NAINUA mikono yangu juu, kwa heshima zote, nikimrudishia Mungu wangu sifa heshima na utukufu. Yeye ni kila kitu katika maisha yangu, bila msaada wake, hakika siwezi kuwa kama nilivyo leo! Nakusihi nawe msomaji wangu mpenzi, jenga utaratibu wa kumshukuru Mungu kwa kila jambo.
Nakukaribisha kwa moyo mkunjufu katika safu yetu ambayo inakupa mwanga juu ya namna ya kuishi vyema katika uhusiano wako. Hapa ni sehemu sahihi ya kupata darasa la maisha na mapenzi. Ukiwa mdau wa ukurasa huu, mapenzi hayatakutesa kamwe.
Nakukaribisha kwa moyo mkunjufu katika safu yetu ambayo inakupa mwanga juu ya namna ya kuishi vyema katika uhusiano wako. Hapa ni sehemu sahihi ya kupata darasa la maisha na mapenzi. Ukiwa mdau wa ukurasa huu, mapenzi hayatakutesa kamwe.
Nazungumzia juu ya kuwa na mwenzi halafu ukawa huna uhakika kama anakupenda kwa dhati au la! Wiki iliyopita nilianza kwa kuelezea kipengele cha kwanza kabisa.
Nilisema zipo hatua za kufanya ambazo kama ukizitumia vyema itakuwa rahisi kwako kugundua kama mwenzi uliyenaye anakupenda kwa dhati au anakupotezea muda.
Katika vipengele nilivyovigawa kwa nyakati na siku, leo tutaingia katika awamu ya mwisho. Hebu twende tukaone.
KWANINI UCHUNGUZE?
Kipengele cha kwanza wiki iliyopita, tuliona unavyotakiwa kuonesha mapenzi yako yote, jinsi unavyomjali na kumthamini kila siku. Kuwa kiongozi wa siku yake, mfanyie manjonjo yote unayoyajua. Lengo hapo ni kumuweka sawa!
Kwa kufanya hivyo, hata kama alikuwa na mpango wa kukutana na patina mwingine, nafsi itamsuta, maana kila baada ya muda mfupi, simu yake huingiza SMS kutoka kwako. Meseji ambazo bila shaka zitakuwa na ujumbe wa mapenzi, kutokana na hilo, siyo rahisi kuingiwa na hisia za kufanya kitu kibaya, vinginevyo atakuwa hakupendi. Kama ndivyo, kwa nini uendelee kuteseka?
Lazima utambue kitu kimoja muhimu katika hili, unapaswa kufanya haya yote, bila kujali kuwa anaonesha kukupenda au hapana! Zingatia kuwa unapaswa kumpigia simu, mara tano au zaidi kwa siku na kumtumia SMS kumi au zaidi kwa siku, bila kusahau kuwa unapaswa kumtupia waraka pepe mara moja au zaidi kwa siku.
Lengo ni kumfanya awe karibu na wewe kila wakati, apende asipende na hiyo ndiyo shabaha yako. Ninachomaanisha hapa ni kumfanya aone kuwa wewe ni sehemu ya maisha yake, sehemu ya siku yake, bila wewe siku haiwezi kukamilika.
WEKA MITEGO
Baada ya kuona mambo ya msingi ya kuzingatia katika siku tatu za mwanzo ikiwa ni pamoja na shabaha ya kuchunguza, sasa tugeukie katika kipengele kingine. Hapa ni vyema kumwekea mitego. Nikisema hivyo nimaanisha mitego ya kimapenzi.
Kumbuka kuwa tayari umeshamsogeza karibu yako, hafurukuti kwa lolote, umemfanya aishi unavyotaka, ni kama hawezi kufanya kitu chochote kabla hujampa maelekezo, sasa mtege!
Usifanye kitu chochote kwa nia ya kumwonesha mapenzi, badala yake kaa kimya. Ingia katika kipindi cha ukimya. Usimwandikie SMS waraka pepe wala kumpigia simu, acha yeye afanye mambo hayo. Usithubutu kumfanyia kitu chochote, naomba hapo nieleweke vizuri. Hupaswi kufanya mawasiliano ya aina yoyote na yeye.
Kumbuka kuwa umeshamfanya aishi unavyotaka, sasa atakapoona anakosa SMS, waraka pepe au simu kutoka kwako, ni hapo sasa atakapoamua kukupigia au kukutumia SMS. Hata akikutumia SMS usijibu. Akikuandikia waraka pepe hivyo hivyo, ila akipiga simu pokea lakini epuka kumuita kwa majina ya kimapenzi.
Mshangaze katika hilo, labda kama akiomba umwite jina la kimapenzi ndiyo ufanye hivyo, lakini wewe kama wewe usithubutu kufanya hivyo. Akihitaji mkutane pamoja kubali, lakini si katika mambo yanayohusiana na chumbani.
UMEGUNDUA NINI?
Hata mgonjwa anapotumia dawa zikiisha lazima aangalie kama amepata nafuu. Sasa hapa unatakiwa kuangalia kama umegundua chochote kutoka kwa mpenzi wako huyo anayeutesa moyo wako. Kwa mambo uliyomfanyia kwa muda wote huo lazima atahisi kuna matatizo katika kipindi cha ukimya wako.
Kama anakupenda, atakutafuta na wakati mwingine atahitaji mkutane kwa ajili ya mazungumzo ya faragha, hapo sasa ndipo atakapokueleza ukweli wa penzi lake, lakini kama hakupendi, hatashtuka na atakuacha, kwa sababu SMS, waraka pepe na simu zako zilikuwa zinampotezea muda.
Jiulize, kama ulikuwa unamkera, kuna sababu gani ya kuwa na mtu ambaye hana mapenzi ya dhati kwako? Hapo ni mwanzo wa utumwa ambao mwisho wake ni mbaya.
Lengo la uchunguzi huu ni kutafuta ukweli wa penzi lake kwako, sasa kama hakupendi huna sababu ya kumng’ang’ania, achana naye, anza maisha mapya huku ukisubiri penzi la dhati kwa mpenzi atakayejali thamani ya penzi lako. Ni kweli ni uamuzi mgumu lakini wenye masilahi na maisha yako ya baadaye.
Kikubwa ulichokuwa unakihitaji ni kugundua ukweli wa kilichokuwa kikiendelea kati yenu. Matokeo yake unatakiwa kuyafanyia kazi na kufanya uamuzi ambao kamwe huwezi kuujutia.
Nawashukuru sana kwa kunisoma wapendwa wasomaji wangu, nawaomba msikose wiki ijayo kwa mada nyingine kali zaidi.
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia magzeti ya Global Publishers. Amendika vitabu vya True Love na Let’s Talk About Love. Kwa makala zaidi tembelea; www.globalpublisherstz.com
No comments:
Post a Comment