Advertisements

Saturday, August 13, 2011

Simba, Yanga sasa kucheza saa 2 usiku

Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura
Mechi ya kuwania Ngao ya Jamii kati ya watani wa jadi, Simba na Yanga itakayofanyika Jumatano kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam imeuzwa kwa mmiliki wa vituo vya kuuzia mafuta vya Big Bon na sasa itachezwa kuanzia saa 2:00 usiku.

Habari zilizopatikana kutoka ndani ya uongozi wa klabu za Simba na Yanga zinasema kwamba watakuwa tayari kusaini mkataba wa kuuza mechi hiyo kwa gharama ya Sh. milioni 300.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, viongozi hao walisema kwamba wataridhia makubaliano na Big Bon kwa kiasi hicho cha fedha na wala si vinginevyo.
Walisema kuwa endapo fedha hiyo ikipatikana, kila timu itaambulia Sh. milioni 84 huku pia wakitaka kupunguza kutoka asilimia 10 hadi tano ya kuchangia mfuko wa uchunguzi wa saratani ya matiti wa Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA).
Kiongozi mmoja wa Simba alisema kwamba watakubali kupatiwa kiasi hicho cha fedha kwa sababu ya kuangalia mazingira yanayoizunguka siku ya mchezo wao.
Alisema kwamba mechi ambayo ilizikutanisha klabu hizo na kuingiza mapato ya juu ni ya fainali ya Kombe la Kagame iliyochezwa Julai 10 mwaka huu, lakini hawana uhakika kama watapata kiasi kama hicho Jumatano, siku isiyokuwa ya mwisho wa wiki.
"Mechi ikichezwa Jumamosi au Jumapili hutoa nafasi kwa watu wengi wa Dar es Salaam na mikoa ya karibu kuhudhuria, lakini Jumatano, walioko mikoani wanaweza kushindwa kuja kuiona kwa sababu siku inayofuata watatakiwa kuwahi kwenye maeneo yao ya kazi," alisema kiongozi huyo wa Simba.
Kwa upande wa Yanga, walisema vilevile kuwa kiasi hicho kwao ni muafaka na ndio wanaweza kukubali na si chini ya hapo kwa sababu huenda pia mapato yakavuka malengo.
Alisema kwamba hali hiyo ya kupata mnunuzi itawasaidia pia viongozi kuweka mawazo yao kwenye kuiandaa timu na kujiondoa kwenye usimamizi wa mapato.
Akizungumza jana, Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema kuwa shirikisho limekubaliana na maombi yaliyotolewa na viongozi wa Simba na Yanga na sasa mechi hiyo imeamuliwa kuchezwa kuanzia saa 2:00 usiku.
Wambura alisema kwamba wamekubali kufanya mabadiliko kwa kuzingatia kwamba mchezo huo unachezwa katika kipindi cha mfungo wa Ramadhani na tena katika siku ya kazi.
Alisema vilevile kuwa kabla ya watani hao kukutana, jioni kuanzia saa 10:30 kutakuwa na mechi ya kutangulizi kati ya timu za vijana za umri chini ya miaka 20 za Simba B na Yanga B.
Taarifa zimeongeza kuwa, kama TFF, Simba na Yanga watafikia makubaliano na mnunuzi huyo, leo ndio watasaini mkataba maalumu na kutangaza taratibu nyingine za mechi hiyo.
KAGO HATIHATI
Mshambuliaji mpya wa Simba, Gervas Kago kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati, yuko katika hatihati ya kuwavaa mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Yanga, katika mechi yao ya Jumatano kutokana na utata wa kibali chake cha uhamisho wa kimataifa (ITC).
Taarifa zilizopatikana jana, zilieleza kuwa chanzo cha utata wa ITC ya Kago ni mfumo uliotumiwa na chama cha soka nchini mwake ambacho kimetuma kwa njia ya faxi badala ya kutumia mfumo wa kielektroniki (TMS) unaotambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Habari zaidi kutoka ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) zimedai kuwa tayari viongozi wa Simba wametakiwa kushughulikia suala hilo kabla ya Kago kuruhusiwa Jumatano.
Mshambuliaji huyo ni muhimu katika kikosi cha Simba kwani ni mhimili muhimu wa safu mpya ya ushambuliaji ya Simba inayoundwa pia na Mzambia Felix Sunzu.
MWAPE APONA
Wakati kiungo Mganda wa Yanga, Hamis Kiiza akiwa mbioni kuadhibiwa kwa kosa la kuondoka nchini bila ruhusa na kutimkia kwao, mchezaji mwingine wa kimataifa wa ‘Wanajwangani’, Mzambia Davis Mwape amepona na anatarajiwa kuwemo katika kikosi kitakachoivaa Simba Jumatano.
Afisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu alisema kuwa Mwape ameshaanza mazoezi, lakini Kiiza ataadhibiwa kwa sababu alitoa taarifa ya kuondoka kwake wakati tayari akiwa uwanja wa ndege, akidai kwamba anakwenda kumtazama mjomba wake ambaye ni mgonjwa.
CHANZO: NIPASHE


No comments: