
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Samuel Sitta
WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amezitaka mamlaka za dola kuwafukuza kazi, viongozi wakiwamo mawaziri wenzake waliojilimbikizia mali kwenye biashara kupitia nafasi zao.
“Nchi imebaki mifupa mitupu huku wananchi wake wakiteseka kwa kushindia mlo mmoja na wengine wakiishi kwa kuokota vyakula majalalani, wakati huo baadhi ya watu wachafu wakiwamo viongozi wao wanaendelea kuneemeka bila kujali maisha duni ya mwananchi,” alisema mjini hapa katika ufunguzi wa Kongamano Vijana wa Kikristo kutoka nchi za Afrika Mashariki.
Sitta alisema kama mamlaka hizo hazitachukua uamuzi mgumu kwa kuwakabili watendaji wake wenye utajiri wa kutisha, nchi itaendelea kuwa maskini na wananchi watabaki na maisha magumu.
Kauli ya Waziri Sitta inakuja kipindi kifupi baada ya kuingia kwenye mjadala na baadhi ya makada wa chama chake cha CCM wakiwamo mawaziri alipoitaka Serikali iwaombe radhi wananchi kutokana na tatizo la umeme.
Akizungumza katika kongamano hilo, Sitta alisema anakerwa kuona kiongozi wa Serikali akipigana vikumbo na wafanyabiashara wadogo kwenye zabuni mbalimbali zinapotangazwa.
Sitta alisema haiwezekani kiongozi kama waziri serikalini ajiingize kwenye biashara ndogondogo za vioski akishindana na wafanyabiashara wadogo kwenye maeneo yao maalumu ambao mitaji yao ni midogo inayohitaji kuongezewa nguvu.
Alizitaka mamlaka hizo husika kufuatilia kwa makini vyanzo vya mapato vya viongozi hao ikiwa ni pamoja na kuchunguza akaunti zao mara kwa mara ili kuona kama zinaendana na vipato vyao, hali ambayo itasaidia kubaini ubadhirifu wa fedha za umma.
Alisema wapo baadhi ya viongozi wanaofanya biashara ambao wamekuwa wakidiriki hata kuingiza majina mengi ya watu kwenye mikopo ya fedha kwa maendeleo ya vijana na kuacha vijana walengwa kukosa mitaji.
"Inakera kumwona mtu ni waziri lakini inapotokea mikopo ya fedha za maendeleo kwa vijana na yeye anaingiza mkono wake anaweka majina kama 10. Kwa hiyo kama mkopo ni Sh5milioni yeye anazoa Sh50milioni vijana wengine walengwa wanakosa," alisema Sitta.
Alisema Tanzania siyo nchi ya kuwa maskini kutokana na rasilimali nyingi zilizopo lakini hali hiyo imekua kutokana na baadhi ya viongozi waliopo madarakani kutozingatia maslahi ya wananchi na kukumbatia wajanja wachache wanaojilimbikizia mali huku wakiwa huru pasipo kuchukuliwa hatua na mtu yeyote.
"Mimi ninachoishauri mamlaka husika za dola ni kwamba, iwachukulie hatua kali viongozi watakaobainika kukutwa na fedha nyingi zisizoeleweka na sheria ichukue mkondo wake kwani watu hawa ndiyo wanaifanya nchi na wananchi kwa ujumla kubakia maskini siku hadi siku huku wao wakizidi kufaidika tu," alisema Sitta.
Sitta alisema kwamba kuna watu wanaopenda kujilimbikizia mali bila kuangalia tabaka dogo la wanyonge wakiwamo vijana kitu ambacho ni cha hatari, kwani vijana wamekuwa wakitajwa kuwa mhimili wa nguvukazi ya taifa lakini yanapokuja maslahi yao wapo wakubwa wanaojaribu kuyapora.
Hata viongozi wa Afrika
Alisema hata baadhi ya viongozi wa Afrika wamekuwa wakijilimbikizia mali wanapokuwa madarakani na wanapokuja kuachia madaraka wamekuwa wakigundulika kuwa na utajiri wa kutisha, kitu ambacho kimekuwa kikichangia nchi za bara hili kuendelea kuwa maskini.
Alisema viongozi wa aina hiyo ni vyema wakaumbuliwa mapema kabla hawajaitafuna nchi na kuiacha ikiwa na umaskini wa kutupwa huku wananchi wake wakiendelea kuteseka siku hadi siku.
Awali, Askofu wa Kanisa la Spiritual Transformation la mjini hapa ambao ndiyo waandaaji wa kongamano hilo, Askofu Francis Mnkande alisema lengo lake ni kuwajenga vijana kiroho na kimaisha hasa ya kiuchumi ili waweze kujikwamua na hali ngumu.
Askofu Mnkande alisema kongamano hilo la wiki moja linalenga pia kuwajengea uwezo vijana hao kuwa viongozi waadilifu na wenye kumcha Mungu katika maisha yao watakapokuwa viongozi hali itakayosaidia kuondokana na changamoto mbalimbali za uadilifu zinazowakabili viongozi walio wengi madarakani.
Kongamano kama hilo linalokutanisha mamia ya vijana hufanyika mara moja kwa mwaka na tayari limekwishafanyika Uganda na Kenya na mwakani linatarajiwa kufanyika nchini Rwanda.
Mwaka huu, zaidi ya vijana 500 walihudhuria wakitokea nchi za Kenya, Rwanda, Uganda, Burundi, Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) ambao waliomba kushiriki.
1 comment:
hata wewe umeshiriki kula hizo nyama za nchi iliyobakia mifupa bwana.
Post a Comment