Israel Nkongo atachezesha mechi ya leo, akisaidiwa na Jesse Erasmo wa Mbeya na Hamisi Chang'walu wa jijini Dar es Salaam.
Mechi hiyo itaanza saa 2:00 usiku na itatanguliwa na mechi ya timu za vijana za umri chini ya miaka 20 za Simba B dhidi na Yanga B.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment